Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana 300 Kenya wapatiwa mafunzo kuepusha baa la nzige

Makuruta wa jeshi la huduma kwa vijana nchini Kenya wakipatiwa mafunzo na afisa wa FAO kuhusu jinsi ya kukabiliana na nzige wa jangwani nchini humo.
FAO/Kenya
Makuruta wa jeshi la huduma kwa vijana nchini Kenya wakipatiwa mafunzo na afisa wa FAO kuhusu jinsi ya kukabiliana na nzige wa jangwani nchini humo.

Vijana 300 Kenya wapatiwa mafunzo kuepusha baa la nzige

Tabianchi na mazingira

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, nchini Kenya, limeanza kuwafundisha vijana 300 wa jeshi la huduma la vijana nchini  humo, NYS mbinu za kukabiliana na nzige wa jangwani walioripotiwa kuvamia taifa hilo la Afrika Mashariki tangu mwezi Disemba mwaka jana.

Hatua  hiyo ya FAO ni sehemu ya mpango wake wa utekelezaji wa kuimarisha uwezo wa serikali ya Kenya wa kufuatilia harakati za nzige hao na hivyo kufikisha idadi ya wafuatiliaji wa nzige hao kuwa 600.

Kampeni za kutokomeza nzige hao zinahusisha timu hizo za ufuatiliaji kukusanya taarifa kuhusu makazi na idadi ya  nzige hao, taarifa ambazo zinatumika kupanga mikakati ya kuwadhibiti  nzige sambamba na hatua za kuzuia.

Mafunzo hayo yanaongozwa na mtaalamu kutoka Morocoo ambapo Kello Harsame, kutoka NYS akimwakilisha Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini  Kenya amesema serikali inaimarisha juhudi zote kuepusha baa la nzige.

Kupitia mafunzo hayo, vijana hao wataweza kushiriki katika upulizaji wa dawa kabla nzige hawajakomaa na kuweza kuruka  kwa makundi.

Nzige hao waliiingia Kenya wakitokea eneo la kaskazini na sasa yaripotiwa kuwa wako katika kaunti 17 nchini Kenya.

Kaimu Mwakilishi mkazi wa FAO nchini Kenya Tobias Takavarasha amesema uwepo wa nzige hao ni shambulizi dhahiri la harakati za shirika hilo za kutokomeza njaa, ukosefu wa chakula na  utapiamlo na kwamba, hofu yao sasa ni kwamba kizazi hiki cha kwanza cha nzige ambacho kimetokea Ethiopia na Somalia kinazaliana na pindi mayai yao yatakapototolewa utakuwa ni msimu wa upanzi na uchipuzi wa mazao.

Wataalamu wanasema kuwa kipindi cha nzige wa jangwani kuzaliana ni kati ya mwezi Januari na Machi na hivyo FAO na serikali ya Kenya wameweka mpango wa pamoja wa miezi sita huku wakifuatilia hali ilivyo.

Mwelekeo wa wadudu hao waharibifu hutegemea upepo na kwa siku moja wanaweza kwenda umbali wa kilometa 150.