Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP 'yawapiga jeki' vijana Vanga Kenya ili kulinda mazingira na kujikwamua kiuchumi

Wanachama wa kikundi cha vijana cha Mchongo eneo la Vanga kaunti ya Kwale nchini Kenya wakiwa kwenye ofisi yao. UNDP inawasaidia kwenye harakati zao za kuhifadhi mazingira.
UN/ Thelma Mwadzaya
Wanachama wa kikundi cha vijana cha Mchongo eneo la Vanga kaunti ya Kwale nchini Kenya wakiwa kwenye ofisi yao. UNDP inawasaidia kwenye harakati zao za kuhifadhi mazingira.

UNDP 'yawapiga jeki' vijana Vanga Kenya ili kulinda mazingira na kujikwamua kiuchumi

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo,UNDP, limeleta tija kwa vijana wa Vanga iliyoko kaunti ya Kwale pwani ya Kenya kupitia ufadhili wa miradi ya jamii. Ufadhili huo umewawezesha vijana kununua vifaa vya kidijitali vya kurekodia Sanaa ya michezo ya kuigiza.

Kwa mujibu wa UNDP sanaa ina nafasi muhimu kwenye maisha ya kila siku kwani inaweza kutumika kuwasilisha ujumbe unaobadili tabia. 

Sanaa na mazingira 

Kwa kutumia sanaa vijana wa eneo la Pwani la Vanga waliamua kuchukua hatua mikononi mwao ili kuwachagiza vijana wenzao kuhifadhi mazingira na hasa mikoko.  

Mikoko ina umuhimu mkubwa kwa wakaazi wa Vanga na ni sehemu ya kusaka mkate wa kila siku hivyo basi juhudi za kuihifadhi mazingira ni lazima zitiliwe mkazo. 

Tunda Mwangombe Haga ni mwenyekiti wa kikundi cha vijana cha Mchongo kilichoko Vanga na anaelezea kuwa,’Ufadhili wa UNDP, umetuwezesha kuwaelimisha wenzetu kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwani ndio tegemeo letu. Awali kulikuwa na tabia za kuchafua mazingira lakini kwa sasa kuna mabadiliko ya tabia katika jamii na uvuvi haramu pia umepungua kwani ukataji wa mikoko unafifia.” 

UNDP imesaidia vijana wa kikundi cha Mchongo kwenye harakati zao za kutumia sanaa ili kuhifadhi mazingira kama inavyoonekana kwenye picha.
UN/ Thelma Mwadzaya
UNDP imesaidia vijana wa kikundi cha Mchongo kwenye harakati zao za kutumia sanaa ili kuhifadhi mazingira kama inavyoonekana kwenye picha.

Mradi wa vijana wa UNDP 

Ofisi ya shirika la UNDP nchini Kenya, ilizindua mwaka 2020 mradi mahsusi kwa vijana lengo likiwa kuwashika mkono katika miradi ya maendeleo kupitia vikundi vyao. 

Bwamri Chengo Masha ni muigizaji katika kikundi cha Mchongo na anasimulia kuwa,”Kila ninapopita mtaani wananikumbuka kuwa mimi ndiye yule mtu mbaya kwenye michezo ya kuigiza ambaye anakata mikoko. Hii ina maana wameelewa na kuupata ujumbe kuwa hicho ni kitu ambacho hakitusaidii na hapo ndio tumeona mabadiliko ya tabia katika jamii.Hatua tunapiga polepole lakini tofauti ipo na watu wanajikanya.” 

Sanaa sio burudani tu ni ajira pia 

Ufadhili wa shirika la UNDP umewawezesha vijana hawa kununua vifaa vya kuandaa video kwa njia ya kidijitali kila wanapofanya michezo ya kuigiza katika jamii. 

Michezo hiyo hujikita kwenye mada tofauti tofauti kama uhifadhi wa mazingira, mimba na ndoa za utotoni, uhalifu na masuala yanayowazonga vijana kwa jumla. Najma Mohamed Suleiman ni mwanachama wa kikundi cha Mchongo cha vijana na kwa mtazamo wake,”Vijana sasa wameona umuhimu wa kupata elimu na kuijunga na vikundi ambavyo vinaletea mabadiliko ya moja kwa moja. Kwa sasa wameiona sanaa kama ajira na wanaikumbatia kwavile inawapa mkate wa kila siku. Kadhalika wameelewa umuhimu wa kukataa kupotezewa muda na vitendo vya uhalifu.” 

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa , asilimia 75 ya vijana wana umri ulio chini ya miaka 35 na wanapitia changamoto nyingi hususan ukosefu wa ajira.

Hilo linawatenga na mipango ya ujenzi wa taifa kwani hawana kipato. Saidi Badi Hamisi ni malenga na mghani wa mashairi katika kikundi cha vijana cha Mchongo na anasisitiza kuwa mradi wao umewavutia vijana na wengi wamebadilika,” Kila ninapotaka kutunga shairi natazama hali halisi kwenye jamii kisha Napata msukumo. Mada ni nyingi ukizingatia ni mambo ya kila siku ninayoyazungumzia. Vijana wameanza kubadilika na sasa wao ndio wasimamizi katika jamii.” 

Umoja wa mataifa kupitia malengo ya maendeleo endelevu SDG's unayapa uzito maslahi ya vijana yakizingatia masuala kama ajira, mabadiliko ya tabiayanchi,usawa ,kupambana na njaa na usawa wa kijinsia.