Matumizi ya bangi kwa tiba bado yana changamoto- INCB

5 Machi 2019

Bodi ya kimataifa ya kuzuia madawa ya kulevya INCB imeonya kuwa progamu dhaifu ya matumizi ya bangi kwa ajili ya kupunguza maumivu huenda ikasababisha ongezeko la matumizi zaidi ya bangi kwa uraibu.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2018 ya INCB ambayo imezinduliwa leo Jumanne ikitathmini hatari na faida za matumizi ya bangi kwa ajili ya tiba na sayansi na athari zake kwa matumizi ya uraibu, ambao unatokana na makubaliano ya matumizi ya dawa ambazo huenda zikahatarisha afya ya umma.

Akizungumzia ripoti hiyo, rais wa INCB, Viroj Sumyai amesema ripoti yao imejikita katika matumizi ya bangi na bidhaa zikonazo na bangi wakati huu ambapo baadhi ya nchi zimepitisha sheria kuhusu matumizi ya bangi kwa misingi ya tiba na vinginevyo.

Bwana Sumyai amesema kuna utata mkubwa kuhusu usalama, usimamizi na usambazaji wa bangi hususan katika maeneo ambako matumizi ya bangi yamekubaliwa kisheria au programu za bangi inayotumika kwa matibabu zinapanuka akiongeza kuwa hakuna taarifa toshelezi kuhusu namna ambavyo mfumo wa kudhibitia madawa unavyofanya kazi akisema, “imekarabatiwa kwa ajili ya kulinda afya ya umma na kuzuia matumizi ya madawa ya kulevya wakati ikihakikisha upatikanaji wa dawa muhimu.

Kwa mantiki hiyo INCB kupitia ripoti yake imetoa wito kwa serikali kufanya hima kuhakikisha dawa za kupooza maumivu  na nyinginezo zinapatikana kwa wote huku ikiongeza kuwa watu wengi wanapitia maumivu mengi na kupitia upasuaji bila dawa za kupooza maumivu hayo.

Imetaja sababu kuwa ni ukosefu wa dawa katika baadhi ya maeneo na wakati mwingine upatikanaji usiodhibitiwa unasababisha ufikiaji wa dawa hizo na uraibu.

INCB imetoa pendekezo kwa nchi za kipato cha chini ambako idadi ya madaktari ni ndogo, kutumia watoa huduma wengine wa afya kwa mfano wauguzi kuruhusiwa kuwaandikia wagonjwa dawa zinazodhibitiwa.

Ripoti ya INCB imeonyesha hatua mujarabu katika kutokomeza matumizi ya kemikali zinazotumika kutengeneza madawa ya kulevya lakini kwamba njia mpya zinahitajika kutafuta njia mpya ya kukabiliana na kuenea kwa kemikali hizo.

Halikadhalika INCB imelaani ukatili dhidi ya watu wanaoshukiwa kutekeleza uhalifu unaohusiana na madawa ya kulevya na kuhimiza serikali kukabiliana na uhalifu unaohusiana na madawa ya kulevya kupitia njia zinazozingatia sheria na ambazo zinaheshimu haki za binadamu.

Ikimulika mambo muhimu katika maeneo mbalimbali, ripoti imeangazia changamoto zinazokabili dunia sehemu tofauti ambapo kumekuwa na mabadiliko ya sera na utekelezaji wake juu ya bangi.

Mathalani,  Amerika Kaskazini ambako Canada matumizi, mauzo na usambazaji wa bangi yalipitishwa Oktoba 2018 nako Mexico mwezi huo huo kubanwa kwa matumizi ya bangi kwa sababu za kitabibu kulitajwa kama kutoendana na katiba wakati huo huo matumizi kupitiliza ya madawa ya kulevya yameongezeka nchini Marekani huku takriban vifo 70,000 kutokana na matumizi ya mihadarati kupitiliza vikiripotiwa.

Aidha uzalishaji wa mihadarati aina ya cocaine Amerika Kusini kuliathiri bara Ulaya na Amerika Kaskazini. Pia migogoro Mashariki ya kati kumechangia usafirishaji wa mihadarati katika ukanda huo.

Halikadhalika INCB ina wasiwasi kuhusu mataifa ya Oceania ambayo hayajaridhia mkataba wa kudhibiti madawa ya kulevya.

Ripoti ya mwaka 2018 ya INCB imekuja wakati huu ambapo bodi hiyo inaadhimisha miaka 50 tangu kuasisiwa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud