Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusimame kidete dhidi ya ongezeko la chuki na  kutovumiliana: Guterres

Kuashiria Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda (2019).
UN Photo/Violaine Martin
Kuashiria Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda (2019).

Tusimame kidete dhidi ya ongezeko la chuki na  kutovumiliana: Guterres

Amani na Usalama

Wakati dunia ikiadhimisha kumbukumbu ya kutisha ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda mwaka 1994, ambapo Wahutu na wengine waliopinga mauaji hayo waliuawa pia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kizazi baada ya matukio hayo ya kutisha, “tusisahau kamwe kilichotokea na hakikisha vizazi vijavyo vinakumbuka kila wakati."

Katika ujumbe wake wa siku hii ya Kimataifa ya kutafakari mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda yalyotokea mwaka 1994ya na kukumbukwa kila mwaka Aprili 7 António Guterres amesema "Tunaomboleza zaidi ya watoto milioni moja, wanawake na wanaume ambao waliangamia katika siku mia moja za kutisha miaka 29 iliyopita".

Guterres ameendelea kusema "Tunaheshimu kumbukumbu za waathiriwa Watutsi walio wengi, lakini pia Wahutu na wengine waliopinga mauaji ya kimbari. Tunatoa pongezi kwa ujasiri wa walionusurika. Tunatambua safari ya watu wa Rwanda kuelekea uponyaji, kurejea katika hali ya kawaida, na upatanisho. Na tunakumbuka kwa aibu kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa."

Kuanzia kauli za chuki hadi uhalifu wa chuki

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa  ameongeza kwamba, "Kizazi baada ya mauaji ya kimbari, hakipaswi kamwe kusahau kilichotokea na kuhakikisha vizazi vijavyo vinakumbuka kila wakati jinsi matamshi ya chuki kwa urahisi yalivyo kiashiria muhimu cha hatari ya mauaji ya kimbari inageuka kuwa uhalifu wa chuki na jinsi kupuuza ukatili ni inavyokuwa kuushiriki. Hakuna mahali, na hakuna wakati ambao unakinga dhidi ya hatari ikiwa ni pamoja na wakati wetu.”

Simama kidete dhidi ya kutovumilia

Bwana Guterres amesisitiza kwamba kuzuia mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita, na ukiukaji mwingine mkubwa wa sheria za kimataifa, ni jukumu la pamoja na jukumu la msingi la kila mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Akitoa wito kwa kila mtu, katika mataifa yote, kusimama kidete dhidi ya kuongezeka kwa hali ya kutovumiliana, kuwa macho daima na tayari kuchukua hatua amehitimisha ujumbe wake kwa kusema "Na tuheshimu kumbukumbu ya Wanyarwanda wote walioangamia kwa kujenga mustakabali wa utu, usalama, haki, na haki za binadamu kwa wote.”

Hafla ya kumbukumbu ya kuadhimisha miaka 29 ya mauaji ya kimbali dhidi ya Watutsi nchini Rwanda zitafanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York siku ya Ijumaa, Aprili 14, zikijumuisha hotuba za Katibu Mkuu, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na maafisa wengine pamoja na ujumbe wa mtu aliyenusurika katika mauaji hayo ya kimbari.

Uwekaji wa shada la maua na kuwasha mishumaa, pamoja na sherehe inayojumuisha taarifa kutoka kwa maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa na ushuhuda kutoka kwa walionusurika, itafanyika pia katika ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Geneva Alhamisi ya 13 Aprili.