Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa Binti Shupavu wafungua fikra za wazazi kuhusu haki za mtoto

Picha ya pamoja ya wazazi wa Kata ya Ngerengere mkoani Morogoro nchini Tanzania na wafanyakazi wa GLAMI.
UN News
Picha ya pamoja ya wazazi wa Kata ya Ngerengere mkoani Morogoro nchini Tanzania na wafanyakazi wa GLAMI.

Mradi wa Binti Shupavu wafungua fikra za wazazi kuhusu haki za mtoto

Utamaduni na Elimu

Mradi wa ‘’Binti Shupavu’’ unaotekelezwa shirika lisilo la kiserikali la Girls Livelihood and Mentorship Initiative (GLAMI), huko mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanznia kwa kuwapatia wanafunzi wa Kike Elimu ya Stadi za Maisha ikiwemo kujitambua, umekupokelewa vyema na wazazi na walezi baada ya kuonesha nia ya kumsadidia mtoto wa kike kukabiliana na changamoto anazoweza kukumbana nazo wakati akiwa Shule.

Soundcloud

Shirika la GLAMI linatekeleza Mradi wa Binti Shupavu ikiwa ni njia ya kufanikisha lengo namba 4 la malengo ya maendeleo endelevu SDG’s linahohusu Elimu, ambapo jumla ya wasichana 824 wameanza kunufaika na mradi huo kutoka shule 9 za sekondari zilizoko halmashauri ya wilaya ya Morogoro Vijijini, ambapo mwezi huu wa Mei limekamilisha programu ya kufanya vikao na wazazi katika shule hizo ili kuwajengea uwezo wa malezi kwa watoto wao.

Wanufaika ni mabinti walio kidato cha 1 hadi cha 4

Msimamizi wa mradi wa Binti Shupavu mkoani Morogoro Einoth Justine alieleza hatua ya mradi iliyofikiwa kwa sasa pamoja na kufafanua matarajio yao kwa wazazi wa wanafunzi wanufaika akisema, “mradi wa Binti Shupavu ni unajihusisha na mabinti ambao wako kidato cha kwanza hadi kidato cha nne na ni mahususi kwa ajili ya kuhakikisha hawa mabinti wanapata mafunzo ya stadi za maisha pamoja na elimu ya uongozi binafsi, ili kuwasaidia kujitambua, kuweza kubaki shule na kuhitimu elimu yao ya Kidato cha Nne na kuendelea mbele zaidi, lakini pia wanafundishwa namna ya kuwa wastahamilivu kuweza kuzikabili changamoto wanazokutana nazo, ambazo kwa namna moja au nyingine zingeweza kuwa kikwazo katika safari yao ya elimu.”

Bi. Justine pia aliongeza kwa kueleza matarajio yao kwa wazazi “tangu mwezi Machi mwaka huu tumekuwa na mfululizo wa vikao na wazazi, lengo kuu likiwa ni kuwakumbusha majukumu yao, kusikia kutoka kwako wao wamekua wakifanya nini kumsaidia huyu binti kuweza kufikia malengo yake lakini pia tutashirikiana nao kwa jinsi gani kama shirika kuhakikisha tunamsaidia Binti kufikia malengo yake. Matarajio yetu ni kwamba hawa wazazi watakua chachu ya mabadiliko kwenye Jamii zao wakitimiza majukumu yao, kwa watoto wao hasa wa kike lakini pia kufuatilia safari yao ya elimu na kuona kwa namna gani kwa pamoja tunaweza kuwasaidia hawa mabinti”

Akitoa mchango wake katika kikao cha wazazi na GLAMI, katika kata ya Ngerengere mzazi Msafiri Lema, alionesha kuvutiwa na aina ya mafunzo waliyopewa na wawezeshaji wa kikao hicho, “kwa kweli mmekuja kutufungua kichwa, kutufungua masikio, tena naenda kuwaambia wale waliokua na udhuru wa kutofika kwenye kikao hiki, jamani tunatakiwa tufanya moja tufanye mbili katika malezi ya mabinti wetu ili tuwe na mabinti shupavu lakini tuwe na taifa jipya”

Afisa Elimu Kata ya Ngerengere katika Tarafa ya Ngerengere Lydia Ntapara alieleza matumaini yake kupitia Mradi wa Binti Shupavu.“Mimi Afisa Elimu kata kupitia huu Mradi wa Binti Shupavu nitahakikisha nafuatilia kwa ukaribu zaidi, kwani kwangu katika kipengele cha Elimu inanisaidia sana baada ya kujua malengo ya Binti shupavu na jisni tutakavyoshirikia kwa pamoja kumjenga Binti, na pia nitafuatilia zaidi ili nijenge mabinti wengi kama nilivyo mimi na wengine kama kina Mama Samia” alisema Lydia Ntapara.

Zebedayo Mbamba Afisa ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini mkoani Morogoro mashariki mwa Tanzania akiendesha mafunzo kwa wazazi kuhusu haki za mtoto.
UN News
Zebedayo Mbamba Afisa ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini mkoani Morogoro mashariki mwa Tanzania akiendesha mafunzo kwa wazazi kuhusu haki za mtoto.

Wazazi wafurahi mafunzo juu ya ushirikishaji watoto

Zebedayo Mbamba ni Afisa ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini amekuwa akishiriki kutoa Elimu ya Haki za Mtoto na Ukatili wa kijinsia katika vikao vya wazazi wa wanafunzi wanufaika wa Mradi wa Binti Shupavu, akihojiwa na mshirika wetu alisema, “tumekutana na wazazi wengi ambao wanafunzi wao wanasoma shule tofauti tofauti katika Halmashauri yetu ya Morogoro vijijini, hakika kwa Elimu tuliyokuwa tunatoa kwa wazazi tumeona ina faida na matunda mengi sana kwasababu mwitikio wa wazazi ulikuwa mkubwa sana na ni Elimu ambao wazazi wengi wameonesha kuifurahia kwa sababu walikuwa hawaijui kwa mfano katika eneo langu nilikuwa nawafundisha juu ya haki za mtoto ili watambue nini wanapaswa kuzitimiza.”

Ameongeza kuwa wazazi wengi walikuwa wakishangazwa na hivi vitu mfano hasa katika haki ya kumshirikisha mtoto, kwamba wanapaswa kuwa marafiki wa mtoto wengi walikuwa wakishangazwa. Wazazi wengi walifurahia na hicho kitu na walionesha kwamba kumbe walikuwa wameweka daraja baina yao na wanafunzi.

Mwalimu Mlezi katika shule ya sekondari Matombo Mwanamvua Bakari alisema, mafunzo wanayopewa wasichana shuleni ni sehemu ya kuwasaidia wazazi katika wajibu wao wa malezi ambapo wanafunzi pia wameyapokea vyema.

Mwanamvua Bakari alisema “hawa mabinti wenyewe wako tayari kupokea mafunzo na wamependa sana kwa sababu sehemu kubwa ya haya mafunzo ni sehemu ambayo walezi na wazazi wao hawawezi kufanya na hawajawahi kuyapata kwa kweli, kwa hivyo hawa wawezeshaji wa Mradi wa Binti Shupavu wao wamekuja kuchukua nafasi ya mzazi na mlezi kwenye kuwapa yale mafunzo ambayo mabinti walikuwa hawayapati majumbani mwao”

Orodha ya Shule za Sekondari zilizofikiwa na Mradi wa Binti Shupavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vijijini ni pamoja na Ngerengere, Bwakila Chini, Kisemu, Kiroka, Mkuyuni, Fatemi, Gwata na Matombo.