Chemchem player: Kifaa cha kuwasaidia watoto kujifunza kusoma na kuhesabu
Chemchem player: Kifaa cha kuwasaidia watoto kujifunza kusoma na kuhesabu
Kuelekea siku ya kimataifa ya vijana duniani tarehe 12 Agost, inayobebwa na kauli mbiu ujuzi kwa vijana kuelekea dunia endelevu, kijana Mbunifu Kelvin Paul amedhihirisha mchango wa vijana duniani kwa kubuni vifaa mbalimbali vya kiteknolojia kama kicheza sauti kilichopewa jina la Chemchem Player ili kufanikisha lengo namba 4 la malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa, linalozungumzia Elimu kwa wote ifikapo Mwaka 2030.
Akihojiwa na Evarist Mapesa wa redio washirika SAUT FM ya Mkoani Mwanza kaskazini Magharibi mwa Tanzania kijana huyo ameeeleza kuwa kinachomsukumu ni takwimu zinazo onesha idadi kubwa hasa ya watoto hawajui kusoma , kuhesabu na kuandika hivyo ameweka nia ya kusaidia idadi kubwa ya watoto kutatua changamoto hiyo.
“Lengo langu ni kuondoa umaskini wa Kujifunza (learning Poverty) kwa kutumia jukwaa hili la Chem Player” alisema Kelvin.
Chemchem ni nini?
Ni kifaa kidogo ambacho kimeunganishwa na vifaa vya kiteknolojia na kumwezesha mtoto kusoma na kuhesabu kwa muda autakao kulingana na umri wake au darasa alilopo. Ili mtoto aweze kutumia kifaa hicho kinachohitajika ni kupata kadi maalum ambayo itamuwezesha kucheza maudhui mbalimbali.
“kitu cha msingi ni kumuondoa mtoto katika uraibu wa kutumia muda mwingi kuangalia Runinga, kitu ambacho dunia nzima inapambana kuondoa watoto kutumia muda mwingi kuangalia Runinga”.
Kwa kawaida siku za jumamosi na jumapili vyombo vya Habari nchini Tanzania vimekuwa vikirusha maudhui mbalimbali yenye lengo la kumpanua akili mtoto kwa kumfundisha masomo ya shuleni kama hesabu, sayansi na Kingereza.
Lakini ni masomo hayo hufundishwa kwa watoto wote bila kujali umri wa mtoto na wakati mwingine darasa alilopo kwa wakati huo, hivyo mtoto hujikuta akiwa darasa la awali anafuatilia masomo ambayo atajifunza akiwa darasa la pili.
Kupitia kifaa hiki mtoto ataweza kucheza maudhui kulingana na umri wake pamoja na darasa alilopo kwa wakati huo, huku mzazi Pamoja na mmiliki wa kifaa hicho watakuwa na uwezo wa kujua aina ya masomo anayoyapenda mtoto, na maswali gani ameyafanya na amepata ngapi.
“Nyumbani watoto wetu huwa wanawasha runinga kuangalia vipindi vya watoto, lakini unakuta siku hiyo wanafundisha kugawanya, au kuzidisha ama kutengeneza kitu fulani cha kisayansi ambapo yeye hajafikia hatua hiyo inakuwa ni kazi sana kuweza kuchanganua maudhui hayo”.
Ameeleza kifaa hicho ni suluhisho “Hiki kifaa kitakuwa kinanitumia mimi taarifa kuwa mtoto fulani aliyepo mtaa fulani kwa hivi sasa anafanya maswali ya hesabu na amepata ngapi, hivyo mimi nitamrudha kutoka hatua aliyopo kwenda nyingine”.
Taarifa hii imeandikwa na Evarist Mapesa wa redio washirika SAUT FM ya mkoani Mwanza nchini Tanzania.