Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa nini ilichukua muda mrefu kumkamata mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari Fulgence Kayishema?

Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda (2019).
UN Photo/Violaine Martin
Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda (2019).

Kwa nini ilichukua muda mrefu kumkamata mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari Fulgence Kayishema?

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ofisi ya mwendesha mashtaka ya mfumo wa kimataifa wa kushughulikia mabaki ya kesi za mauaji ya kimbari, IRMCT iliyoko Arusha Tanzania,  Serge Brammertz ameeleza kuwa Fulgence Kayishema, mmoja wa watuhumiwa vinara waliokuwa wanasakwa zaidi kwa kuhusika na mauaji ya kimbari nchini Rwanda, aliyekamatwa juzi Mei 24 huko Paarl nchini Afrika Kusini huenda akapelekwa nchini Rwanda kukabiliana na mkono wa sheria kutokana na tuhuma za kushiriki kuwaua watu zaidi ya 2000 wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994. 

Serge Brammertz anaeleza namna mtuhumiwa huyu Fulgence Kayishema ambaye amekuwa akijificha kwa zaidi ya miaka 20 alivyokamatwa huko Afrika Kusini. 

Mwendesha Mashitaka Mkuu huyo wa ofisi ya mwendesha mashtaka ya mfumo wa kimataifa wa kushughulikia mabaki ya kesi za mauaji ya kimbari ya Rwanda na Yugoslavia, IRMCT iliyoko chini ya Umoja wa Mataifa anasema kwamba ndani ya Afrika Kusini pekee imezichukua takribani mwaka mmoja mamlaka na kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa kufuatilia mienendo ya Fulgence Kaishema ambapo walitumia takribani miezi kumi kukusanya taarifa kutoka kwa watu ambao walikuwa wanaangaliwa kwamba wanamsaidia mtuhumiwa kujificha na kutoroka mkono wa sheria. Aidha walitumia utalaamu wa kisasa wa upelelezi ikiwemo uchambuzi wa mawasiliano ya simu, uchunguzi miamala ya kifedha na mbinu nyingine.  

Nilipomuuliza kuhusu ni kwa nini imechukua muda mrefu wa zaidi ya miaka 20 hadi kufikia kumtia mbaroni Fulgence Kayishema, Bwana Serge Brammertz anafafanua akisema, “Mojawapo ya shida ni dhahiri kwa watuhumiwa wengi waliojificha katika nchi za Kiafrika ni kwamba walitumia vibaya utambulisho bandia na kujificha, na hata mara nyingi zaidi kati ya jamii ya wakimbizi. Tukimtazama Kaishema, kama unavyojua alihusika kwa kiasi kikubwa katika kufanya mauaji ya kimbari. Kisha akakimbilia DRC. Kutoka hapo akaenda Tanzania. Alienda kwenye kambi za wakimbizi huko. Alihamia Msumbiji kwenye kambi nyingine ya wakimbizi. Kisha alikaa muda huko Eswatini kabla ya mwishoni mwa miaka ya 90, kuhamia Afrika Kusini. Wakati huo huo, alikuwa ametumia hati nne tofauti za kusafiria. Ametumia pasipoti, vitambulisho tofauti. Alikuwa hata anapata hadhi ya ukimbizi wakati huo huo katika nchi tofauti. Kwa hivyo, hoja ninayotaka kusema ni rahisi sana kupata hati bandia. Ni vigumu sana kwa mamlaka kufanya udhibiti wa namna hii, hasa ikiwa una idadi muhimu ya watuhumiwa walio mafichoni, na hivyo ndivyo alivyoweza kujificha kwa miaka mingi katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini.” 

Na kuhusu atakakopelekwa mtuhumiwa huyu wa mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda, Mwendesha Mashitaka Serge Brammertz ananiambia  Afrika Kusini wameanza mchakato wa kisheria kisha ombi lililopo ni mtuhumiwa kupelekwa Arusha Tanzania lakini uwezekano mkubwa ni kwamba mashitaka na usikilizwaji wa kesi vitafanyika nchini Rwanda, “Kama unavyojua, tuko katika awamu hii ya mwisho ya ofisi ya mwendesha mashtaka ya mfumo wa kimataifa wa kushughulikia mabaki ya kesi za mauaji ya kimbari. Pia Baraza la Usalama limetuhimiza kuhakikisha kwamba kesi zote zilizosalia zinasikilizwa na ofisi za mashtaka na yeye anapaswa kufanyiwa hivyo katika taasisi za Rwanda.” 

Mnamo mwaka 2001 Fulgence Kayishema alishtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa nchini Rwanda (ICTR) iliyokuwa Arusha Tanzania kwa makosa ya mauaji ya kimbari, kufanikisha mauaji ya kimbari, kuchochea mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu kwa mauaji na makosa mengine yaliyofanyika kwenye kitongoji cha Kivumu jimbo la Kibuye.  

Inadaiwa kuwa tarehe 15 mwezi Aprili mwaka 1994, Kayishema pamoja na watuhumiwa wengine waliua zaidi ya watu 2,000 kwenye kanisa huko Nyange na inadaiwa kuwa alishiriki moja kwa moja katika kupanga na utekelezaji wa mauaji hayo ikiwemo kununua na kusambaza petroli na kuchoma moto kanisa ilhali wakimbizi hao wakiwa ndani na hata waliobaki hai baada ya moto, walikufa baada ya wauaji hao kutumia tingatinga kuangusha kanisa lote. Watuhumiwa wengine watatu bado wanasakwa ili wakutane na mkono wa sheria.