Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Baraza Kuu la UN ahimiza Sudan kusitisha mapigano

Rais wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi.
UN Photo/Loey Felipe
Rais wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi.

Rais wa Baraza Kuu la UN ahimiza Sudan kusitisha mapigano

Amani na Usalama

Rais wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi amelaani vikali kuzuka upya kwa ghasia na mapigano nchini Sudan.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kutoka jijini New York Marekani Kőrösi amesema “Ninaeleza masikitiko yangu makubwa kwa watu kupoteza maisha na majeruhi, ikiwa ni pamoja na raia wengi, wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kibinadamu na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.”

Rais huyo wa UNGA77 amesema ongezeko lolote zaidi la mapigano hayo litakuwa na athari mbaya kwa nchi na kanda.

“Naungana na wito wa Katibu Mkuu (wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres) kwa pande zote za Sudan kusitisha mara moja uhasama na kuanzisha mazungumzo bila kuchelewa ili kuondokana na tofauti na kurejea kwenye njia ya mpito ya kidemokrasia.”

Rais huyo wa Baraza Kuu amesema yuko tayari kuunga mkono juhudi zozote za kuleta amani.