Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yataka hatua za mabadiliko makubwa kutokomeza janga la maji duniani

Watoto wakinawa mikono katika bomba la maji kwenye shule yao ya msingi nchini Uganda
© UNICEF/Proscovia Nakibuuka
Watoto wakinawa mikono katika bomba la maji kwenye shule yao ya msingi nchini Uganda

UN yataka hatua za mabadiliko makubwa kutokomeza janga la maji duniani

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa siku 3 wa Umoja wa Mataifa kuhusu maji duniani umeng’oa nanga hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani huku kauli zikitolewa kutaka majawabu ya kibunifu, hatua za kasi na  uwekezaji zaidi kwenye sekta ya maji duniani wakati huu ambapo rasilimali hiyo adhimu inakumbwa na uchafuzi, matumizi kupindukia na usimamizi wake unakumbwa na changamoto.

Washiriki wa mkutano huo wana matarajio ya kuondoka na ahadi za kijasiri kwa lengo la kutatua janga la maji duniani wakati huu ambapo kuna shinikizo kubwa la maji kuanzia uhitaji wa matumizi, ongezeko la uchafuzi wa maji na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa António Guterres amesema “huu ni aidi ya mkutano kuhusu maji. Ni mkutano juu ya dunia ya leo inayoonekana kutoka katika mtazamo wa rasilimali yake adhimu zaidi duniani. Mkutano huu lazima usongeshe kwa kasi na na kwa mapana uwezo wa nchi wanachama na jamii ya kimataifa wa kutambua na kuchukua hatua juu ya umuhimu wa maji kwa ajili ya uendelevu wa dunia na pia kama mbinu ya kuchagiza amani na ushirikiano wa kimataifa.”

Maji yapate hadhi inayostahili

Mathalani, kutoka maji kama kichocheo kikuu cha uchumi na utungaji wa sera, hadi kutambua maji na huduma za kujisafi kama haki ya binadamu.

Kutoka kujumuisha maji na sera za tabianchi hadi kuwa na hatua bunifu katika matumizi ya maji kwenye uzalishaji wa chakula.

Kwa Csaba Kőrösi, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yeye amehoji, tunapaswa kufanya nini ili kufanikiwa?”

Akataja hatua za kuchukua kuwa ni pamoja na kuendeleza utamaduni wa ufadhili makini kwenye maji, tabianchi na bayonuai. Ufadhili ambao amesema utakuwa na manufaa kwa kila mtu, kuanzia watu wa jamii ya asili na wale wa pembezoni hadi wale waliobahatika ambao wamezaliwa na wazazi wenye uwezo.

“Tunatakiwa kukomesha haraka upotevu wa maji. Kuwa na mzungumko wa matumizi ya maji, yaani kuyatumia tena na tena badala ya kuchimba mengine, huo ndio unapaswa kuwa mwelekeo,” amesema Kőrösi .

Ripoti ya Maendeleo ya Maji duniani 2023
UN News
Ripoti ya Maendeleo ya Maji duniani 2023

Simu za mkononi zimetapakaa kuliko vyoo na maji

Umoja wa Mataifa unasema kuwa upatikanaji wa maji na huduma za kujisafi ni suala muhimu zaidi kwa ajili ya afya na ustawi na pia ni haki ya binadamu. Hata hivyo watu bilioni 2 duniani kote bado hawana huduma ya maji safi na salama ya kunywa.

Watu wengi zaidi wana simu za kiganjani au mkononi kuliko vyoo au huduma za kujisafi, ambapo asilimia 80 ya majitaka yanatiririshwa kwenye mazingira bila kupunguzwa uchafu wake.

Zaidi ya asilimia 80 ya majanga yanahusiana na maji, ambapo mabadiliko ya tabianchi yanaongeza shinikizo.

Mahitaji ya maji kwa binadamu nayo yanazidi kuongezeka ambapo shinikizo la kupata maji linakadiriwa kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 ifikapo mwaka 2050.

Licha ya changamoto hizo, jawabu la kulinda sayari dunia liko dhahiri na hatua lazima zichukuliwe sasa, unasema Umoja wa Mataifa.

Hakuna ‘kulala’ hadi ajenda zote muhimu ziko kwenye nyaraka yetu ya mwisho

“Wakati wa mkutano huu, tunataka sote tuzungushe gurudumu hili la maji,” amesema Willem-Alexander, Mfalme wa Uholanzi ambaye nchi yake na Tajikistan ndio waandaaji wenza wa mkutano huu wa maji, akiongeza “hatutopumzika hadi pale maji yanapatiwa hadhi inayostahili katika ajenda za dunia na sera za miradi. Tutaleta ahadi zetu na hatua zetu katika Ajenda ya Hatua kwa Maji.”

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu maji

Washiriki ni pamoja na viongozi wa serikali na zaidi ya makundi ya kiraia 6,000 yaliyojisajili kushiriki wakiwemo vijana, wataalamu, viongozi wa sekta ya biashara ambapo watatoa majawabu bunifu ya kuchochea marekebisho katika sekta ya maji duniani.

Nyaraka ya mwisho ya mkutano huo ni Ajenda ya Hatua Kwa Maji itakayoweka pamoja ahadi zote kutoka nchi wanachama na wadau wengine kwa lengo la kuleta mabadiliko makubwa yenye majawabu ili kusongesha na kutekeleza lengo namba 6 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama.

Ingawa tayari ahadi mbalimbali zimeshatolewa na zinapatikana mtandaoni, matangazo ya kimsingi ya kujumuisha kwenye nyaraka hiyo yatatolewa wakati wa mkutano.

Mkutano huu umeandaliwa kwa pamoja na Uholanzi na Tajikistan na mara ya mwisho mkutano kama huu ulifanyika mwaka 1977.