Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Program ya GLAMI toka Tanzania yajitwalia tuzo ya UNESCO ya elimu ya wasichana na wanawake 2022

Devotha Mlay, Mkurugenzi Mwenza wa GLAMI Tanzania akizungumza wakati wa kupokea tuzo ya UNESCO huko Paris, Ufaransa. Oktoba 2022.
Video ya UNESCO
Devotha Mlay, Mkurugenzi Mwenza wa GLAMI Tanzania akizungumza wakati wa kupokea tuzo ya UNESCO huko Paris, Ufaransa. Oktoba 2022.

Program ya GLAMI toka Tanzania yajitwalia tuzo ya UNESCO ya elimu ya wasichana na wanawake 2022

Utamaduni na Elimu

“Tunachokifanya GLAMI ni kazi ya kuwajenga wasichana ili wajiamini, wawe na mnepo na ambao wanaelewa jinsi ya kukabiliana na changamoto katika maisha yao huku wakiweka kipaumbele katika elimu yao," anasema Devotha Mlay, Mkurugenzi Mwenza wa programu za GLAMI, ambao ni mpango wa maisha ya masichana na ushauri.

GLAMI ni mmoja wa washindi wawili wa tuzo ya mwaka 2022 ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO ya “Elimu ya Wasichana na Wanawake.”  Makala hii iliyochapishwa katika wavuti wa UNESCO yenye makao yake makuu huko Paris, Ufaransa inafafanua kwa kina.

Program GLAMI, iliyoanzishwa mwaka 2001, inatunukiwa tuzo kwa programu zake mbili kubwa na mashuhuri, Binti Shupavu na Kisa ambazo zinasaidia wasichana 7,400 katika mkoa wa Kilimanjaro na Arusha nchiniTanzania kuvuka kwa usalama katika viwango mbalimbali vya elimu, kumaliza masomo yao, na kujiendfeleza kuwa viongozi wanaojiamini. 

Kuleta mabadiliko katika jamii 

Wanafunzi katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es salaam nchini Tanzania.
Sarah Farhat/World Bank
Wanafunzi katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es salaam nchini Tanzania.

Kulingana na taasisi ya UNESCO ya takwimu za elimu na sayansi UIS, ni asilimia 39 tu ya wasichana wa Kitanzania ndio wanaokwenda shule za sekondari na chini ya asilimia 3 wanakwenda elimu ya juu. 

"Wasichana nchini Tanzania wanakabiliwa na vikwazo vingi vya kumaliza elimu yao, kuanzia mahitaji ya nyumbani na shuleni hadi shinikizo la kijamii na kiuchumi," amesema Devotha. 

Monica Swai, ambaye ni Mkurugenzi Mwenza wa operesheni wa GLAMI anasema licha ya changamoto hizo elimu ni muhimu kwa wasichana akiongeza kuwa “Utafiti unaonyesha kuwa wasichana wanaomaliza elimu wanaweza kupata ajira bora, kulea familia zenye afya bora, na wana uwezekano mkubwa wa kutanguliza elimu kwa watoto wao. Msichana mmoja aliyeelimishwa huleta athari nzuri ya mabadiliko ambayo hujirudia kwa vizazi vingi.” 

Kujifunza kuchangamkia fursa 

Programu ya Binti Shupavu ya GLAMI au ‘Binti Jasiri’ iliyozinduliwa mwaka 2017 katika mkoa wa Kilimanjaro, ni kozi ya stadi za maisha kwa wasichana wenye umri wa miaka 12 hadi 18 ambayo inaendeshwa katika miaka minne ya kwanza ya shule ya sekondari.  

Kozi hiyo inashughulikia mada kama vile ujuzi wa kusoma, uongozi wa kibinafsi, afya, na kujiamini kwa lengo la kuongeza viwango vya kuhitimu katika elimu.  

Kwa sasa kuna wahitimu 2,934 ambao wameshiriki katika mpango huo, na wasomi 5,146 wa Binti walisajiliwa katika shule 22 washirika mwaka 2022. 

Washauri, asilimia 80 ambao wamepitia program hii hufanya kazi moja kwa moja na wasichana kupitia mikutano ya kila wiki ya klabu ambapo wanajadili mada kama vile afya ya uzazi, na mikakati ya kukabiliana na changamoto. 

