Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi hauna nafasi ndani ya UN - Guterres 

Bendera za mataifa mbalimbali wanachama wa Umoja wa Mataifa zikipepea nje ya makao makuu ya umoja huo jijini New York Marekani
UN Photo/Rick Bajornas
Bendera za mataifa mbalimbali wanachama wa Umoja wa Mataifa zikipepea nje ya makao makuu ya umoja huo jijini New York Marekani

Ubaguzi hauna nafasi ndani ya UN - Guterres 

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo amerejelea kauli yake ya kwamba ubaguzi na ubaguzi wa rangi hauna nafasi kwenye dunia ya sasa na zaidi ya yote hauna fursa kabisa ndani ya Umoja wa Mataifa. 

Guterres amesema hayo kupitia ujumbe wake wa video akitangaza azma yake ya kushughulikia ubaguzi na ubaguzi wa rangi ndani ya Umoja wa Mataifa na kwingineko. 

Utofauti wetu ndio utajiri wetu 

“Kutokomeza kadhia hii ni msingi wa sisi ni akina nani na ni muhimu kupeleka lengo letu duniani kote. Umoja wa Mataifa ulio fanisi unategemea stadi, utalaamu na uzoefu wa kila mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa”, amesema Katibu Mkuu. 

Amesema ana Menejimenti inayopatia kipaumbele hatua dhidi ya ubaguzi na kwamba “tumekubaliana Mpango Mkakati wa Hatua katika kushughulikia Ubaguzi na Kusongesha Utu kwa kila mtu”. 

Ametanabaisha kuwa Mshauri wake Maalum, Mojankunyane Gumbi, na timu nzima ya Harakati dhidi ya Ubaguzi wanasimamia utekelezaji, wakishirikiana na wafanyakazi wa Sekretarieti ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa, kuongeza uelewa na kusikiliza fikra na hofu za watendaji. 

Katibu Mkuu amesema nje ya Sekretarieti, ameyaomba mashirika yote ya Umoja wa Mataifa kwenye mfumo mzima wa UN kuchukua hatua kushughulikia ubaguzi pahala pa kazi. 

Safari ni ndefu lakini tumejizatiti 

Tuna safari ndefu, lakini tumejizatiti kusonga mbele. Tumeanzisha mtandao wachechemuzi wa kupambana na ubaguzi, na mtandao huo unahusisha viongozi waandamizi katika Sekretarieti yote ya Kimataifa ya UN, amefafanua Katibu Mkuu. 

Amekumbusha kuwa wanafanya kazi kwa karibu na vyama vya wafanyakazi na kwamba mapitio ya malalamiko ya awali kuhusu ubaguzi na ubaguzi wa rangi yamebaini mianya ambayo hivi sasa wanashughulikia kuiziba. 

Hata hivyo amesema tathmini nyingine huru inaendelea kuondoa upendeleo kwa misingi ya rangi au kibaguzi katika ngazi zote za mchakato wa ajira. 

Ni kwa mantiki hiyo amesema mwaka ujao wa 2024 watazindua Mfufmo wa kina wa mafunzo dhidi ya ubaguzi wa rangi. “Tumeendesha mashauriano kwa njia ya mtandao kuhusu hatua dhidi ya ubaguzi na ninawashukuru kwa kina wale walioshiriki.” 

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa wamejizatiti kuweka mazingira salama kwa watu kuweza kutoa ripoti kuhusu vitendo vya ubaguzi na ubaguzi wa rangi. 

Wengine wana shaka na shuku lakini tutalinda watakaojitokeza 

“Ninaelewa kuwa bado kuna shaka na shuku kuhusu suala hili, lakini nataka niwahakikishie kuwa tutapatia kipaumbele kuwalinda wale wote watakaojitokeza kuripoti.” 

Guterres amekumbusha kuwa utofauti ndio uthabiti wa Umoja wa Mataifa na kwamba kila mtu ana haki ya kuweko kwenye Umoja wa Mataifa. 

Makabila mbali mbali, rangi, mataifa tofauti ndio yanafanya tuwe na utajiri, amesema Katibu  Mkuu na hivyo ametamatisha akisema hebu na tujenge Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa iliyo thabiti, jumuishi na watu kutoka kona mbali mbali.