Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa kwanza wa chakula wa WFP umegawanywa Khartoum Sudan

Chakula kinasambazwa Omdurman, karibu na mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
© Sudanese Red Crescent Society
Chakula kinasambazwa Omdurman, karibu na mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

Msaada wa kwanza wa chakula wa WFP umegawanywa Khartoum Sudan

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) leo Jumanne limeeleza kuwa kwa mara ya kwanza tangu mapigano yazuke nchini Sudan tarehe 15 Aprili, wahudumu wa kibinadamu sasa wameweza kufikisha msaada wa chakula kwa familia zilizokata tamaa zilizokwama katika kitovu cha mzozo huo, Khartoum.  

Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan, Eddie Rowe, akizungumza kutoka Port Sudan, kwa njia ya video amewaeleza waandishi wa habari kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi  kwamba katika mafanikio makubwa, ugawaji wa kwanza wa msaada wa chakula kwa Khartoum umeanza Jumamosi, 27 Mei, ambapo wameweza kutoa msaada wa chakula kwa Wasudan 15,000 katika maeneo yaliyo chini ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na kwa mahasimu wao RSF “katika maeneo ya Omdurman, ambayo ni sehemu ya eneo la mji mkuu wa Khartoum." 

Ugawaji huo wa misaada unakuja katika siku za mwisho za makubaliano ya usitishaji mapigano ya siku saba uliokubaliwa na pande zote mbili za mzozo, ambao ulitarajiwa kumalizika Jumatatu jioni.

“Haya ni mafanikio makubwa. Hatimaye tumeweza kusaidia familia ambazo zimekwama huko Khartoum na zinazohaha kila siku huku chakula na mahitaji ya msingi yakipungua,” ameongeza Eddie Rowe.

Tunafanyakazi usiku na mchana kusaidia kila tuwezaye

Pia mkurugenzi huyo amesema "Tumekuwa tukifanya kazi usiku kucha kuwafikia watu huko Khartoum tangu mapigano yalipoanza. Upenyo ulifunguliwa mwishoni mwa wiki iliyopita ambao ulituruhusu kuanza usambazaji wa chakula. WFP lazima ifanye kazi zaidi, lakini hiyo inategemea pande zinazohusika katika mzozo huo, usalama na fursa ambao watatuhakikisha katika maeneo hayo."

WFP inapanua kwa kasi wigo wa usambazaji wa msaada wa dharura wa chakula nchini kote.

Haya ndiyo yaliyofanyika hadi sasa katika usambazaji wa chakula wa WFP Sudan:

• WFP imesambaza msaada wa chakula kwa watu 12,445 katika maeneo yanayodhibitiwa na vikosi vya wanajeshi wa Sudan (SAF) na maeneo yanayodhibitiwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na maeneo ya Omdurman, sehemu ya eneo la mji mkuu wa Khartoum. Siku tatu za usambazaji zilianza Jumamosi na ni mara ya kwanza kwa WFP kuweza kusambaza msaada wa chaskula katika mji huo tangu mapigano yalipozuka mjini Khartoum tarehe 15 Aprili.

• Usaidizi zaidi wa chakula umetayarishwa ili kuendelea na usambazaji mjini Khartoum kadiri hali ya usalama inavyoruhusu. WFP inapanga kuwafikia watu wasiopungua 500,000 mjini Khartoum.

• Mwishoni mwa juma, ugawaji wa chakula na lishe pia ulianza Wadi Halfa katika jimbo la Kaskazini kwa Wasudan 8,000 waliokimbia Khartoum na wanafunga safari ndefu kwenda Misri. Mwishoni mwa wiki iliyopita, WFP pia ilianza usambazaji wa msaada wa chakula kwa watu 4,000 wapya waliokimbia makazi yao huko Port Sudan.

