Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mifumo ya ardhi na maji duniani kote imeathirika vibaya yaonya FAO

Katika kilimo, bidhaa za plastiki husaidia sana tija.
© FAO/Cristina Aldehuela
Katika kilimo, bidhaa za plastiki husaidia sana tija.

Mifumo ya ardhi na maji duniani kote imeathirika vibaya yaonya FAO

Tabianchi na mazingira

Rasilimali za ardhi na maji ziko katika shinikizo la hali ya juu kufuatia kuzorota kwa kiasi kikubwa mifumo ya rasilimali hizo katika muongo mmoja uliopita, kulingana na ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO. 

Ripoti hiyo inayoitwa, “Hali ya rasilimali za ardhi na maji duniani kwa chakula na kilimo :Mifumo iliyo karibu kusambaratika (SOLAW 2021)”, inaangazia changamoto zilizopo katika kulisha idadi ya watu duniani ambayo inapaswa kukaribia bilioni kumi ifikapo 2050. 

Katika uzinduzi wa ripoti hiyo mkurugenzi mkuu wa FAO, QU Dongyu, amesema kuwa "Mifumo ya sasa ya uzalishaji wa mazao ya kilimo haithibitishi kuwa endelevu." 

Hata hivyo, ameongeza kuwa mifumo hii "inaweza kuchukua jukumu kubwa katika kupunguza shinikizo hizi na kuchangia vyema katika malengo ya mabadiliko ya tabianchi na maendeleo." 

Yaliyobainiwa na ripoti 

Ripoti imebaini kwamnba endfapo dunia itaendelea na mwelekeo wa sasa, kuzalisha asilimia 50 ya ziada ya chakula kinachohitajika, kunaweza kumaanisha ongezeko la asilimia 35, katika uupunguzaji wa maji yanayohitajika kwa kilimo. 

Hiyo inaweza kusababisha majanga ya kimazingira, kuongeza ushindani wa rasilimali, na kuchochea changamoto mpya za kijamii na migogoro. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo hivi sasa, uharibifu wa udongo unaosababishwa na binadamu unaathiri asilimia 34 (karibu ekari milioni 1,660), za ardhi ya kilimo. 

Ingawa zaidi ya asilimia 95 ya chakula chote kinazalishwa ardhini, kuna nafasi ndogo ya kupanua eneo ambalo linaweza kufanywa kuwa na tija zaidi. 

FAO imesema “Kwa kweli, maeneo ya mijini hayachukui zaidi ya asilimia 0.5 ya uso wa ardhi wa dunia, lakini ukuaji wa haraka wa miji umepunguza rasilimali kwa kiasi kikubwa, kuchafua mazingira na kupenya katika ardhi za kilimo.” 

Katika miaka 17 pekee,  matokeo ya ripoti yanaonyesha kwamba kati ya mwaka 2000 na 2017, matumizi ya ardhi kwa kila mtu yalipungua kwa asilimia 20. 

Uhaba wa maji sasa unatishia watu bilioni 3.2 wanaoishi katika maeneo ya kilimo. 

Wanawake wanafanya kazi katika mradi wa kuhifadhi udongo kama sehemu ya Mpango wa Dunia wa Kustahimili Ustahimilivu na Mabadiliko ya Tabianchi nchini El Salvador.
WFP/Rein Skullerud
Wanawake wanafanya kazi katika mradi wa kuhifadhi udongo kama sehemu ya Mpango wa Dunia wa Kustahimili Ustahimilivu na Mabadiliko ya Tabianchi nchini El Salvador.

Suluhu tulizonazo 

FAO inaamini kwamba kuongezeka kwa kasi kwa teknolojia na uvumbuzi ni muhimu ili kukabiliana na changamoto hizi. 

Inasema ulimwengu unahitaji kuimarisha mifumo ya kidijitali inayotoa takwimu za msingi, taarifa na masuluhisho ya kisayansi kwa kilimo. 

Utawala wa ardhi na maji lazima ujumuishe zaidi na ubadilike, ili kufaidisha mamilioni ya wakulima wadogo, wanawake, vijana na watu wa asili, ambao ndio walio hatarini zaidi, kukabiliana na uhaba mkubwa wa chakula. 

Pia kunahitajika kuwa na mipango jumuishi zaidi katika ngazi zote, ripoti inasema, na uwekezaji katika kilimo lazima uelekezwe kwenye faida za kijamii na kimazingira. 

Na hatimaye, FAO inasema kuwa matumizi endelevu ya rasilimali hizi ni muhimu katika kufikia malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuweka mipango ya malengo ya kujenga mnepo. 

Pia matumizi mazuri ya udongo, kwa mfano, yanaweza kuchukua theluthi moja ya uzalishaji wa gesi chafu kutoka kwaenye ardhi ya kilimo.