Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wafungwa 900 waachiliwa huru nchini Yemen

Kitongoji cha Al Gahmalyya katika mji wa Taiz, Yemen, kimeharibiwa vibaya kutokana na mzozo wa miaka mingi.
© WFP/Mohammed Awadh
Kitongoji cha Al Gahmalyya katika mji wa Taiz, Yemen, kimeharibiwa vibaya kutokana na mzozo wa miaka mingi.

Zaidi ya wafungwa 900 waachiliwa huru nchini Yemen

Amani na Usalama

Zaidi ya wafungwa 900 waliokuwa wameshikiliwa na pande zinazokinzana nchini Yemen wameachiliwa huru hii leo na zoezi hilo linatarajiwa kuendelea kwa siku tatu zijazo ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa mwezi Machi mwaka huu nchini Uswisi kati ya pande hizo.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen OSESGY imesema mwakilishi huyo  Hans Grundberg amezipongeza pande zote kwa kuteleza makubaliano ya kubadilisha wafungwa zoezi linalosimamiwa kwa ushirikiano na ofisi yake na kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu ICRC.

“Operesheni hii imekuja wakati huu wa matumaini kwa Yemen ikikumbusha kuwa mazungumzo ya kujenga na maelewano ya pande zote ni zana zenye nguvu zinazoweza kufikia matokeo mazuri. Leo, mamia ya familia za Yemen zita sherehekea Sikukuu ya Eid na wapendwa wao kwa sababu wahusika wa pande zinazo zozana walijadiliana na wamefikia makubaliano. Natumaini roho hii itaendelea katika juhudi zinazoendelea za kusaka suluhu za kisiasa.”

Mipango ya baadae

Pande zinazopigana nchini Yemen zinatarajia kukutana tena mwezi Mei ili kuweka mipango zaidi ya kuwaachia wafungwa wengine.

“Maelfu ya familia bado wanangoja kuunganishwa tena na wapendwa wao. Natumai wahusika wa pande zote wataendeleza mafanikio ya operesheni hii ili kutimiza ahadi waliyotoa kwa watu wa Yemen katika Mkataba wa Stockholm wa kuwaachia wafungwa wote wanaohusishwa na migogoro na hatimaye kumaliza kabisa mateso haya,” amesema Grundberg.

Katika operesheni hiyo, ICRC inahusika na kuandaa ndege zitakazo safirisha wafungwa walioachiwa kati ya viwanja sita nchini Yemen na Saudi Arabia ndani ya kipindi cha siku hizo tatu za kuwaachia wafungwa huru.