Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na washirika wake watembelea kambi ya wakimbizi ya Jenin iliyoharibiwa vibaya

Operesheni hiyo ya siku mbili ya jeshi la Israel, ambayo ilijumuisha mashambulizi ya anga katika jumuiya hiyo yenye wakazi wengi, ilisababisha kiwango kibaya zaidi cha uharibifu kuwahi kutokea katika zaidi ya miaka 20 katika kambi ya Jenin.
© UNRWA/Tareq Shalash
Operesheni hiyo ya siku mbili ya jeshi la Israel, ambayo ilijumuisha mashambulizi ya anga katika jumuiya hiyo yenye wakazi wengi, ilisababisha kiwango kibaya zaidi cha uharibifu kuwahi kutokea katika zaidi ya miaka 20 katika kambi ya Jenin.

UN na washirika wake watembelea kambi ya wakimbizi ya Jenin iliyoharibiwa vibaya

Wahamiaji na Wakimbizi

Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa na washirika wafadhili Jumapili walitembelea kambi ya wakimbizi wa Kipalestina katika mji unaokaliwa wa Ukingo wa Magharibi wa Jenin, ambapo wameshuhudia uharibifu wa kushtua uliofanyika wakati wa uvamizi wa Israeli wiki hii iliyopita.

Operesheni hiyo ya kijeshi ya siku mbili ndiyo kali zaidi katika kipindi cha miaka 20, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA.

Takriban watu 12 waliuawa, wakiwemo watoto wanne, na wengine 140 walijeruhiwa pia takriban nyumba 900 ziliharibiwa, na nyingi sasa haziwezi kukalika tena.

"Tumekwenda kwenye kambi ya Jenin na washirika wetu kuonyesha mshikamano na wakaazi na kuwahakikishia kuwa hawako peke yao," amesema Leni Stenseth, naibu kamishna mkuu wa UNRWA.

Kiwewe, uchovu na hofu

Ujumbe huo pia ulijumjumuisha Adam Bouloukos, mkurugenzi wa ofisi ya Ukingo wa Magharibi wa shirika hilo, na Lynn Hastings, mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa na  wa misaada ya kibinadamu. 

Waliandamana pia na wawakilishi kadhaa wakuu kutoka jumuiya ya kimataifa na wafadhili.

Bi Stenseth  ameongeza kuwa "Uharibifu niliouona ulikuwa wa kushangaza. Baadhi ya nyumba ziliteketea kabisa, magari yalikuwa yamesambaratishwa kwa kuta, barabara zimeharibiwa, kituo cha afya cha UNRWA kimeharibiwa pia. Lakini, zaidi ya uharibifu wa kimwili, nimeona kiwewe machoni pa wakazi wa kambi ambao walikuwa wameshuhudia vurugu. Nimewasikia wakizungumza kuhusu uchovu na woga wao.”

Madarasa yamesalia patupu

Kwa mujibu wa UNRWA takriban watu 24,000 wanaishi katika Kambi ya Wakimbizi ya Jenin, ambayo iko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi. 

Kituo cha afya cha UNRWA hapo kimeharibiwa vibaya kiasi kwamba hakiwezi kutumika tena, na shule zake nne zilipata uharibifu mdogo, shirika hilo lilisema.

Wakati baadhi ya wanafunzi walikuwa wamerudi darasani siku ya Jumapili, mahudhurio yalikuwa ya chini sana, huku baadhi ya wazazi wakiripoti kwamba watoto wao walikuwa wakiogopa sana kuondoka nyumbani kwao na hivyo kuyaacha madarasa mengi kusalia patupu.

Bwana. Bouloukos amesema wajumbe hao walitembelea darasa ambalo wanafunzi waliwaeleza kwamba siku 10 tu zilizopita, walikuwa wamemzika mwanafunzi mwenzao aliyeuawa katika uvamizi wa awali. 

Alisema ni vigumu sana kwa watoto kutembea kwenda shuleni kwani barabara kuu bado hazitumiki.

“Wakati wa kujaribu kutafuta njia mbadala za kwenda shuleni, baadhi ya watoto wadogo walipotea njia. Kwa kweli tulihofia usalama wao kwa sababu ya hatari za vilipuzi ambayvo havikulipuka. Kipaumbele sasa ni kutoa msaada wa afya ya akili na kisaikolojia ili kuwasaidia watoto kukabiliana na woga na wasiwasi wao,” ameongeza.

Shughuli za usafi zinaendelea

UNRWA imesema kambi ya wakimbizi ya Jenin imeshuhudia ghasia kali katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, huku mwaka 2023 ukiwa mbaya zaidi.

"Kambi hiyo kwa sasa haina umeme na maji. Takriban kilomita nane za mabomba ya maji na kilomita tatu za njia za maji taka ziliharibiwa kutokana na matumizi ya mashine nzito zilizorarua sehemu kubwa za barabara." amesema Bouloukos.

Shughuli kubwa za kusafisha zinaendelea, na UNRWA imepongeza mamlaka za mitaa na manispaa kwa juhudi zao katika suala hili.

Watu wapatao 3,500 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na operesheni hiyo ya kijeshi. 

UNRWA imesema kipaumbele ni kusaidia kurejesha hali ya kawaida kwa wakazi kwa kurejesha huduma zake za msingi kambini katika masuala kama vile elimu, afya, usafi wa mazingira, na kutoa msaada wa fedha kwa familia.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limewataka wafadhili na washirika kutoa fedha mara moja kwa ajili ya kutekeleza hatua zake za kibinadamu katika kambi hiyo.

Bi. Stenseth pia amesisitiza hitaji kubwa la amani katika maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu "kupitia suluhisho la kisiasa linalohitajika sana ambalo pia litashughulikia changamoto ya wakimbizi wa Kipalestina".