Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka jalalani hadi kuuzwa Ulaya: Asante UNEP

Paul Maoncha ni mfanyakazi katika kiwanda cha Africa Collect Textiles nchini Kenya ambacho kupitia mradi wa UNEP wa kubadili taka kuwa bidhaa, wanakusanya nguo kuukuu na kuzalisha bidhaa mba mbali na hivyo kulinda mazingira.
Idhaa ya Kiswahili/Thelma Mwadzaya
Paul Maoncha ni mfanyakazi katika kiwanda cha Africa Collect Textiles nchini Kenya ambacho kupitia mradi wa UNEP wa kubadili taka kuwa bidhaa, wanakusanya nguo kuukuu na kuzalisha bidhaa mba mbali na hivyo kulinda mazingira.

Kutoka jalalani hadi kuuzwa Ulaya: Asante UNEP

Tabianchi na mazingira

Kila mwaka, nguo zenye thamani ya mabilioni ya fedha ambazo bado zinavalika hutupwa. Mitindo ya nguo hubadilika kila mara kuendana na wakati pasina kujali madhara kwa mazingira. Tathmini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, UNEP, inaashiria kuwa fani ya mitindo huchangia asimilia kati ya 2 hadi 8 ya gesi ya ukaa kwenye mazingira. 

Shughuli ya kutia rangi vitambara ina mchango mkubwa kwenye vyanzo vya uchafuzi wa mifumo ya maji kote ulimwenguni. Kulingana na wataalam,kiasi ya galoni elfu 2 za maji zinahitajika kutengeneza suruali ndefu aina ya jeans. Nguo hizo huishia jalalani na kuchangia katika uchafuzi wa mazingira. 

Ili kuondokana na uchafuzi huu utokanao na utupaji wa nguo zilizotumika, Alex Musembi muasisi na afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Africa Collect Textiles anasema kampuni yao iliibuka na mbinu ya kutumia nguo kuukuu maarufu mitumba kama malighafi kuunda bidhaa mpya. Bwana Musembi anasema, “tunaziweka hizi nguo kwenye mashubaka kwa kuzingatia kila kiwanco cha nguo.Hivyo ndio tunafanya baada ya kuzikusanya kutoka maeneo tofauti tofauti.Tuna duka kwenye eneo la maduka makubwa la Village Market Shopping Mall, tuna duka Sarit Centre, pia tuna duka Opportunity Factory,pia tunazituma hizi bidhaa ng’ambo mfano Uswisi,  ujerumani, Uholanzi. Pia tuna duka letu mtandaoni au Webshop.” 

Nguo hizo kuukuu zinakusanywa kwenye kumbi za maduka ya jumla, mjini au hata mitaani. Ili kurefusha muda wa utumiaji wa nguo, shirika la Umoja wa mataifa la mazingira, UNEP, kupitia mradi wa ubunifu katika biashara na mifumo ya kiuchumi ya kuongeza thamani kwenye bidhaa ya nguo,InTex lilizindua mradi wa miaka mitatu kuzishika mkono kampuni za mitindo. 

Kutoka jalalani hadi kuuzwa Ulaya

Moja ya kampuni hizo ni kampuni hii ya Africa Collect Textiles inayotengeneza mazulia,bidhaa za nakshi,vifaa vya watoto kuchezea na vijamvi vya mezani. 

Kupitia mradi wa InTex wa kuunda bidhaa mpya kutumia mali ghafi ya mitumba na kampeni ya kupambana na uchafuzi wa mazingira ya Beat Pollution, UNEP imefanikiwa kuzindua mifumo ya biashara ambayo inapunguza athari za uchafuzi wa mazingira na kuimarisha afya ya binadamu.

