Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya UN ya Haki za Binadamu Uganda yafungwa; Türk asikitishwa

Kampala, Mji Mkuu wa Uganda
Unsplash/Drew Willson
Kampala, Mji Mkuu wa Uganda

Ofisi ya UN ya Haki za Binadamu Uganda yafungwa; Türk asikitishwa

Haki za binadamu

Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu  UN Volker Türk, hii leo ameelezea masikitiko yake makubwa kufuatia kufungwa kwa ofisi yake nchini Uganda kufuatia uamuzi wa serikali hiyo kutotia saini mkataba wa kuendelea kuweko kwa ofisi hiyo nchini humo.

Taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR) imesema tayari ofisi ndogo za Gulu na Maroto zilifungwa tarehe 30 Juni na 31 Julai mtawalia, huku ofisi kuu ya jijini Kampala ikifungwa kesho Jumamosi Agosti 5. 

Bwana Türk  amesema “nasikitika ofisi yetu Uganda inafungwa baada ya kuweko nchini humo kwa miaka 18, ambapo tuliweza kushirikiana na mashirika ya kiraia, watu kutoka pande mbalimbali nchini Uganda pamoja na taasisi za serikali kusongesha na kulinda haki za binaamu za waganda wote.” 

Amesema tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo mwaka 2005 wameshirikiana na serikali na wadau kwenye masuala kama vile kujumuisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kwenye mipango ya kitaifa na kushauri juu ya kuoanisha sheria za nchi na sheria za kimataifa za haki za binadamu. 

Hata hivyo amesema licha ya maendeleo makubwa yaliyopatikana kwenye haki za binadamu Uganda bado kuna changamoto kubwa za haki za binadmau, akitaja hususan hofu juu ya haki za binadamu kuelekea uchaguzi mkuu wa Uganda mwaka 2026 ambako watetezi wa haki, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira magumu. 

Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu  UN Volker Türk
OHCHR
Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu UN Volker Türk

Bwana Türk ameonya juu ya uwezekano wa kudorora kwa ahadi za Uganda kwenye mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu iliyoridhia, ikiwemo kupitishwa kwa sheria dhidi ya ushoga ambayo tayari imekuwa na madhara kwa waganda. 

Kamishna huyo Mkuu wa Haki za Binadamu ameisihi serikali ya Uganda ihakikishe kuwa taasisi ya kitaifa ya haki za binadamu inafanya kazi kwa ufanisi, kwa uhuru kama chombo chenye jukumu la kusimamia haki nchini humo. 

Amesema kwa upande wake, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu inasalia kuendelea kushughulikia haki za binadamu Uganda kwa mujibu wa mamlaka ya kimataifa.