Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel-Palestine: Mateso yasiyovumilika ya raia huko Gaza yanataka kukomeshwa kwa ghasia, asema Türk

Wanawake wa Kipalestina wakiomboleza kifo cha mwanafamilia mmoja katika Hospitali ya Matibabu ya Al-Nasser huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
©UNICEF/UNI472270/Zaqout
Wanawake wa Kipalestina wakiomboleza kifo cha mwanafamilia mmoja katika Hospitali ya Matibabu ya Al-Nasser huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Israel-Palestine: Mateso yasiyovumilika ya raia huko Gaza yanataka kukomeshwa kwa ghasia, asema Türk

Amani na Usalama

Kurejea kwa mapigano huko Gaza na athari zake za kutisha kwa raia kunasisitiza haja ya ghasia kukomesha na suluhu la muda mrefu la kisiasa kati ya Wapalestina na Waisraeli kupatikana, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema leo Jumapili.

"Nyamazisha bunduki na mrejee kwenye mazungumzo - mateso wanayopata raia ni mengi sana kuyastahimili. Vurugu zaidi sio jibu. Haitaleta amani wala usalama, "Volker Türk amesema katika taarifa yake, akionesha wasiwasi mkubwa kwamba mazungumzo ya kuendelea kwa usitishaji mapigano ya wiki iliyopita yameripotiwa kukwama.

Mapigano yalianza tena Ijumaa (ya tarehe 1 Desemba) na mamia ya Wapalestina wameuawa na mashambulizi ya Israel, amesema, akinukuu Wizara ya Afya ya Gaza.

Hakuna msaada ulioingia katika eneo hilo kupitia kivuko cha Rafah na Misri siku ya Ijumaa, na usambazaji siku ya Jumamosi ulizuiwa, na kuathiri zaidi shughuli za kibinadamu kusaidia mamilioni ya watu huku kukiwa na uhaba wa chakula, maji, mafuta na mambo mengine muhimu.

Hakuna sehemu salama

Bwana Türk anahofia kwamba uhasama huo uliozuka upya utasababisha vifo, magonjwa, na uharibifu zaidi.

"Kutokana na mwenendo wa uhasama wa Israel na maagizo yake kwa watu kuondoka kaskazini na sehemu za kusini, mamia kwa maelfu wanazuiliwa katika maeneo madogo zaidi kusini mwa Gaza bila ya usafi wa mazingira, upatikanaji wa chakula cha kutosha, maji na vifaa vya afya,wakati mabomu yakidondoka karibu nao,” akasema na kuongeza “hakuna mahali salama katika Gaza.”

Amesisitiza kuwa sheria za kimataifa na sheria za haki za binadamu zinasisitiza ulinzi wa raia na kuwezesha upatikanaji wa kibinadamu bila vikwazo kwa watu wanaohitaji.

Wasiwasi kuhusu kaskazini mwa Gaza

Mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa pia ameangazia jinsi mamia kwa maelfu ya watu waliosalia kaskazini mwa Gaza wako katika hatari mpya ya kushambuliwa kwa mabomu na kuendelea kunyimwa chakula na mambo mengine muhimu.

Amesema hali hii ya kutisha na maagizo ya kuhamia kusini yanamaanisha kwamba watu kimsingi wanalazimishwa kuhama katika kile kinachoonekana kuwa ni jaribio la kuwaondoa Wapalestina eneo la kaskazini mwa Gaza.

Badilisha mwelekeo sasa

Türk amezitaka Nchi Wanachama kufanya kila wawezalo ili kuhakikisha pande zote zinatii wajibu wao chini ya sheria za kimataifa na kuzuia kutendeka kwa uhalifu wa kimataifa.

“Wakati wa kubadili mkondo ni sasa. Wale wanaochagua kukiuka sheria za kimataifa wanataarifiwa kwamba uwajibikaji utafanyika. Hakuna aliye juu ya sheria,” amesema Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Volker Türk.