Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaisaidia Botswana kuanzisha kituo cha ufuatiliaji polio  

Kituo cha afya nchini Botswana
UNFPA/Thalefang Charles
Kituo cha afya nchini Botswana

WHO yaisaidia Botswana kuanzisha kituo cha ufuatiliaji polio  

Afya

Kutokana na msaada kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, Botswana sasa ina kituo chake cha kwanza kabisa cha uchunguzi wa mazingira kwa ajili ya kuufuatilia ugonjwa wa polio.

 

Kwa msaada kutoka WHO, wafanyakazi katika kituo hiki cha uchunguzi wa mazingira ili kufuatilia mwenendo wa polio wamefunzwa kuhusu ukusanyaji na ushughulikiaji wa sampuli za maji taka. Timu za wachunguzi zinaendelea kukusanya sampuli mara kwa mara ili kufuatilia virusi na ilikuwa kupitia mpango huu Botswana iliweza kugundua aina yake ya kwanza ya virusi vya polio type 2 mnamo Oktoba mwaka jana 2022. 

Thongbotho Mphoyakgosi, Mwanasayansi wa Maabara Tiba katika Maabara ya Taifa mjini Gaborone, Botswana alikuwa mmoja wa walioshirikia katika utafiti huu anaeleza  kuhusu matokeo ya utafiti wao yalipowekwa wazi akisema, "Nadhani ilikuwa karibu kama saa kumi alfajiri hivi. Nilimpigia simu mwenzangu na kumwambia, “Umeona matokeo? Tulipata uthibitisho kwamba kweli tulikuwa na virusi vya polio katika nchi yetu.” 

Mathata Kgalalelo, Afisa Udhibiti Ubora, wa Shirika la Huduma ya Maji, Botswana anaeleza wanachokifanya akisema kwamba wanakusanya sampuli asubuhi ili hali mazingira iwasaidie. Baada ya kukusanya sampuli, wanahitaji kuzisafirisha hadi kwenye maabara haraka iwezekanavyo. “Lengo kuu ni kuhifadhi sampuli hiyo katika hali yake”. 

Katika maabara ndiko sampuli zinamkuta Thongbotho Mphoyakgosi, mtaalamu wa maabara wa miaka mingi, "Sampuli zinapokuja hapa, tunaangalia ikiwa mnyororo mzima wa baridi umehakikishwa wakati wote wa usafirishaji wa sampuli ili kudumisha hali halisi ya virusi tunavyovipima. Na tunapakia upya sampuli kwa ajili ya usafirishaji hadi Maabara ya NICD (Taasisi ya Kitaifa ya Magonjwa ya Kuambukiza) iliyoko Johannesburg. Ikiwa hatungeanzisha na kuanza ufuatiliaji wa mazingira nchini Botswana, hatungejua kwamba tuna virusi vya polio type 2 vinavyozunguka nchini. Kwa hiyo, hii inasaidia kwa sababu nchi sasa inajiandaa kuhusu nini kitatokea baadaye? Je, tunawalindaje Watoto wetu?”