Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNITAMS imesikitishwa na kulaani vikali mauaji ya Gavana wa West Darfur

Tarehe 27 mwezi Aprili mwaka 2023, shule ya Al-Imam Al-Kadhim kwenye mji wa Al-Geneina jimbo la Darfur Magharibi nchini Sudan, ambayo imekuwa hifadhi kwa wakimbizi wa ndani iliteketezwa kwa moto wakati huu ambapo mapigano yanaendelea nchini Sudan.
Mohamed Khalil

Amani na Usalama

 Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kusimamia kipindi cha mpito nchini SUDAN, UNITAMS umelaani vikali mauaji ya Gavana wa jimbo la Darfur Magharibi Khamis Abdullah Abbaker yaliyotekelezwa hapo jana  kwenye mji wa El Geneina na kutaka wale wote waliohusika kufikishwa mbele ya sheria. 

Taarifa ya UNITAMS imesema mashahidi mbalimbali wameeleza mauaji hayo yametekelezwa na kikundi cha wanamgambo wa RSF ingawa wamekataa kuhusika na mauaji hayo. 

Mpango huo umesema kifo cha marehemu Khamisi Abdullah Abbaker aliyekuwa mpatanishi mkuu katika jimbo hilo na ndiye alitia saini mkataba wa amani wa Juba ni cha kujutiwa na kusikitisha.

UNITAMS imetoa wito kwa wahusika wote wa mauaji hayo kufikishwa mahakamani haraka na kuzuia kuongezeka kwa mzunguko wa ghasia katika eneo hilo. 

“Tunatoa wito wa hekima kwa watu wa Sudan kutovutwa na kutumbukia katika katika wimbi la kauli za chuki na mgawanyiko wa kikabila.”

Wakimbizi kutoka Sudan wakipata hifadhi chini ya miti katika vijiji kilometa 5 ndani ya mpaka wa Chad
© UNHCR/Aristophane Ngargoune
Wakimbizi kutoka Sudan wakipata hifadhi chini ya miti katika vijiji kilometa 5 ndani ya mpaka wa Chad

UNITAMS pia imekemea vikali ongezeko la operesheni za kijeshi na mapigano yanayoendelea huko Darfur na inataka kusitishwa mara moja kwa operesheni zote za kijeshi ili kupunguza hali ya mambo kuwa mbaya zaidi, kukabiliana na ongezeko la ghasia za kikabila, kuruhusu upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na kuzuia hali kuzorota zaidi ambayo inaweza kusababisha ghasia kubwa na migogoro mikubwa zaidi.

UNITAMS imewakumbusha wahusika wote  katika mzozo huo wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu ili kuhakikisha usalama na ulinzi wa raia. “Uhalifu na ukiukaji uliofanywa wakati wa mzozo huu hautapuuzwa na haupaswi kupita bila uwajibikaji.” Umesisitiza mpango huo na kuongeza kuwa “Watu wa Sudan wanastahili amani, usalama, na heshima kubwa kwa haki zao za kibinadamu.”