Ukatili wa kijinsia dhidi ya wasichana na wanawake DRC umefikia viwango vya kutisha:UNICEF
Ukatili wa kijinsia dhidi ya wasichana na wanawake DRC umefikia viwango vya kutisha:UNICEF
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF leo limetoa wito wa kuongezwa kwa msaada muhimu na wa dharura wa uingiliaji kati na ufadhili ili kukabiliana na ongezeko la visa vinavyoripotiwa vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto na wanawake katika jimbo la Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
Ripoti za ukatili wa kijinsia GBV, dhidi ya wasichana na wanawake Kivu Kaskazini zimeongezeka kwa asilimia 37 katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2023 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka mmoja uliopita, kulingana na kikundi cha uratibu wa GBV katika jimbo hilo, limesema shirika la UNICEF katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Zaidi ya visa 38,000 vya ukatili wa kijinsia vimeripotiwa kwa mwaka mzima wa 2022 huko Kivu Kaskazini pekee.
Katika visa vingi, walionusurika walisema walishambuliwa na watu wenye silaha na watu waliokimbia makazi yao ndani na karibu na kambi.
Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC Grant Leaity amesema “Mara chache watoto na wanawake walio katika mazingira magumu wanaotafuta hifadhi katika kambi badala yake wanajikuta wakikabiliwa na unyanyasaji na mateso zaidi. Ongezeko la unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto ni la kuogofya, kukiwa na ripoti kwamba baadhi ya watoto wenye umri mdogo wa miaka 3 wamedhulumiwa kingono. Hali hii inapaswa kutuamsha, kutuuguza na kutuchochea sote kuchukua hatua”.
Zaidi ya 1,000,000 wamehama makazi yao tangu Machi 2022
Tangu mapema Machi 2022, zaidi ya watu milioni 1.16 wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano kati ya pande hasimu kwenye mzozo huko Kivu Kaskazini.
Takriban asilimia 60 ya watu waliokimbia makazi yao wanaishi katika maeneo yenye msongamano mkubwa na makazi ya pamoja nje kidogo ya Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu ambapo hatari ya unyanyasaji wa kijinsia ni kubwa sana. UNICEF pia inafahamu kuhusu viwango vya juu sana vya ukatili wa kingono kwa watoto katika zaidi ya maeneo 1,000 ndani na karibu na kambi za wakimbizi wa ndani.
Kulingana na shirika hilo la Umoja wa Mataifa, athari kwa afya ya kimwili na kiakili ya wasichana na wanawake haiwezi kupimika na ni ya muda mrefu. Kikundi cha uratibu wa GBV, kimesema karibu mwathirika 1 kati ya 4 wa ukatili wa kijinsia anahitaji usaidizi maalum wa matibabu na kisaikolojia.
UNICEF imeimarisha shughuli zake za kuzuia na kukabiliana na ukatili huo. Shirika hilo linatoa huduma muhimu za matibabu na kisaikolojia kwa wasichana na wanawake walioathirika katika kambi nne kubwa zaidi za wakimbizi karibu na Goma.
Kwa kufanya kazi na idara ya jimbo ya masuala ya kijamii na kwa kushirikiana na Heal Africa, UNICEF pia imeunda nyumba salama kwa wasichana na wanawake katika kambi za wakimbizi wa ndani, ambapo wanasaikolojia, wafanyakazi wa kijamii wa kitaalamu na wafanyakazi wa kijamii waliofunzwa kutambua na kutunza watoto na wanawake wenye uhitaji, huwaelekeza kwa huduma za ziada ikiwa inahitajika.
Wito kwa wahisani
Ili kuwalinda wanawake na wasichana UNICEF inatoa ombi la haraka kwa ajili ya kuongeza operesheni zake na huduma za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kingono ndani na karibu na kambi za wakimbizi, kukomesha kiwango kikubwa cha unyanyasaji wa kingono kwa wasichana na wanawake na kusambaratisha madanguro yatakayobainika ndani na karibu na kambi kuwa yanaendesha unyanyasaji wa kingono.
UNICEF pia inatoa wito kwa wahisani ili kuongeza msaada kwa watu wanaoishi kwenye kambi za waliotawanywa na wakimbizi wa ndani hususani kuwapa msaada wa fursa za maji salama na huduma za usafi na pia kuongeza huduma za msingi za afya, elimu na chakula.