Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CODECO waendelea kuua raia DRC, MONUSCO yazidi kuimarisha ulinzi

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwenye ujumbe wa kulinda amani, DRC, MONUSCO wakiwa doriani kujibu mashambulizi baada ya kupata taarifa za CODECO kushambulia raia huo Djugu, jimboni Ituri. (Mei 4, 2022)
Kikosi cha MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwenye ujumbe wa kulinda amani, DRC, MONUSCO wakiwa doriani kujibu mashambulizi baada ya kupata taarifa za CODECO kushambulia raia huo Djugu, jimboni Ituri. (Mei 4, 2022)

CODECO waendelea kuua raia DRC, MONUSCO yazidi kuimarisha ulinzi

Amani na Usalama

Usiku wa kuamkia leo huo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, wanamgambo wa kikundi cha CODECO wameshambulia kambi ya Plaine Savo jimbo Ituri na kuua wakimbizi wa ndani 7 huku wengine wengi wakilazimika kukimbia makazi yao.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani kwamba kwa mujibu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, shambulio hilo limetokea takribani kilometa 9 kutoka Djugu mji mkuu wa Ituri.

Walinda amani wa UN walipelekwa mara moja kulinda kambi hiyo na kuepusha mashambulizi zaidi.

Shambulio hili limekuja takribani mwaka mmoja tangu kutokea kwa shambulio kubwa la mwezi Februari mwaka 2022 ambalo lilisababisha vifo vya watu takribani 60.

Halikadhalika limefanyika siku chache tangu kubainika kwa makaburi mawili ya halaiki yakiwa na jumla ya maiti 49 wakiwemo wanawake, watoto na wanaume kwenye vijiji vya Nyamamba na Mbogi vilivyoshambuliwa na CODECO mwishoni mwa wiki.

Mfululizo wa mashambulizi Ituri wafurusha wahudumu wa kibinadamu

Bwana Haq amesema matukio haya mapya ni sehemu ya mfululizo wa mashambulizi dhidi ya raia katika wiki chache zilizopita, matukio ambayo yanaathiri operesheni za usaidizi wa kibinadamu huko Djugu na mji Jirani wa Mahagi.

Halikadhalika matukio haya yanazidi kupanua wigo wa janga la kibinadamu jimboni Ituru ambako tayari kuna takribani wakimbizi wa ndani milioni 1.5.

Tangu mapema mwezi huu wa Januari takrbani mashirika 12 ya kiutu yamepunguza operesheni zao kwenye miji ya Djugu na Mahagi kutokana na ongezeoko la ukosefu wa usalama.

MONUSCO kwa sasa inafuatilia kwa karibu kile kinachotokea huku ikisihi mamlaka husika kuhakikisha ulinzi wa raia, hasa kambini.

“Halikadhalika tunawasiliana na wadau wa kiutu ili waendelee kutoa misaada kadri hali ya usalama itakavyoruhusu,” ametamatisha Bwana Haq.