Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNODC Kenya na wadau wazindua awamu ya pili ya mradi mbadala wa kusaka haki

Uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa mbinu mbadala za kudumisha haki nchini Kenya, PLEAD 2 iliyofanyika Safari Park Hotel jijini Nairobi. PLEAD inafadhiliwa na UNODC, Umoja wa Ulaya na serikali ya Kenya.
©UNODC Kenya

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na mihadarati na dawa za kulevya, UNODC, imezindua awamu ya pili ya mradi mbadala wa kusaka haki ulio na azma ya kukwepa mfumo wa kushtakiana mahakamani, PLEAD 2. 

Wafungwa wa jela ya Langata wakiwatumbuiza wageni kwenye uzinduzi wa kituo cha ushauri nasaha kwa maafisa wa magereza.
UN News/Thelma Mwadzaya
Wafungwa wa jela ya Langata wakiwatumbuiza wageni kwenye uzinduzi wa kituo cha ushauri nasaha kwa maafisa wa magereza.

Awamu ya kwanza ya PLEAD ilijikita katika kuhakikisha kila mhusika anapata haki kwa kuziwezesha taasisi za serikali kutimiza hilo ima kwa kutumia teknolojia au pia mazungumzo ya suluhu katika jamii. 

Soundcloud

Mwanzoni wa mwezi Mei mwaka huu, awamu ya pili ya mradi mbadala wa kusaka haki, PLEAD 2 ilizinduliwa jijini Nairobi. Lengo kuu ni kuzishirikisha taasisi zaidi ya serikali kupambana na ufisadi na kudumisha haki kupitia idara ya mahakama na polisi.Mradi wa PLEAD unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa kupitia mashirika ya UNDP la maendeleo na afisi ya kupambana na mihadarati ya UNODC. 

Kwenye uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa haki wa PLEAD, Jaji Mkuu wa Kenya Martha Koome alibainisha kuwa, “mpango huo utasogezwa mbele na mafanikio ya awamu ya kwanza na dhamira ni kuimarisha utimizaji wa haki katika sekta ya mahakama na jamii.” 

Wawakilishi wa UNODC, idara ya mahakama  na usalama ya Kenya waliohudhuria uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa PLEAD 2 kwenye hoteli ya Safari Park jijini Nairobi.
©UNODC Kenya
Wawakilishi wa UNODC, idara ya mahakama na usalama ya Kenya waliohudhuria uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa PLEAD 2 kwenye hoteli ya Safari Park jijini Nairobi.

PLEAD 2 inadhamiria kutimiza mahitaji ya haki na kuondoa vikwazo vinavyoathiri utoaji wa huduma hiyo katika sekta husika. “Matumizi ya teknolojia kusawazisha utoaji wa haki Pamoja na kupambana na ufisadi ni nguzo muhimu za awamu hii ya pili ya mradi wa PLEAD,” anafahamisha Michael Lusweti, Afisa wa mradi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na mihadarati na dawa za kulevya, UNODC

Wakenya wanaohitaji kutimiziwa haki wamepewa kipaumbele wakiwemo pia walio katika hatari ya kutengwa na kusahauliwa. Malengo kamili ya mradi wa PLEAD 2 ni kuuwezesha mfumo wa kupambana na uhalifu, kuupiga vita ufisadi kwa njia bora zaidi, kuimarisha utekelezaji na uratibu kwenye sekta ya haki, kuimarisha utendaji, ubora na kasi ya taasisi za kupambana na uhalifu pamoja na kupata usaidizi wa kisheria. Mradi huu umefadhiliwa na mchango wa Umoja wa Ulaya na kutekelezwa na Umoja wa Mataifa kupitia ofisi ya kupambana na mihadarati, UNODC na shirika la maendeleo la UNDP.

Taarifa hii imeandaliwa na Thelma Mwadzaya.