Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Botswana licha ya kuendelea kiuchumi bado makabila madogo yako nyuma- Mtaalamu

Watoto darasani.(Picha:UNFPA Botswana / Nchidzi Smarts)

Botswana licha ya kuendelea kiuchumi bado makabila madogo yako nyuma- Mtaalamu

Utamaduni na Elimu

Botswana ni lazima iongeze juhudi zake za kutambua na kulinda haki za makabila madogo nchini  humo hasa katika maeneo ya huduma za umma, umiliki wa ardhi, namatumizi ya lugha za makabila hayo madogo katika ufundishaji shuleni.

Kauli hiyo imetolewa mjini Gaborone, Botswana na mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu makundi madogo Fernand de Varennes mwishoni mwa ziara yake ya siku 12 nchini humo.

Bwana de Verennes amesema ingawa Botswana imepiga hatua kiuchumi, na nyanja nyingine kama elimu, uhuru wa kuabudu,vita dhidi ya Virusi vya Ukimwi, VVU pamoja na ufisadi bado hatua zaidi zichukuliwa kuinua makundi madogo nchini humo.

Ametaja mfano wa watoto kutoka kabila dogo la jamii ya Baswara wanaoishi kusini na kusini mashariki mwa nchi ambao amesema wanakabiliwa na ugumu wa kupata elimu bora ikiwemo ya sekondari kutokana na uhaba wa shule pamoja na changamoto ya usafiri.

 

Image
Picha: World Bank/Curt Carnemark
Sehemu za mashambani za Botswana ambako makabila madogomadogo huishi. .(Picha: World Bank/Curt Carnemark)

Halikadhalika amesema nchini Botswana elimu hutolewa kwa lugha moja ya taifa ya kitswana na kwa kiingereza ambayo ni lugha rasmi bila kutumia  lugha mama za watoto wa makabila madogo ilhali kifaransa kwa mshangao kinaonekana kama lugha ya tatu.

Bwana de Vernes ametoa wito kwa serikali ya Botswana ifuatilie ahadi yake iliyomo kwenye ya dira 2063 na ianzishe matumizi ya lugha za makabila madogo katika shule za awali.

Amesema sambamba na hilo, ihakikishe kuwa kwenye mikoa ambamo kuna idadi kubwa ya makabila madogo, waajiri walimu wanaofahamu lugha hizo.