Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna wa haki za binadamu ataka kukomeshwa mara moja kwa uhasama Sudan 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk akikutana na viongozi wa mashirika ya kiraia nchini Sudan.
OHCHR/Anthony Headley
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk akikutana na viongozi wa mashirika ya kiraia nchini Sudan.

Kamishna wa haki za binadamu ataka kukomeshwa mara moja kwa uhasama Sudan 

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk leo ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama nchini Sudan na kuwasihi Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka kurejea kwenye meza ya mazungumzo. 

"Sudan tayari imevumilia maumivu na mateso mengi. Mapigano hayo yanatokana na michezo ya madaraka na masilahi ya kibinafsi ambayo yanasaidia tu kutenganisha matarajio ya kidemokrasia ya watu," Türk amesema na akiongeza kuhoji "Je, wale wanaohusika hawaelewi kwamba raia sasa wanatamani tu maisha ya amani?" 

Mapigano mengi yamejikita katika maeneo yenye wakazi wengi wa mji mkuu Khartoum na maeneo ya makazi ya miji kwingineko nchini humo. Mashambulizi ya anga na mizinga, ikiwa ni pamoja na utumiaji wa silaha za milipuko zenye athari za eneo kubwa, yameweka raia katika hatari ya kifo na majeraha, Kamishna Mkuu amesema. Katika muda wa siku nne tangu mapigano kuanza, takriban watu 185 wameuawa na 1,800 kujeruhiwa. 

"Maelfu kwa maelfu ya raia wamekwama katika nyumba zao, wakijikinga na mapigano, bila umeme, hawawezi kutoka nje na wana wasiwasi wa kukosa chakula, maji ya kunywa na dawa," Türk ameeleza.  

Sheria za kimataifa

"Pande zote mbili lazima ziwakumbushe wapiganaji wao wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kuhakikisha ulinzi wa raia na miundombinu ya kiraia kama vile shule na hospitali, na lazima kuhakikisha kwamba majukumu haya yanaheshimiwa." 

Kamishna Mkuu pia amesema anashangazwa na ripoti za jaribio la ubakaji. 

Ametoa wito wa uchunguzi wa haraka, wa kina na huru kuhusu mauaji ya raia, wakiwemo wafanyakazi watatu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, pamoja na ukiukaji mwingine ulioripotiwa. Wale waliohusika lazima wawajibishwe, Türk amesisitiza. 

"Wiki chache tu zilizopita, Sudan ilionekana kuwa katika njia sahihi kuelekea makubaliano ambayo yangerejesha utawala wa kiraia," amesema. "Akili ya kawaida lazima itawale, na pande zote lazima zichukue hatua ili kupunguza mvutano. Maslahi ya pamoja ya watu wa Sudan lazima yatangulie."