Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Türk alaani kuuawa kwa Kenneth Eugene Smith kwa hewa ya Nitrojeni hypoxia

Mwanaharakati akiwa na ishara za kupinga adhabu ya kifo nje ya jengo la mahakama kuu ya Marekani mjini Washington.
© Unsplash/Maria Oswalt
Mwanaharakati akiwa na ishara za kupinga adhabu ya kifo nje ya jengo la mahakama kuu ya Marekani mjini Washington.

Türk alaani kuuawa kwa Kenneth Eugene Smith kwa hewa ya Nitrojeni hypoxia

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, Volker Türk amesikitishwa na mauaji ya Kenneth Eugene Smith mkazi wa Alabama nchini Marekani yaliyofanyika kwa kutumia gesi ya Nitrojeni hypoxia.

 

Smith aliuawa usiku wa Alhamisi ya tarehe 25 Januari 2024 kwa saa za Marekani kwa kutumia gesi hiyo licha ya wito wa watetezi wa haki za binadamu wa kuteka kitendo hicho kisifanyike.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na ofisi ya Kamishna Türk, imemnukuu akisema utekelezaji wa hukumu ya kifo dhidi ya Smith kwa kutumia gesi hiyo umefanyika licha ya hofu iliyokuweko ya matumizi ya mbinu hiyo mpya ya kuua na ambayo haijajaribiwa kwamba inaweza kuwa ni utesaji au ukatili na udhalilishaji kwa yule ambaye adhabu hiyo imetumika dhidi yake.

Adhabu hiyo mpya ya hukumu ya kifo kwa matumizi ya gesi ya Nitrojeni hypoxia iliidhinishwa na mamlaka za jimbo la Alabama nchini Marekani hivi karibuni. 

Katika taarifa yake Bwana Türk amesema “adhabu ya kifo ni kinyume na haki ya msingi ya uhai. Nasihi nchi zote zikomeshe matumizi ya adhabu hiyo kama njia ya kuelekea kufuta kabisa adhabu hiyo duniani kote."