Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakuu wa Umoja wa mataifa wakemea ukatili wa kijinsia nchini Sudan

Hawaye Ibrahim, mkimbizi wa Sudan nchini Chad, anasema wanamgambo walivamia nyumba yao huko Darfur nchini Sudan ambapo walimuua mume wake, wakamjeruhi mtoto wake huku wakitumia fimbo kumchapa sikio la kushoto na hadi sasa ana maumivu.
UNHCR Video
Hawaye Ibrahim, mkimbizi wa Sudan nchini Chad, anasema wanamgambo walivamia nyumba yao huko Darfur nchini Sudan ambapo walimuua mume wake, wakamjeruhi mtoto wake huku wakitumia fimbo kumchapa sikio la kushoto na hadi sasa ana maumivu.

Wakuu wa Umoja wa mataifa wakemea ukatili wa kijinsia nchini Sudan

Wanawake

Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa hii leo wameeleza kushtushwa na kulaani ripoti zinazoongezeka za unyanyasaji wa kijinsia unaoendelea nchini Sudan, ikiwa ni pamoja na ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro dhidi ya wakimbizi wa ndani na wakimbizi wanawake na wasichana tangu kuzuka kwa mapigano mwezi Aprili 2023.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na mashirika matano kutoka Geneva Uswisi na New York Marekani imetaka kukomeshwa mara moja kwa unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na kuacha kuutumia kama mbinu ya vita na kuwatisha watu na kutaka kuongezwa kwa haraka huduma za kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia nchini Sudan na pia katika nchi jirani, ambako wale wanaokimbia ghasia wametafuta usalama kama wakimbizi, ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.

Mashirika hayo ni lile la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, linalohudumia Wakimbizi (UNHCR), la Kuhudumia Watoto (UNICEF), la Idadi ya Watu na Afya ya uzazi (UNFPA), linashughulika na masuala ya wanawake UN Women na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO).

Martin Griffiths, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Kibinadamu na Mratibu OCHA Martin Griffiths amesema wanachoshuhudia nchini Sudan sio tu janga la kibinadamu bali ni mgogoro wa ubinadamu “Ni jambo lisiloeleweka kwamba wanawake na watoto wa Sudan - ambao maisha yao yamechochewa na mzozo huu usio na maana - wanapata kiwewe zaidi kwa njia hii.”

Kamishna Mkuu wa OHCHR Volker Türk amesema uchunguzi wa haraka na wakina unapaswa kufanyika bila upendeleo kwa madai yote ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Tunapokea ripoti za kushangaza za unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana, ikiwa ni pamoja na ubakaji. Na baada ya ukatili huo, wanawake na wasichana wanaachwa na msaada mdogo wa matibabu na kisaikolojia. Lazima kuwe na kutovumilia kabisa unyanyasaji wa kijinsia. Wahusika wote lazima wawajibishwe.” Amesema Türk

Wakuu wote wa mashirika ya UN wamesisitiza pande zote lazima ziheshimu wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na sheria za haki za binadamu kulinda raia, wakiwemo wanawake na wasichana, ikiwa ni pamoja na kuruhusu njia salama kwa walionusurika kupata huduma za afya na wafanyakazi wa afya kufika kwenye vituo vya afya.

Kusoma zaidi nini kimesemwa na wakuu wa mashirika ya UN WOMEN, WHO, UNFPA, UNICEF na UNHCR bofya hapa.

Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR limeeleza kunasikitishwa na ripoti zinazoendelea za raia nchini Sudan, wakiwemo wakimbizi wa ndani na wakimbizi waliokumbwa na mzozo unaoendelea, wamekuwa wahanga wa mauaji ya kiholela wa mapigano na kuzuiwa kutafuta usalama.

Taarifa ya shirika hilo kutoka Geneva Uswisi imesema mpaka sasa imethibitishwa kuwa tarehe 25 Juni mwaka huu, wakimbizi 28 waliokuwa wakishikiliwa na Sudan waliuawa mjini Khartoum wakati eneo walimokuwa wakiishi lilipokumbwa na mapigano, huku wakimbizi wengine wakijeruhiwa katika tukio hilo.

UNHCR imetuma rambirambi zake kwa familia zilizoathirika.