Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunawaondoa watoto kwenye ajira na kuwarejesha shuleni-CAMFED 

Wanafunzi wa wakiwa darasani katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es Salaam tanzania
World Bank / Sarah Farhat
Wanafunzi wa wakiwa darasani katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es Salaam tanzania

Tunawaondoa watoto kwenye ajira na kuwarejesha shuleni-CAMFED 

Utamaduni na Elimu

Shirika lisilo la kiserikali la CAMFED nchini Tanzania linaendeleza harakati za kutetea haki za watoto, hususani wa kike, kuwaondoa kwenye ajira za utotoni na kusaidia kuwarejesha shuleni. John Kabambala wa redio washirika KidsTime FM ya Morogoro amewahoji wadau wa shirika hilo.

Kwanza ni Zamoyoni Selemani Mratibu wa Miradi wa CAMFED halmashauri ya wilaya ya Kilosa na Gairo“miradi yetu imejikita sana katika kumsaidia mtoto wa kike, katika elimu yake lakini hatuishii katika elimu. Vilevile kwa mto wa kike ambaye ameshamaliza shule, tunamwendeleza katika vyuo vya ufundi, lakini pia tunawapeleka katika vyuo vya kati, ngazi ya cheti na diploma, lakini pia wale ambao hawana sifa za kwenda vyuo tunawapa miradi ambayo wanaweza wakafanya biashara zao katika kata zao, hii yote ni kuhakikisha kwamba mtoto wa kike hawezi kuwa tegemezi katika mazingira ya sasa.” 

Asha ni mnufaika wa mradi huu na sasa amekuwa muelimishaji anayewasaidia wengine kama yeye ambao kutokana na sababu mbalimbali wamejikuta wakiishi katika mazingira magumu. Asha anasema, “mimi kama msichana nimepitia huko kwa sababu baada ya kumaliza elimu yangu ya sekondari, baba alikuwa na matatizo yaliyompelekea kuugua kwa muda mrefu. Kwa hivyo ikanibidi niende kutafuta kazi, nikaajiriwa.”  

Mwalimu Elisifa Nasali ni mwalimu katika sekondari ya Kimamba na pia ndiye mlezi wa wanafunzi wanufaika wa mradi wa CAMFED anasema, wengi kama Asha wamenufaika lakini uhitaji bado ni mkubwa, “watoto ni wengi ambao wana shida. Wengi sana ambao wana shida na wana uhitaji. Ingewezekana tungeongezewa hata namba ya watoto ambao wangepata msaada.” 

Tumaini Geugeu ni Afisa Ustawi wa jamii wilaya ya Kilosa, anaeleza namna wanavoshirikiana na mashirika kama haya yasiyo ya kiserikali, pamoja na jamii, “sisi kama serikali, kitu kikubwa ambacho tunakifanya, cha kwanza ni kuzunguka kwenye maeneo au mitaakutoa elimu kwa wazazi, vijana na jamii kwa ujumla. Inasaidia, mtu wa kawaida anapomwona mtoto ambaye amebeba biashara wakati wa mda wa shule kututafuta na kutpa taarifa moja kwa moja.”