Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres atiwa hofu na sheria mpya Uganda dhidi ya ushoga

Moja ya mtaa katikati ya mji mkuu wa Uganda, Kampala
UN News/ Conor Lennon
Moja ya mtaa katikati ya mji mkuu wa Uganda, Kampala

Guterres atiwa hofu na sheria mpya Uganda dhidi ya ushoga

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ana hofu kubwa baada ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni kusaini Sheria dhidi ya Ushoga nchini humo.

Taarifa iliyotolewa Jumanne usiku na msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema sheria hiyo katili na onevu inaelekeza adhabu ya kifo au kifungo cha muda mrefu gerezani kwa tendo la kujamiiana kati ya watu wazima.

Kanuni  ya kutobagua

Bwana Guterres ametoa wito kwa Uganda kuheshimu wajibu wake kwa sheria za kimataifa, “hususan kanuni ya kutobagua na kuheshimu faragha ya mtu,” bila kujali utambulisho wa mtu kijinsia.

Ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutokomeza uharamishaji wa kitendo cha watu wa jinsia moja kuridhia kujamiiana.

Kwa mujibu wa mpango wa pamoja wa Umoja wa MAtaifa wa kukotokomeza Virusi vya Ukimwi na UKIMWI, UNAIDS, uharamishaji huo unaendelea katika nchi 67 duniani kote, ambapo kati ya hizo, nchi 10 zinatoa adhabu ya kifo.

Inadumaza maendeleo

Wiki iliyopita, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Türk alisema sheria za kupinga mahusiano ya jinsia moja, kubadili jinsia au ushoga, (LGBTQI) kama ya Uganda, “inaleta ukinzani baina ya watu na kuacha wengine nyuma huku maendeleo yakidumazwa.”

Katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa mwezi Machi, wakati Bunge la Uganda lilipopitisha kwa mara ya kwanza sheria hiyo, Bwana Türk  aliielezea sheria hiyo ya kibaguzi kama tatizo kubwa kwa maendeleo, na kwamba inaweza kuwa moja yasheria mbaya zaidi za aina hiyo duniani.

“Iwapo itatiwa saini kuwa sheria na Rais, itafanya wasagaji, mashoga na wanaegemea pande zote nchini Uganda kuwa wahalifu kwa uwepo wao tu, au kwa kuwa walivyo. Inaweza kutoa ruhusa kwa kuweko kwa mfumo wa ukiukwaji wa haki zote za kibinadamu na kuchochea chuki baina ya watu,” alisema Bwana Türk.

‘Inapeleka kando' vita dhidi ya ukatili wa kingono

Muswada wa sheria hiyo, ulipitishwa rasmi tarehe 21 mwezi Machi mwaka huu, ukipendekeza adhabu ya kifo kwa ushoga unaoudhi au kuchukia, kifungo cha maisha kwa kosha la ushoga na hadi kifungo cha miaka 14 kwa kujaribu ushoga na kifungo cha hadi miaka 20 kwa kuchagiza ushoga.

Bwana. Türk alisema sheria hiyo itapeleka mrama harakati za lazima za kutokomeza ukatili wa kingono.

Ameonya kuwa itawaweka gerezani muda mrefu waandishi wa habari , wahudumu wa afya na watetezi wa haki za binadamu kwa kutokana tun a kufanya kazi zao.