Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa kuimarisha jukumu muhimu la wanawake katika kukabiliana na kauli za chuki umezinduliwa na OSAPG

Matamshi ya chuki, yawe ya mtandaoni au nje ya mtandao, ni tishio kwa demokrasia na haki za binadamu.
Unsplash/Dan Edge
Matamshi ya chuki, yawe ya mtandaoni au nje ya mtandao, ni tishio kwa demokrasia na haki za binadamu.

Mpango wa kuimarisha jukumu muhimu la wanawake katika kukabiliana na kauli za chuki umezinduliwa na OSAPG

Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Mshauri Maalum wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari (OSAPG) leo, imezindua mpango mpya ulioundwa ili kutoa mwongozo wa kuimarisha nafasi ya wanawake katika kukabiliana na kauli za chuki, na kuzuia uchochezi wa ghasia ambao zinaweza kusababisha uhalifu wa kikatili.

Mpango huo mpya wa kijasiri umezinduliwa siku chache kabla ya maadhimisho ya pili ya kimataifa ya siku iliyopitishwa na na Umoja wa Mataifa ya kupinga kauli za Chuki.

Mpango huo wa utekelezaji kwa wanawake katika jamii ambao pia unajulikana kama “Mpango wa Utekelezaji wa Wanawake wa Napoli katika jamii” umetokana na mashauriano ya mwaka mzima na wanawake kutoka duniani kote ambao wananafanya kazi katika nyanja za kupinga kauli za chuki na kuzuia uhalifu wa ukatili.

Lengo kubwa ni kuwawezesha wanawake kuchangia kwa utaratibu na kwa kiasi kikubwa kukabiliana na janga hilo na kuzuia kutekelezwa kwa vitendo vya uchochezi wa kikatili.

Changamoto kubwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika hotuba yake kwenye hafla ya uzinduzi huo iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa ofisi ya Katibu Mkuu Courtenay Rattray.

Taarifa hiyo imesema "Kwanza, kuzuia uhalifu wa kikatili, mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita, mauaji ya kikabila na uhalifu dhidi ya ubinadamu bado ni changamoto ya muda mrefu na ni kiini cha dhamira ya Umoja wa Mataifa,”

"Pili, uhalifu wa kikatili una mwelekeo wa kijinsia, kwa hivyo juhudi za kuzuia na kukabiliana nao lazima pia zizingatie jinsia," ameongeza mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akisisitiza umuhimu mkubwa wa mpango huo kwa sababu mbili:

Mpango wa Utekelezaji wa Wanawake wa Napoli katika Jamii uliandaliwa kwa mtazamo wa wanawake, ambao walichangia kujumuisha sauti na uzoefu wa wanawake.

Kushindwa kuunga mkono

"Tunahitaji kufikiria upya jinsi tunavyokabiliana na kuzuia, tukianza kwa kukiri kwamba tumeshindwa kuwajumuisha wanawake na kuunga mkono jukumu lao katika kuzuia mauaji ya halaiki na uhalifu mwingine wa kikatili," amebainisha mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari Alice Wairimu Nderitu, ambaye pia ni msimamizi wa Umoja wa Mataifa kuhusu kauli za Chuki.

Maoni yake yaliungwa mkono na mwakilishi wa kudumu wa Italia kwenye Umoja wa Mataifa, Maurizio Massari, ambaye pia ni makamu wa Rais wa Baraza la uchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC.

Balozi Massari ameongeza kuwa "Ikiwa tunataka kujumuisha kikamilifu mtazamo wa wanawake na kukuza mipango inayoongozwa na wanawake inayolenga kukabiliana na kauli za chuki, lazima tuhakikishe kwamba sauti zao zinasikika na hata zaidi kwamba sauti zao zijumuishwe kwenye meza ambapo maamuzi yanachukuliwa,"

Majadiliano juu ya Mpango wa Utekelezaji wa Wanawake wa Napoli katika jamii yalianza Napoli, Italia, na mkutano ulioitishwa na OSAPG, tarehe 13 na 14 Juni 2022, ambao ulikuwa chanzo cha hati ya sera ya Jumatatu, ikiwataka wadau wote wanaohusika kuhakikisha kuwa wanawake wanashirikishwa, wana fursa ya kujihusisha, au kuwa na uwezo unaoongezeka wa kushiriki katika kukabiliana na kauli za chuki na kuzuia uchochezi wa ghasia ambao unaweza kusababisha uhalifu wa kikatili.