Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande kinzani Yemen zaafikiana kuachilia wafungwa zaidi ya 1,000 

Ujumbe wa wawakilishi wa serikali ya Yemen na kundi la Ansar Allah wakiwa na wenyeviti wa kamati ya ushauri, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Yemen Martin Griffiths na mkurugenzi wa kikanda wa ICRC Fabrizio (Kushoto) , 27 Septemba 2020
ICRC
Ujumbe wa wawakilishi wa serikali ya Yemen na kundi la Ansar Allah wakiwa na wenyeviti wa kamati ya ushauri, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Yemen Martin Griffiths na mkurugenzi wa kikanda wa ICRC Fabrizio (Kushoto) , 27 Septemba 2020

Pande kinzani Yemen zaafikiana kuachilia wafungwa zaidi ya 1,000 

Amani na Usalama

Katika mwisho wa mazungumzo ya wiki moja yaliyokuwa yakifanyika nchini Uswis pande kinzani kwenye mzozo wa Yemen zimefikia muafaka katika kile mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen alichokiita hatua muhimu ya kihistoria ya kuachilia awamu ya kwanza ya kundi la wafiungwa. 

Wajumbe kutoka serikali ya Yemen na kundi la Ansar Allah ambalo awali lilijulikana kama waasi wa Houthi wametia Saini muafaka huo leo Jumapili wa kuwaachilia wafungwa 1,081 waliokuwa wakishikiliwa kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo na wameachiliwa kufuatia kukubalina majina yao. 

“Leo ni siku muhimu sana kwa familia zaidi ya 1000 ambazo zitarajie kuwakaribisha tena nyumbani wapendwa wao na matumaini ni kwamba itakuwa muda si mrefu”amesema Martin Griffiths mwakilishi wa Umoja wa Mataifa yemen baada ya kukamilika kwa mkutano wa nne wa kamati ya usimamizi wa utekelezaji wa makubaliano ya kubadilishana wafungwa ambao uliongozwa kwa pamoja na ofisi yake na kamati ya kimataifa ya chama cha msalaba mwekundu (ICRC). 

Mchakato wa amani unaendelea 

Wanawake wakiwa wamepanga foleni kwenye kituo cha mgao kambini Kharaz nchini Yemen, ambako pia hatua za kukabiliana na Corona zinazingatiwa.
© UNOCHA/Mahmoud Fadel
Wanawake wakiwa wamepanga foleni kwenye kituo cha mgao kambini Kharaz nchini Yemen, ambako pia hatua za kukabiliana na Corona zinazingatiwa.

Hatua hiyo inatekeleza mpango wa makubaliano yaliyoafikiwa mjini Amman mwezi Februari mwaka jana. Pia wajumbe hao wamekubaliana kuitisha mkutano mwingine wa kamati ya ushauri kwa lengo la kutekeleza matokeo yaliyosalia ya makubalino ya mkutano wa Amman. 

Ama kuhusu makubaliano ya 2018 ya Stockholm pande hizo zimerejea ahadi zao za kuachilia wafungwa wote, mahabusu, watu ambao hawajulikani waliko, watu wanaoshikiliwa kinyume na sheria, watu waliotoweshwa kwa lazima na walio katika vifungo bvya nyumbani. 

Zaidi ya hapo pande hizo zimeahidi kufanya kila juhudi kuongeza idadi ya wafungwa wa kuachiliwa ikiwemo wale waliotajwa kwenye maazimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Bwana Griffiths ameongeza kuwa“Nazishukuru pande zote kwa kwenda mbali zaidi, kuweka kando tofauti zao na kufikia makubaliano ambayo yatawanufaisha watu wa Yemen. Nazitaka pande zote kusonga mbele kwa kuwaachilia wafungwa hao mara moja na kufanya kila liwezekenalo kuendeleza mchakato huu ili kuweza kukubalina kuwaachilia wafungwa zaidi. Kwa kufanya hivyo Umoja wa Mataifa utatimiza ahadi yake uliyoitoa Stockholm na kukomesha madhila kwa familia nyingi za Wayemen ambazo zinawasubiri wapendwa wao.”

Familia iliyofurushwa mjini Marib, Yemen, wakiwa wamebeba msaada waliopewa kurejea katika eneo lao la malazi. Matatizo kama haya huwafanya watu kutaka kuzikimbia nchi zao kwenda kutafuta maisha kwingine.
IOM
Familia iliyofurushwa mjini Marib, Yemen, wakiwa wamebeba msaada waliopewa kurejea katika eneo lao la malazi. Matatizo kama haya huwafanya watu kutaka kuzikimbia nchi zao kwenda kutafuta maisha kwingine.

Kuzifanya ahadi kuwa hatua za vitendo 

Mwenyekiti mwenza wa ICRC kanda ya Mashariki ya Kati nay a Karibu Fabrizio Carboni ameuita muafaka huo kuwa ni“Hatua chanya kwa mamia ya wafungwa na familia zao huko nyumbani ambao wametenganishwa kwa miaka na sasa wataunganishwa tena hivi karibuni.” 

Hata hivyo ameeleza kwamba hatua hii ni mwanzo tu wa mchakato unaoendelea na amezichagiza pande zote kuendelea na uharaka na kukubalia mpango Madhubuti wa utekelezaji“ili operesheni hii iweze kusonga mbele kutoka kwenye utiaji Saini kwenye makatratasi na kuwa hali halisi mashinani. “ 

Bwana Griffithi ametoa wito kwa pande zote“kuendeleza mafanikio haya muhimu na kusonga mbele kwa pamoja kuelekea suluhu ya pamoja ya kuleta amani ya kudumu Yemen. Umoja wa Mataifa uko tayari kuzisaidia pande zote pamoja na watu wa Yemen kutimiza lengo hili.”