Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN ina wasiwasi kuhusu kesi dhidi ya Jaji Kisaakye wa Mahakama Kuu nchini Uganda

Kampala, Makao Makuu ya Uganda
Unsplash/Drew Willson
Kampala, Makao Makuu ya Uganda

UN ina wasiwasi kuhusu kesi dhidi ya Jaji Kisaakye wa Mahakama Kuu nchini Uganda

Haki za binadamu

Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa majaji na mawakili Margaret Satterthwaite ameonesha wasiwasi wake mkubwa kuwa kesi za kinidhamu zilizoendeshwa dhidi ya Jaji wa Mahakama Kuu nchini Uganda Esther Kisaakye huenda zikawa sawa na kulipiza kisasi dhidi yake kwa kutekeleza majukumu yake ya kimahakama.

Taarifa iliyotolewa leo jijini Geneva Uswisi ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa mwaka 2021, Jaji Esther Kisaakye alitoa uamuzi pekee uliopinga katika ombi la uchaguzi kati ya kiongozi mkuu wa chama cha upinzani Bobi Wine na rais aliye madarakani Yoweri Museveni, uamuzi wa kumpa kiongozi huyo wa upinzani muda zaidi wa kurekebisha malalamiko yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa majaji na mawakili Margaret Satterthwaite alionyesha wasiwasi wake mkubwa kwamba kesi za kinidhamu dhidi ya Jaji Kisaakye "zilikuwa na kasoro za kiutaratibu" na zinatokana na matukio yanayohusiana na uamuzi wake katika kesi iliyohusu uchaguzi wa rais wa 2021 Uganda.

Mwaka 2021, Jaji Esther Kisaakye alitoa uamuzi pekee katika shauri la kupinga uchaguzi kati ya kiongozi mkuu wa chama cha upinzani Bobi Wine na rais aliye madarakani Yoweri Museveni, uamuzi wa kumpa kiongozi huyo wa upinzani muda zaidi wa kurekebisha malalamiko yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema "Majaji hawapaswi kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na maudhui ya maamuzi yao halali. Iwapo Jaji Kisaakye angekabiliwa na vikwazo kutokana na kutaka kutoa maoni tofauti katika kesi hiyo ya ngazi ya juu basi itakuwa ni kinyume na kanuni ya msingi ya uhuru wa mahakama.”

Nini kilitokea

Tarehe 18 machi 2021 kulikuwa na sintofahamu iwapo Jaji Kisaakye anaweza kutoa uamuzi wa uchaguzi huo wa urais bila ya kuwaonesha wenzake nakala ya hukumu yake. Inadaiwa kuwa Jaji huyo alipotaka kuingia kwenye chumba cha mahakama, maafisa wa polisi walidaiwa kumnyang’anya mafaili yake, wakafunga chumba cha mahakama na kuzima taa.

Zoezi hilo la kutoa hukumu lilishindikana pia siku iliyofuata kwani mahakama ilifungwa na kumnyima Jaji Kisaakye kuingia, na mpaka leo jaji huyo bado hajarejeshewa mafaili yake.

Siku iliyofuata, Machi 19, chumba cha mahakama kilifungwa, na kumnyima Jaji Kisaakye kuingia, ambaye alikusudia kutoa uamuzi kuhusu ombi linalohusiana na hilo kuhusu kujiuzulu kwa Jaji Mkuu. Kufikia sasa, Jaji Kisaakye hajaweza kurejesha faili zake.

Tarehe 20 Machi, Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) ilianzisha uchunguzi kuhusu matukio hayo. Na ndio hapa ambapo Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa anasema kuna wasiwasi kwamba kesi za JSC dhidi ya Jaji Kisaakye zimekuwa na kasoro za kiutaratibu na zinatokana na matukio yanayohusiana na uamuzi wake katika kesi iliyohusu uchaguzi wa rais wa 2021 Uganda.

Kesi dhidi ya jaji Kisaakye

Mnamo tarehe 8 Februari 2023, Tume ilihitimisha kuwa kesi ya awali iliundwa kuhusu madai ya utovu wa nidhamu ya Jaji Kisaakye na kupendekeza Rais ateue mahakama itakayozingatia suala la kuondolewa madarakani kwa Jaji Kisaakye.

Jaji Kisaakye anaweza kusimamishwa kazi wakati wa uchunguzi wa mahakama hiyo.

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa majaji na mawakili Satterthwaite amesema “Sheria na viwango vya kimataifa vinahitaji kwamba pale ambapo kuna madai ya utovu wa nidhamu kitaaluma, haki ya kusikilizwa kwa haki ni pamoja na haki ya kujulishwa ipasavyo kuhusu mashtaka na mashauri yoyote ya kinidhamu yatakayo chukuliwa.”

Ameeleza kuwa kuondolewa kwa jaji bila kufuata utaratibu ni pigo kubwa kwa uhuru wa mahakama. Na ni wajibu wa serikali zote kuheshimu na kuzingatia uhuru wa mahakama.

Satterthwaite amehitimisha taarifa yake kwakusema “Chini ya viwango vya kimataifa, majaji wanaweza kusimamishwa kazi au kuondolewa tu kwa sababu za kutokuwa na uwezo au tabia iliyothibitishwa ambayo inawafanya kutofaa kutekeleza majukumu yao, na kwa mujibu wa utaratibu unaofaa mbele ya chombo huru.”

Mtaalamu huyo Maalum amekuwa akiwasiliana na Serikali ya Uganda kuhusu madai haya.