Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi ya nyuklia katika kuhakikisha jamii inakula chakula kilicho salama 

Wafanyakazi wakiweka lebo kwa chakula kinachoandaliwa kwenye maabara na kusindiliwa kwa mikembe kwa ajili ya kuuza.
FAO/Giulio Napolitano
Wafanyakazi wakiweka lebo kwa chakula kinachoandaliwa kwenye maabara na kusindiliwa kwa mikembe kwa ajili ya kuuza.

Matumizi ya nyuklia katika kuhakikisha jamii inakula chakula kilicho salama 

Ukuaji wa Kiuchumi

Usalama wa chakula ni suala muhimu kwa afya ya umma na usalama wa chakula duniani, hata hivyo walaji hawawezi kugundua kwa kuona, kuonja au kunusa chakula kilichochafuliwa na ndio maaana maabara za usalama wa chakula zinazotumia sayansi ya nyuklia kuhakikisha wananchi wanalindwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO linakadiria watu milioni 600 kila mwaka wanapata madhara kutokana na kula chakula kisicho salama, idadi hii ni sawa na mtu mmoja kati ya kila watu 10 au mara mbili ya idadi yote ya wananchi wa Marekani.

Usalama wa chakula ina maanisha chakula kinacholiwa linatakiwa kisilete madhara kwa mlaji na pale chakula kinapobainika kuwa si salama basi wataalamu hukataza wananchi kula chakula hicho.

Maendeleo ya sayansi yamewezesha nyuklia kutumika katika ukuaji wa chakula na mbogamboga na pia nyuklia hutumika kupima kiasi cha virutubisho vinavyofyonzwa. Swali ni je nyuklia inawezaje kuhakikisha chakula tunachokula ni salama?

Na anayejibu ni Carl Blackburn, mtaalamu kutoka kituo cha pamoja cha Mbinu za Nyuklia katika Chakula na Kilimo kinachosimamiwa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Chakula na Kilimo FAO na la nguzu za Atomiki IAEA.

“Kisayansi tuna viwango vya kimataifa vya chakula ambapo tunatoa kikomo kwa vyakula vinavyochafua.Zimewekwa kanuni nzuri za kuanzia uchakataji wa chakula, usindikaji, mpaka uhifadhi wa chakula. Mamlaka ya udhibiti wa chakula kwa kila nchi zinaweka viwango na sheria zinazosaidia usambazaji wa chakula kukidhi viwango vya kimataifa na ni muhimu kwa nchi zote kukidhi viwango hivyo kwa usawa kwani hatutaki viwe kizuizi kwa watu kufanya biashara ya chakula duniani kote.”

Zaidi ya nchi 200 zinahusika katika utungaji wa sheria hizo zinazosimamia kuhakikisha chakula kinakuwa salama na IAEA ndio muangalizi wa sheria hizo. 

Moja ya maabara zinazopima usalama wa chakula kwakutumia nyuklia zipo nchini Botswana, nchi inayofahamika zaidi kwa usambazaji wa nyama duniani kote, Sandy Mookantsa, ni afisa katika maabara ya Kitaifa ya Mifugo ya Botswana na anasema mbali na kupima nyama lakini pia wanasaidia kutoa mafunzo kwa nchi jirani.

“Maabara yetu ni ya usalama wa chakula, ilianzishwa mwaka 1989, tunashirikiana na IAEA katika kutujengea uwezo, rasilimali na kiufundi. Kwakupitia IAEA tumeweza kutengeneza mtandao ambapo tumekuwa tukitoa mafunzo kwa wanasayansi kutoka nchini Nigeria, Lesoth, Burundi na Uganda kwakutaja nchi chache tu."