Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya #ACTogether kutumika wakati wa Kombe la Kiarabu la FIFA

Uwanja wa michezo New York
UN News/ Anton Uspensky
Uwanja wa michezo New York

Kampeni ya #ACTogether kutumika wakati wa Kombe la Kiarabu la FIFA

Afya

Kwa kutumia jukwaa la Kombe la kwanza la Kiarabu la FIFA™, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO, FIFA na mamlaka ya Qatar wanazindua kampeni ya #ACTogether ili kutoa wito wa ushirikiano na umoja ili kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo, matibabu na vipimo vya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona, COVID-19.

Kupitia taarifa iliyotolewa hii leo na WHO, sehemu kubwa ya idadi ya watu ulimwenguni inabakia kuathiriwa na maambukizi na hatari ya kuongezeka kwa magonjwa na vifo.

“Ukosefu wa usawa wa chanjo unaendelea katika sehemu nyingi za dunia; kati ya takriban dozi bilioni 7.5 za chanjo za COVID-19 zilizotolewa duniani kote kufikia katikati ya Novemba 2021, ni asilimia 0.6 pekee ndiyo zilikuwa zimetolewa katika nchi za kipato cha chini.”

WHO inasisitiza haja ya kuongeza ufikiaji wa chanjo, matibabu na uchunguzi, kupitia usaidizi wa mpango wa kimataifa wa Usawa wa Ufikiaji wa Zana za COVID-19 (ACT), pamoja na umuhimu wa uzingatiaji wa kina wa hatua za afya ya umma. 

FIFA itatumia jukwaa kubwa la soka wakati wa Kombe hilo la Kiarabu la FIFA Qatar 2021™ na mfululizo wa video za matangazo, ndani ya uwanja na kote Doha. Manahodha wa timu pia wataonesha kuunga mkono ujumbe huo, huku kila chama kishirikiri kitakuwa na vitu vya kutoa kwa mashabiki wake kupitia majukwaa yake ya kijamii na kidijitali.

Mpango wa huo wa #ACTtogether wa kuhamasisha uelewa ulianzishwa kwa mara ya kwanza wakati wa toleo la mwisho la Kombe la Dunia la Vilabu la FIFA™ nchini Qatar mnamo Februari 2021 na marudio yake ya hivi punde yanasisitiza kwamba janga la COVID-19 bado halijaisha. 

Kutokana na mpango wa FIFA na UNICEF, watoto watapata chakula na kufanya mazoezi ya mwili kupitia mchezo wa mpira wa miguu.
OSCE
Kutokana na mpango wa FIFA na UNICEF, watoto watapata chakula na kufanya mazoezi ya mwili kupitia mchezo wa mpira wa miguu.

 

Rais wa FIFA Gianni Infantino amenukuliwa akisema, “hakuna aliye salama hadi kila mtu awe salama na sote tuna wajibu wetu katika kusambaza ujumbe huo. Afya huja kwanza, na kupitia kandanda, tunaweza kusisitiza ujumbe kwamba viwango vya juu vya maambukizi na vifo vitaendelea duniani kote mradi tu hakuna ufikiaji ulio sawa wa zana za kupambana na janga hili. Kazi ya pamoja ni muhimu kwa hilo na ndiyo maana tunasimama pamoja na WHO, Wizara ya Afya ya Umma ya Qatar na Kamati Kuu ya Uwasilishaji na Urithi na tunatoa wito kwa kila mtu #ACTogether na kuweka misingi ya Kombe la Dunia lenye afya la FIFA mnamo 2022.” 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, "kuibuka kwa mnyumbuliko mpya wa virusi vya Corona, Omicron kunasisitiza umuhimu wa mshikamano wa kimataifa na kufanya kazi pamoja ili kushinda janga hili. Ninakaribisha uungwaji mkono kutoka kwa Wizara ya Afya ya Umma ya Qatar, Kamati Kuu ya Uwasilishaji na Urithi, FIFA, wachezaji, watazamaji na washirika kuunga mkono ujumbe huu muhimu wakati wa Kombe la Kiarabu la FIFA. Sasa, zaidi ya hapo awali, tunahitaji kuwezesha ufikiaji sawa wa chanjo, matibabu na vipimo vya COVID-19, na kuhimiza kila mtu kufuata hatua za afya ya umma. Kufadhili kikamilifu kiongeza kasi cha ACT kitasaidia kufanya matamanio ya kumaliza hatua kali ya janga hili kuwa ukweli.” 

Kwa upande wa serikali ya Qatar, Waziri wa Afya ya Umma wa nchi hiyo, Dkt Hanan Mohamed Al Kuwari, amesema, "wizara inajivunia kushirikiana na FIFA na WHO ili kukuza ushirikiano wa kimataifa na kuhakikisha usalama na afya ya wote. Wakati janga hilo likiendelea kudhibitiwa nchini Qatar, tishio la janga hilo bado liko ulimwenguni kote, na kwa bahati mbaya ufikiaji wa zana za kushinda virusi unabaki kuwa mdogo kwa nchi nyingi.” 

Kwa kutumia uzinduzi wa Kombe la Kiarabu la FIFA 2021 kusambaza ujumbe, FIFA na washirika wake wanasisitiza kujitolea kwao kwa usawa katika kulinda afya ya umma, kuangazia maadili ya msingi uwanjani, wakati wote wakiendelea kufuata hatua kuu za afya ya umma.