Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia ya nyuklia yaleta matumaini kwa wakulima nchini Kenya

Miriam Kinyua, Profesa wa uzalishaji wa mimea kutoka Chuo Kikuu cha Eldoret nchini Kenya akiwa kwenye konde la ngano na mkulima Michael Kirwa.
IAEA Video
Miriam Kinyua, Profesa wa uzalishaji wa mimea kutoka Chuo Kikuu cha Eldoret nchini Kenya akiwa kwenye konde la ngano na mkulima Michael Kirwa.

Teknolojia ya nyuklia yaleta matumaini kwa wakulima nchini Kenya

Tabianchi na mazingira

Je ni kwa vipi teknolojia ya nyuklia inaweza kuleta tofauti katika uzalishaji wa chakula wakati huu ambapo janga la tabianchi linazidi kugonga vichwa vya watu na kubisha hodi kila uchao?  

Baadhi ya watu wakisikia nyuklia kinachowajia kichwani ni mabomu ya nyuklia, lakini nchini Kenya, wanasayansi na wakulima wanaelezea kwa maneno yao wenyewe vile ambavyo sayansi ya nyuklia inasaidia kupambana na uhaba wa chakula na maji. Kuanzia uzalishaji wa mbegu mpya zinazohimili ukame hadi teknolojia za kutambua ni muda gani muafaka kumwagilia mazao. Utaalamu huu unafanyika kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya nyuklia, IAEA ambapo video moja ya shirika hilo inaanzia  

Je wajua chakula upikacho kinatoka wapi? 

Jikoni mapishi ya chapati yakiendelea! Kama ujuavyo chapati kwa kiasi kikubwa hupikwa kwa kutumia unga wa ngano. 

Kisha video inahama tunamuona Miriam Kinyua, Profesa wa uzalishaji wa mimea katika Chuo Kikuu cha Eldoret nchini Kenya akikagua konde la ngano lililomea vizuri. 

Anatembea akisema, “tunapopika chakula nyumbani, hatuachi kufikiria  chakula hiki mikononi mwetu kinatoka wapi?. 

Hapa kondeni, Profesa Kinyua yuko na mkulima hapa Eldoret ambaye anajitambulisha akisema, “naitwa Michael Kirwa na ni mkulima hapa Kenya. Tabianchi imebadilika katika miaka 10 iliyopita. Na hali inazidi kuwa mbayá. Wakati wa msimu wa upanzi hatuna mvua za kutosha. Na mvua ikinyesha, inakuja wakati usio sahihi, wakati tunakaribia kuvuna.” 

Teknolojia ya sayansi ya nyuklia inawezesha wakulima kutambua kiwango cha unyenyevu kwenye udongo, halikadhalika wakati wa kumwagilia.
IAEA Video
Teknolojia ya sayansi ya nyuklia inawezesha wakulima kutambua kiwango cha unyenyevu kwenye udongo, halikadhalika wakati wa kumwagilia.

Mvua inanyesha isipohitajika, mbegu zakumbwa na magonjwa mapya 

Profesa Kinyua anasema mabadiliko ya tabianchi yameleta changamoto kubwa katika kilimo cha ngano. Mathalani anasema,“magonjwa mapya ambayo hatukuwa tumezoea yameibuka. Na maji yatokanayo na mvua nayo ni changamoto kwa sababu ni kidogo na yanapatikana wakati usio sahihi.” 

Changamoto hii ililazimua Profesa Kinyua na wenzake kuingia maabara ambapo anasema, “tuliibeba changamoto hiyo na tukaamua kutumia teknolojia ya nyuklia kuzalisha lahaja mpya au aina mpya ya mbegu ya ngano ambayo inastahimili ukame halikadhalika inaweza kuhimili aina mpya ya magonjwa. Ijapokuwa ilituchukua miaka mitatu na nusu, tuliweza aina mpya ya mmea ambao unavumilia ugonjwa mpya wa ukuvu kwenye shina na pia unahimili ukame.” 

ELDO Mavuno ni mkombozi kwa wakulima Kenya 

Mbegu hiyo mpya ingawa kwa muonekano inafanana na mbegu za kawaida, ilipatiwa jina Eldo Mavuno. 

Kwa mujibu wa Profesa Kinyua “mahitaji ya mbegu hii ni makubwa na hatuwezi kutosheleza mahitaji ya wakulima. Nadhani katika siku zijazo, mbegu hii itakuwa imepandwa katika eneo kubwa.”   

Profesa Kinyua anaendelea mbali akisema wakulima hawahitaji mbegu bora pekee, bali pia mbegu hiyo bora lazima ipandwe kwenye udongo wenye rutuba, halikadhalika wawe na maji ya kutosha. 

Changamoto hiyo nayo tayari inashughulikiwa na shirika la utafiti wa kilimo na mifugo nchini Kenya. Jane Akoth, mwanafunzi huyu wa shahada ya uzamivu akiwa maabara anasema, “kazi yangu hapa ni kusaka mbinu bora zaidi ya kilimo ambayo inaweza kutumiwa na wakulima kwenye maeneo yenye maji kidogo. Tunatumia teknolojia ya nyuklia kutathmini aina mbalimbali za kilimo ambazo zinaweza kutumiwa na wakulima. Tunaweza kufahamu ni mbinu ipi ya upandaji mazao inapoteza maji mengi kuliko nyingine. 

Teknolojia ya nyuklia yawezesha umwagiliaji wakati muafaka 

Dkt. Kizito Kwena kutoka shirika la Kenya la utafiti wa kilimo na mifugo anasema, “teknolojia kama vihisishi vya unyevunyevu na virutubisho humwezesha mkulima kutambua wakati wa kumwagilia maji, na wakati gani asimwagilie na hivyo kuwawezesha kutumia vema maji waliyo nayo.” 

 Kwa mujibu wa IAEA, teknolojia ya mbegu bora na matumizi ya maji imesaidia wakulima kuongeza mapato kwa asilimia 30 na kupunguza matumizi ya mbolea kwa asilimia 20. 

Eunice Francis mkulima kaunti ya Machakos ni shuhuda akisema,“tangu kuanza kupata mafunzo haya nimefaidika, nimepata ujuzi mwingi wa kulima kuliko hapo awali nilipokuwa nalima.”