Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na wadau kubeba jukumu la kuongoza mpango wa bahari safi wenye thamani ya dola milioni 115

Samaki wakiogelea kuzunguka mwamba wa matumbawe katika Bahari Nyekundu karibu na pwani ya Misri.
Coral Reef Image Bank/Alexander
Samaki wakiogelea kuzunguka mwamba wa matumbawe katika Bahari Nyekundu karibu na pwani ya Misri.

FAO na wadau kubeba jukumu la kuongoza mpango wa bahari safi wenye thamani ya dola milioni 115

Tabianchi na mazingira

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO pamoja na mashirika manne wadau, wamepewa jukumu la kuongoza mpango wa pamoja wa bahari safi na zenye afya, ambao ni mradi unaolenga kuanzia kwenye chanzo taka hadi baharini  ambao utaelekeza ruzuku ya hadi dola milioni 115 kuzisaidia nchi kukabiliana na uchafuzi wa mazingira ya pwani na mfumo mzima wa Maisha ya baharí. 

Uamuzi huo umefanywa katika mkutano wa 64 wa baraza la kituo cha mazingira duniani GEF, ambacho hutoa ufadhili wa fedha ili kukabiliana na upotevu wa bayoanuwai, mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira, na changamoto zingine za mazingira ya nchi kavu na afya ya bahari.

FAO inasema “Bahari zimepoteza karibu asilimia 2 ya oksijeni yake tangu miaka ya 1950, na kusababisha maeneo yaliyokufa yajulikanayo kama hypoxia ambayo hayawezi kusaidia viumbe vya baharini. 

Uchafuzi kutoka kwenye vyanzo vya ardhi, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mbolea, hewa ukaa inayotokana na mifugo, na maji machafu ya manispaa na viwandani ambayo hayajasafishwa, kwa kawaida husababisha hypoxia duniani kote. “

Mashirika hayo yamesema programu hii inalenga kuboresha mazoea endelevu kwa ekari 200,000 za ardhi na ekari milioni 14.3 za makazi ya baharini.

Malengo ya ziada ni pamoja na kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuboresha usimamizi katika zaidi ya mifumo mikubwa mitatu ya ikolojia na kupunguza tani milioni 5.6 za uzalishaji wa gesi chafuzi.