Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jenin: UN ina wasiwasi kuhusu mashambulizi ya kijeshi yanayofanywa na Israel

Ukuta uliojengwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi.
UN News/Shirin Yaseen
Ukuta uliojengwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi.

Jenin: UN ina wasiwasi kuhusu mashambulizi ya kijeshi yanayofanywa na Israel

Amani na Usalama

Mashambulizi ya ardhini na angani yanayoendelea katika mji wa Jenin eneo la Palestina linalokaliwa kwenye Ukingo wa Magharibi, yanaendelea kuleta wasiwasi kuhusu maisha ya watu.  

Kabla ya leo, jana Jumatatu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea wasiwasi wake mkubwa ambapo mashambulizi ya anga ya Israel yamepiga kambi ya wakimbizi iliyo na watu wengi. 

Katika taarifa iliyotolewa mjini New York, Marekani, Guterres alithibitisha kwamba operesheni zote za kijeshi lazima zifanywe kwa heshima kamili ya sheria za kimataifa za kibinadamu. 

Huduma muhimu za kibinadamu 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) hii leo Jumanne nalo limesema linasikitishwa na ukubwa wa operesheni za angani na ardhini zinazoendelea huko Jenin hii ikiwa ni operesheni ya pili katika Jenin inayohusisha mashambulizi ya anga ndani ya wiki mbili. 

Msemaji wa OCHA Vanessa Huguenin hii leo mjini Geneva, Uswisi amewaeleza wanahabari kwamba “Hadi leo asubuhi, Wizara ya Afya ya Palestina imethibitisha vifo vya Wapalestina kumi wakiwemo watoto watatu. Takriban wengine mia moja wamejeruhiwa, kati yao ishirini wanaripotiwa kuwa katika hali mbaya." 

Msemaji huyo wa OCHA amefafanua zaidi kuwa mashambulizi ya anga pia yameharibu kwa kiasi kikubwa majengo ambayo watu walikuwa wakiishi katika kambi na katika maeneo ya jirani. Kutokana na uharibifu wa miundombinu, “sehemu kubwa ya kambi ya Jenin kwa sasa haina maji ya kunywa na makadirio ya kwanza yanaonyesha kuwa sehemu kubwa ya kambi hiyo pia haina umeme.” 

Hali ya afya ni tete Jenin 

Kwa upande wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), Msemaji wake, Christian Lindmeier, amesema, "Kiwango cha majeraha kinaweka matatizo katika mfumo dhaifu wa afya wa Jenin. WHO inafanya kazi na timu za afya ili kusaidia uanzishaji wa Mpango wa Dharura wa Hospitali ya Jenin,” na uhamasishaji wa vifaa vilivyowekwa tayari kwa ajili ya kuhudumia wanaopatwa na kiwewe. 

“Magari ya kubebea wagonjwa na watoa huduma yamezuiwa kuingia sehemu za kambi ya wakimbizi, ikiwa ni pamoja na kuwafikia watu ambao wamejeruhiwa vibaya.” Ameeleza Msemaji wa WHO akiongeza kuwa, “Kwa sasa hakuna ushoroba au eneo salama kwa ufikiaji wa misaada ya kibinadamu, ambayo ni lengo kuu la mazungumzo yanayoendelea ya Umoja wa Mataifa.”  

Aidha Christian Lindmeir amesema kuwa tayari Wizara ya Afya ya Palestina imewasilisha vifaa vya matibabu vinavyohitajika haraka, ambayo inakaguliwa na WHO na wadau wa afya. 

Uvamizi huu wa sasa unakuja baada ya operesheni nyingine katika kambi hiyo tarehe 19 Juni, ambayo ilisababisha Wapalestina wanne kuuawa na wengine 91 kujeruhiwa.