Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maafa ya mafuriko ya Ukraine: mahitaji yanaongezeka huku athari za muda mrefu zikijongea 

Malori matano yalipeleka msaada kwa Bilozerka, mojawapo ya jamii zilizoathirika zaidi na mafuriko yaliyosababishwa na mlipuko wa Bwawa la Kakhovka nchini Ukraine.
© UNOCHA
Malori matano yalipeleka msaada kwa Bilozerka, mojawapo ya jamii zilizoathirika zaidi na mafuriko yaliyosababishwa na mlipuko wa Bwawa la Kakhovka nchini Ukraine.

Maafa ya mafuriko ya Ukraine: mahitaji yanaongezeka huku athari za muda mrefu zikijongea 

Haki za binadamu

Hali ya kibinadamu baada ya kuharibiwa kwa bwawa la Kakhovka nchini Ukraine bado ni "lengo linaloongezeka", mahitaji ya haraka ni "makubwa", na wasiwasi unaongezeka kuhusu siku zijazo, kwa mujibu wa afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Denise Brown.

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Bilozerka, mji ulioko kwenye Mto Dnipro takriban kilomita 20 magharibi mwa Kherson na kilomita tano kutoka mstari wa mbele wa vita, Bi. Brown ambaye ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu, amesema kuwa leo Ijumaa, Umoja wa Mataifa umeletamsafara wa lori tano Kwenda maeneo yaliyoathirika, wakipeleka maji ya kunywa, chakula na vifaa vinavyohitajika sana kusaidia ukarabati wa nyumba zilizoharibika. 

Bi Brown amekuwa akizuru maeneo yaliyoathiriwa na kusema kuwa watu walishitukizwa kabisa na mafuriko hayo yaliyotokea Jumanne usiku wa manane baada ya bwawa hilo kupata ubovu mkubwa. Ukraine na Urusi zimelaumiana kwa uharibifu wake. 

Ametembelea Bilozerka, ambapo OCHA ilipeleka lori 5 kwa mojawapo ya jamii zilizoathiriwa zaidi na mafuriko yaliyosababishwa na mlipuko wa Bwawa la Kakhovka. 

"Kwa zaidi ya watu 700 wamelazimika kuondoka katika jamii hii ya watu 6000 na kuhamia mjini. Msaada wa kibinadamu ulitolewa siku ya kwanza. Chakula na maji vilikuwa hapa. Timu zetu ziko hapai, kusaidia jamii, kusaidia serikali za mitaa. Lakini jamii hii imepigwa kihalisi na makombora. Na sasa imepigwa kwa mafuriko yaliyosababishwa na uharibifu wa bwawa, ambao unasababishwa na vita. Ni kiwango kisichovumilika cha mateso. Lakini tuko hapa kusaidia.” 

Ongezeko la mahitaji 

Katika maeneo mengi, maji bado hayajapungua, ndiyo maana athari imebaki kuwa ngumu kuitathmini na picha za satelaiti ni "mbaya", Bi. Brown amesema.  

Ofisi ya kuratibu misaada ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema Alhamisi kwamba mafuriko bado yatadumu "angalau kwa wiki moja"

Kwa sasa, takriban watu 17,000 wameathirika katika eneo la mafuriko kulingana na Bi. Brown.  

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) Shabia Mantoo ameongeza kuwa idadi hii inaweza kuongezeka hadi 40,000 kadri hali inavyoendelea. 

Kuhusu malalamiko ya Rais Zelenskyy 

Alipoulizwa kutoa maoni yake juu ya ukosoaji wa hapo awali kutoka kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy wa juhudi za Umoja wa Mataifa za kutoa misaada, Bibi Brown amesema kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na la Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wamekuwa wakileta misaada "tangu siku ya kwanza" kwa kutumia magari ya kukodi na kwamba UNHCR na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM) pia walikuwa katika maeneo ya tukio. 

“Nimeuliza swali hilo kwa wenye mamlaka wa Ukraine, ‘Je, tulifika hapa kwa wakati unaofaa?’ Na jibu lilikuwa ndiyo,” akasema. 

Bi. Brown ameeleza kuwa hali ya sasa ni ngumu sana na inaenda haraka, na kwamba ukweli kwamba mashirika ya Umoja wa Mataifa yalileta usaidizi kwa kutumia wasafirishaji wa kibiashara kwa maana ya magari ya kukodi na huenda ilifanya wasionekane kwa mamlaka. 

Pia amekumbushia mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba siku ya Alhamisi, yakilenga "nini zaidi tunaweza kufanya pamoja". 

"Ninafanya nimewazavyo kuhakikisha kwamba tunafanya kazi yetu," amesisitiza.