Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukingo wa Magharibi: UNICEF na OHCHR wakemea mashambulizi ya Israel mjini Jenin

Kambi ya wakimbizi ya Jenin inapakana na manispaa ya Jenin na ndiyo kambi ya kaskazini kabisa katika Ukingo wa Magharibi.
© UNRWA/Dominiek Benoot
Kambi ya wakimbizi ya Jenin inapakana na manispaa ya Jenin na ndiyo kambi ya kaskazini kabisa katika Ukingo wa Magharibi.

Ukingo wa Magharibi: UNICEF na OHCHR wakemea mashambulizi ya Israel mjini Jenin

Amani na Usalama

"UNICEF ina wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa ghasia za hivi karibuni huko Jenin, katika Ukingo wa Magharibi.” Anasema Adele Khodr, Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wakati Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk akisema vurugu huzaa tu vurugu zaidi. Mauaji, kulemaza watu na uharibifu wa mali lazima vikomeshwe. 

Kwa mujibu wa ripoti za kufikia juzi Jumatatu watoto wasiopungua watatu walikuwa wameshauawa na wengine wengi kujeruhiwa, huku mamia ya familia zikikosa makazi kutokana na mapigano yanayoendelea na wakati huo katika kambi ya wakimbizi wa ndani, huduma muhimu, kama vile maji na umeme, zimekatizwa. 

Adele Khodr amenukuliwa katika taarifa iliyosambazwa jana akisema, “UNICEF inachukizwa na vitendo vyote vya ukatili dhidi ya watoto na inataka kukomeshwa mara moja kwa unyanyasaji wa kutumia silaha. Watoto lazima daima walindwe dhidi ya aina zote za unyanyasaji, na ukiukwaji mkubwa, na pande zote zina wajibu wa kulinda raia - hasa watoto - kulingana na sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu." 

Haki za binadamu 

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ambaye ndiye Mkuu wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) akitoa maoni yake kuhusu mashambulizi haya amesema kwamba vurugu huzaa tu vurugu zaidi. Mauaji, kulemaza watu na uharibifu wa mali lazima vikomeshwe. 

Anasema usiku wa kuamkia juzi Wapalestina 3,000 waliripotiwa kukimbia kambi ya Jenin baada ya wimbi la mashambulizi ya anga kwenye kambi hiyo. Kisha, asubuhi ya jana Jumanne watu saba walijeruhiwa katika shambulio la kugonga gari huko Tel Aviv. 

“Kiwango cha operesheni inayoendelea ya Kikosi cha Usalama cha Israeli huko Jenin, pamoja na utumiaji wa mashambulizi ya anga ya mara kwa mara, pamoja na uharibifu wa mali, inaibua masuala mazito yanayohusiana na kanuni na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, pamoja na kulinda na kuheshimu haki ya maisha.” Amesema Turk. 

Baadhi ya mbinu na silaha zilizotumiwa wakati wa operesheni za ISF katika Kambi ya Wakimbizi ya Jenin na maeneo ya jirani kwa ujumla wake zinahusishwa zaidi na uhasama katika migogoro ya silaha, badala ya utekelezaji wa sheria. Matumizi ya mashambulizi ya anga hayaendani na sheria zinazotumika katika uendeshaji wa shughuli za utekelezaji wa sheria. Katika muktadha wa uvamizi, vifo vinavyotokana na mashambulizi hayo ya anga vinaweza pia kuwa mauaji ya kukusudia. Operesheni za jeshi la Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu zinahitaji kuzingatia viwango vya kimataifa vya haki za binadamu kuhusu matumizi ya nguvu; viwango hivi havibadiliki kwa sababu tu lengo la operesheni hiyo limetajwa kama "kukabiliana na ugaidi"

Sheria ya kimataifa ya haki za binadamu inaweka wazi wajibu kwa Israeli, kama mamlaka inayokalia, kuhakikisha kwamba shughuli zote zinapangwa na kudhibitiwa ili kupunguza, kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo, kutumia nguvu na hasa nguvu mbaya. Israel ni lazima pia ihakikishe upatikanaji wa matibabu kwa wakati kwa wale wote waliojeruhiwa.