Paul Maonchafundi cherehani ACT akielezea mfumo wanaoutumia ili kuhifadhi mazingira anasema, “tuna kitu inaitwa ku upcyle...yaani kuipa thamani mpya….kutumia tena na tena...na kutengeza tena.Hivyo vitatu tunavifanya hapa.Kama ni kutumia tena na tena ,nguo ambazo ziko sawa tunazigawa kwa watoto wanaohitaji.Kwa kuzipa bidhaa thamani mpya...tunatumia mfumo wa kuunga vitambaa na kutengeza bidhaa mpya.Tunaunda pia mazulia makubwa na madogo kutokana na suruali za jinzi za bluu.” 

Mradi wa UNEP wa InTex wa kulinda mazingira kupitia mifumo bora ya biashara ya mitindo, ulizinduliwa Septemba mwaka 2020 na utaendelea hadi Januari 2024.

Je, washirika wa karibu wa mradi huo wana mtazamo upi?

Everlyne Auma ni fundi cherehani kwenye kampuni ya Africa Collect Textiles na anasema, “wakati nlipokuja kwa hii kampuniya ACT Collects hapo ndipo nlijua ya kwamba,kuna umuhimu wa kutunza zile nguo ambazo zimetumika kama jinzi kama khaki na nguo nyinginezo zinazoweza kutumia tena na tena  kama vitenge ambazo pia tunatumia kama nguo ya ndani wakati wa kushona. Hapo ndio nilijua kuna umuhimu hata mimi nikapata kufahamu kuwa nikiwa nje kule naweza kuwaelezea wenzangu jinsi ya kutumia nguo ambazo zimetumika.Wasizitupe,watuletee hapa.

Ripoti mpya ya wakfu wa Changing Markets ulioko Uholanzi,imebaini kuwa kiasi ya nguo milioni 900 kukuu zinaingia Kenya kila mwaka. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia,shughuli za biashara ya viwanda vya nguo huchangia 20% ya uchafuzi wa mifumo ya maji safi ulimwenguni.

Zippora Wanja ni mhudumu katika kiwanda cha Africa Collect Textiles cha kutengeza bidhaa kutokana na nguo kukuu na anaamini kuwa juhudi zao zinaleta mabadiliko. Huko nje, tumezoea kuona majalala yamejaa taka za kila aina zikiwemo nguo.Kwa hii njia ya kutumia tena na tena bidhaa imesaidia sana kwani zimepungua na mazingira yanakuwa masafi.Baada ya wakati mazingira yatakuwa sambamba.” 

Mradi wa InTex wa UNEP una sehemu 5: mbili zinaazimia kuubadili ulimwengu na tatu zinajikita kwenye utekelezaji kitaifa kupitia kampuni za mataifa 3 barani Afrika nayo ni Afrika Kusini,Tunisia na Kenya.

Kupitia UNEP sasa watu wameerevuka

Bwana Musembi muasisi wa kampuni ya Africa Collects Textiles ambayo ni moja ya washiriki wa mradi huo wa kulinda mazingira na anaelezea mafanikio mpaka sasa akisema, “UNEP wametupa mwanya wa kututangaza na kutunadi kwa ulimwengu ili kuihimiza dunia nzima kwamba kuna kampuni kama Africa Collect Textiles inayoweza kukusanya nguo kwa hiyo wasizitupe hovyo bali wazilete kwetu.UNEP kupitia Chuo Kikuu cha Moi nchini Kenya wanaendelea kutufanyia mikutano na kutupa mafunzo ili kutuandaa ndio ifikapo mwaka wa 2025 kampuni kama Africa Collect Textiles itakuwa imewajibika.” 

Dhamira ya mradi wa InTex wa UNEP ni kuzishika mkono kampuni za sekta ya nguo na mitindo kuunda mifumo ya biashara inayojali na kuhifadhi mazingira ukizingatia uchafuzi hata inapolenga kuuza bidhaa kwenye soko la Ulaya. 

Taarifa hii imeandaliwa na Thelma Mwadzaya, wa Idhaa ya Kiswahili ya UN Nairobi, Kenya.