Devotha anasema "tunafanya kazi na shule washirika kuwalenga wasichana ambao wanafikiri wako hatarini zaidi na wako katika hatari ya kuacha shule. Mfuko wa dharura wa GLAMI ni kwa ajili ya wanachuo wa Binti Shupavu ambao wanakabiliwa na vikwazo bvikubwa ambavyo vinavyowaweka katika hatari ya kuacha shule, kulipia gharama zinazohusiana na karo, vifaa, sare za shule , afya, chakula, na  vingine vingi,"  

Ameongeza kuwa "GLAMI inasisitiza kuhusisha na kujenga uhusiano na wazazi tangu binti yao anapojiunga na Binti Shupavu. Wazazi wanapoelewa kile wasichana wanachojifunza, wanasaidia binti zao kufaulu shuleni na zaidi, mitazamo yao inabadilika, na wanakuwa washiriki watendaji zaidi.” 

Kujenga kujiamini na hisia za jumuiya 

“Kisa” ni kozi ya uongozi ambayo hutayarisha wasichana wenye umri wa miaka 16 hadi 20 kuhudhuria chuo kikuu na kuleta mabadiliko chanya ya kijamii katika jamii zao.  

Kwa sasa wasichana 2,338 wameandikishwa, na wasichana 4,136 wamemaliza kozi hiyo.  

Kozi inajumuisha madarasa ya kila wiki, yakiongozwa na washauri ambao wengi wao ni wahitimu wa program hiyo, pia makongamano matatu ya afya kwa mwaka, siku ya kazi, na miradi ya kila mwaka ambapo wasichana hutambua na kutatua changamoto katika jumii zao. 

"Wasichana hujifunza ujuzi muhimu kutoka kwa mtaala wetu, lakini ushindi wa kweli kwa GLAMI ni kuona wasichana hawa wakikua na kufanya kazi pamoja kuweka ujuzi wao mpya katika vitendo. Kujiamini kwao kunaongezeka sana kwa sababu wanajifunza katika mazingira ya kuungana mkono pamoja na wenzao, kutoka kwa mshauri mwanamke aliyeelimika wa chuo kikuu ambaye anaonyesha kile wanachoweza kufanya na kuwa.” 

Wasomi wa Kisa sio tu wanahitimu kwa viwango vya juu, na alama za juu za mtihani kuliko wenzao, pia wanaripoti kuwa na viwango vya juu vya kujiamini, na kujieleza mwishoni mwa programu. 

Msaada unaendelea hata baada ya kuhitimu 

Kwa mujibu wa mkurugenzi mwenza Monica "tunatoa fursa kwa wahitimu wetu kuendelea kushikamana na GLAMI na kuendelea kujifunza na kukua pamoja na mafunzo ya utayari wa kazi, fursa za mitandao, na nafasi ya kushiriki katika semina za kukuza biashara,"  

Mwanachuo mmoja wa Binti Shupavu, Maua Shaban Fonga, amesema: “kujiamini na kuhamasika kulinifanya nisiogope kuanzisha biashara. Ninaweza kuzungumza na mtu yeyote kwa ujasiri mahali popote! Sasa nauza vitambaa, chupi, magauni na nguo za kiume. Ninaendesha hata duka la vipuri vya pikipiki! Ninajitegemea kifedha kwa 100% na pia ninaweza kusaidia familia yangu.” 

Devotha na Monica wanasema Tuzo ya UNESCO la Elimu ya Wasichana na Wanawake itasaidia mpango huo kuendelea kukua na kuwafikia wasichana wengi zaidi.  

Mwaka huu wa 2023, GLAMI itapanua wigo wa programu yake ya Binti Shupavu hadi Morogoro Mashariki mwa Tanzania, ambako kiwango cha wasichana wanaoacha shule ni kikubwa sana. 

"Mwishowe, nia yetu ni kwamba kila msichana wa Kitanzania awe na elimu, ujasiri, mnepo, na uwezo wa uongozi wa kubuni maisha yake kama anavyotaka," amemalizia Devotha.