• WFP imeongeza msaada kwa haraka nchini Sudan hadi kufikia watu 675,000 hadi sasa kwa msaada wa dharura wa chakula na lishe katika majimbo 13 kati ya 18 ya nchi hiyo tangu operesheni zianze tena chini ya mwezi mmoja uliopita tarehe 3 Mei. WFP inapanuka kusaidia watu milioni 5.9 kote Sudan katika kipindi cha miezi sita ijayo huku njaa ikiongezeka.

Baadhi ya watu 10,000 wanatarajiwa kupokea msaada wa chakula katika usambazaji wa kwanza huko Omdurman, Sudan.
© Sudanese Red Crescent Society
Baadhi ya watu 10,000 wanatarajiwa kupokea msaada wa chakula katika usambazaji wa kwanza huko Omdurman, Sudan.

WFP inatoa msaada wa huduma za mawasiliano

• WFP pia inatoa huduma za dharura za mawasiliano ya simu kwa mashirika yote ya Umoja wa Mataifa na jumuiya kubwa ya kibinadamu nchini Sudan ambapo mawasiliano ya msingi ni changamoto.

• WFP inahitaji dola za Marekani milioni 731 ili kufikia watu milioni 5.9 walioathiriwa na migogoro nchini kote katika kipindi cha miezi sita ijayo.

• WFP inatoa wito wa haraka kwa pande zote kuwezesha ufikishaji salama wa msaada wa chakula unaohitajika haraka, hasa katika jimbo la Khartoum ambako mapigano yamekuwa yakiendelea kwa wiki sita.

• Takriban watu milioni 2 - 2.5 nchini Sudan wanatarajiwa kukumbwa na njaa katika miezi ijayo kwa sababu ya ghasia zinazoendelea.

Hii itafanya uhaba mkubwa wa chakula nchini Sudan kufikia rekodi ya viwango vya juu zaidi huku watu zaidi ya milioni 19 wakiathirika, saw ana asilimia 40 ya watu wote.

Kituo cha muda cha UNHCR, karibu na mpaka wa Joda huko Renk, Sudan Kusini, kinawapatia wahamiaji wapya mambo ya msingi kama vile chakula, maji na blanketi.
© UNHCR/Charlotte Hallqvist
Kituo cha muda cha UNHCR, karibu na mpaka wa Joda huko Renk, Sudan Kusini, kinawapatia wahamiaji wapya mambo ya msingi kama vile chakula, maji na blanketi.

Grandi achagiza msaada kwa Wasudan

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Filippo Grandi akihitimisha ziara ya siku tatu nchini Misri ametoa wito wa dharura wa msaada kwa watu wanaokimbia Sudan na akazisihi nchi zinazowapokea wakimbizi wa Sudan kuendelea kuacha mipaka yao wazi kwa ajili ya wale wanaotoroka vita. 

Zaidi ya watu 170,000 wameingia Misri tangu mzozo huo wa Sudan uanze tarehe 15 Aprili, wengi kupitia Qoustul, kivuko cha mpaka ambacho Grandi alitembelea karibu na mwisho wa safari yake. Misri inawahifadhi karibu nusu ya zaidi ya watu 345,000 ambao wameikimbia Sudan hivi karibuni. 

Baada ya kusajiliwa na UNHCR, wakimbizi na wanaotafuta hifadhi wanapata huduma mbalimbali zikiwemo za afya na elimu na pia program ya UNHCR ya msaada wa dharura wa pesa taslimu ilianza wiki iliyopita. 

Katika eneo la mpakani apokutana na wakimbizi wapya wanaowasili Misri na kuzungumza nao Grandi amesema "Nimesikia matukio ya kutisha ya watu kupoteza maisha na mali kwa kiwango kikubwa. Watu wamezungumzia juu ya safari hatari na za gharama kubwa kufika hapa kwa ajili ya kusaka usalama. Familia nyingi zimesambaratika. Wameumizwa na wanahitaji ulinzi na usaidizi wetu haraka."