Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan lindeni uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani-UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Sudan lindeni uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani-UN

Amani na Usalama

Kutokana na hali ya vurugu na mauaji nchini Sudan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake mjini New York Marekani amesihi kuweka mazingira ya uwepo wa utulivu na anatoa wito kwa mamlaka nchini humo kufanya uchunguzi wa kina kuhusu vifo na vurugu.

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametuma salamu za rambirambi kwa wale wote waliowapoteza wapendwa wao katika vurugu.

Vyombo mbalimbali vya kimataifa vinasema kuwa hadi sasa takribani watu 19 wameshapoteza maisha kutokana na vurugu.

Antonio Guterres amesisitiza umuhimu wa kulinda uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani.

Kwa takribani siku 10 sasa yaani kuanzia tarehe 19 December waandamanaji wamekuwa katika maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya bidhaa, uhaba wa mafuta na chakula, hali ambayo imeleta sintofahamu na mzozo uliosababisha mvutano katika ya waandamanaji na vikosi vya serikali.

Hivi karibuni wataalam wa Umoja wa Mataifa wamesihi mamlaka za Sudan ziwaachie huru wale wanaoshikiliwa na ufanyike uchunguzi huru na kuhakikisha vikosi vya usalama vinadhibiti maandamano kwa kuzingatia makubaliano ya kimataifa kuhusu haki za binadamu.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.