Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa maji wa UN wafunga pazia kwa wito wa kuchukua hatua kuhakikisha kila mtu anapata maji

Washiriki wakiwasili UN kwa ajili ya mkutano wa maji wa 2023
UN News/Daniel Dickinson
Washiriki wakiwasili UN kwa ajili ya mkutano wa maji wa 2023

Mkutano wa maji wa UN wafunga pazia kwa wito wa kuchukua hatua kuhakikisha kila mtu anapata maji

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa maji umekunja jamvi mjini New York Marekani kwa kupitishwa “ajenda ya kuchukua hatua” kuhusu suala la maji duniani.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo wa siku tatu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza kuwa “Bila maji hakutokuwa na maendeleo endelevu” huku akiwashukuru wadau wote waliofanikisha mkutano huo wa kihistoria zikiwemo nchi za Uholanzi na Tajikistan kwa kuuandaa lakini pia waliohudhuria nchi wanachama, wanasayansi, wanazuoni, makundi ya asasi za kiraia, watu wa asili, wawakilishi wa sekta binafsi na vijana.

Guterres amesema “Kwa pamoja, maono yenu kabambe na kujitolea kwenu kuchukua hatua na mabadiliko kunatusukuma kuelekea mustakabali endelevu, wenye usawa na unaojumuisha usalama na uhakika sawa wa maji kwa watu na sayari.”

Binti wa miaka 6 akinywa maji kutoka kwenye pumpu ya maji nchini Pakistan
© UNICEF
Binti wa miaka 6 akinywa maji kutoka kwenye pumpu ya maji nchini Pakistan

Ukweli kuhusu maji umedhihirika, 

Katibu Mkuu amesema mkutano huu umedhihirisha ukweli mkuu kwamba kwa manufaa ya kawaida ya wanadamu duniani kote, “maji yanatuunganisha sisi sote. Na yanapitia changamoto lukuki za kimataifa, kwani maji yanahusu afya, usafi wa mazingira, kujisafi na kuzuia magonjwa, maji ni kuhusu amani.”

Ikiwa ni bidhaa ya thamani zaidi kwa manufaa ya binadamu duniani kote, maji yanatuunganisha sote.  Ndiyo maana maji yanahitaji kuwa kitovu cha ajenda ya siasa kimataifa.  Matumaini yote ya binadamu kwa siku zijazo yanategemea kwa namna fulani, mjadala mpya wa kusimamia  na kuhifadhi maji kwa kizazi cha sasa na kijacho. -Katibu Mkuu Antonio Guterres

Ameongeza kuwa pia maji yanahusu maendeleo endelevu, kupambana na umaskini, kusaidia mifumo ya chakula na kutengeneza ajira na ustawi.

“Maji ni kuhusu haki za binadamu na usawa wa kijinsia na ndiyo maana maji yanahitajika kuwa katikati ya ajenda ya kisiasa ya kimataifa.”

Bwana Guterres amesema "Kwa pamoja, maono yenu kabambe na kujitolea kwa hatua na mabadiliko kunatusukuma kuelekea mustakabali endelevu, wenye usawa na unaojumuisha usalama wa maji kwa watu na sayari. Na matumaini yetu yanategemea kuihuisha Ajenda ya Hatua ya Maji iliyoandaliwa wiki hii. Hii ina maana ya kuimarisha suala la maji kama haki ya msingi ya binadamu.”

 Pia amesema inamaanisha kupunguza shinikizo kwenye mfumo wetu wa kihaidrolojia, na kuhakikisha sera nzuri za kufanya maamuzi ambayo ni mahiri.

 Na zaidi ya hapo inamaanisha kuendeleza mifumo mipya ya chakula mbadala ili kupunguza matumizi yasiyo endelevu ya maji katika uzalishaji wa chakula na kilimo.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa walio kwenye kikosi cha kuchukua hatua haraka, QRF nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambao wanatoka Kenya wakisambaza lita 24,000 za maji.
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa walio kwenye kikosi cha kuchukua hatua haraka, QRF nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambao wanatoka Kenya wakisambaza lita 24,000 za maji.

Kubuni mifumo mipya ya kimataifa

Katibu mkuu pia ameongeza kuwa hii inamaanisha kubuni na kutekeleza mfumo mpya wa taarifa za maji duniani ili kuongoza mipango na vipaumbele ifikapo mwaka 2030.

 Pia inamaanisha kujumuisha mbinu yetu kuhusu maji, mazingira na hali ya hewa ili kupunguza utoaji wa gesi chafuzi na kuimarisha jamii kuanzia kwenye miundombinu thabiti, mabomba ya maji na mipango ya kutibu maji machafu, hadi kuhakikisha kila mtu ulimwenguni kote analindwa na mifumo ya tahadhari ya mapema dhidi ya majanga ya asili ifikapo mwaka 2027.

Inamaanisha kuendelea kushinikiza haki ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na hatua za kimataifa kupunguza ongezeko la joto duniani na kusalia kwenye nyuzi joto 1.5.

Na inamaanisha kuongeza kasi ya rasilimali na uwekezaji katika uwezo wa nchi zote kufikia Lengo la 6 la Maendeleo Endelevu.

SDG Goal 6: Maji safi na salama
United Nations
SDG Goal 6: Maji safi na salama

UN inaunga mkono juhudi zote

Akihitimisha tarifa yake Guterres amesema anatarajia kushiriki kwenye mchakato wa tathimini ya lengo hilo wakati wa mikutano ya  kisiasa ya ngazi ya juu itakayofanyika mwezi Julai na kuhakikisha kwamba maji na usafi wa mazingira yanapewa kipaumbele wakati wa mkutano wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs utakaofanyika mwezi Septemba na mikutano mingine ijayo.

“Na ninawahakikishia uungwaji mkono wa kina kutoka mfumo wa Umoja wa Mataifa katika mchakato mzima. Tunapoondoka kwenye mkutano huu wa kihistoria, hebu tujitolee tena kwa mustakabali wetu wa pamoja, hebu tuchukue hatua zinazofuata katika safari yetu ya mustakabali wenye uhakika wa maji kwa wote. Kwa pamoja, mmeileta dunia pamoja katika kutatua changamoto ya maji na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa rasilimali hii muhimu.”

Ukurasa wa kihistoria

Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu Csaba Kőrösi amesema ahadi za dola bilioni 300 zilizotolewa ili kuhimiza mageuzi ya “Ajenda ya Hatua ya Maji” ina uwezo wa kufungua angalau dola trilioni 1 ya faida za kijamii na kiuchumi na mfumo wa ikolojia.

"Matokeo ya mkutano huu sio hati inayofunga kisheria, lakini bado inafungua ukurasa wa kihistoria. Mkutano umethibitisha tena ahadi ya kutekeleza haki ya binadamu ya maji na usafi wa mazingira kwa wote."Hiyo ina maana ni kuwafikia mamilioni ambao hata hawajui kuhusu mkutano huu,” ameongeza Rais huyo wa Baraza Kuu.

Ameendelea kusema kwamba "Tutaweka masikio na akili zetu wazi kwa ushahidi wa kisayansi tunaposonga mbele ili kutambua mabadiliko yaliyojadiliwa.”

Mashirika ya kiraia na sekta kibinafsi ndio kiini cha mageuzi haya na "ufunguo wa mafanikio yetu" amesema, akiongeza kuwa lazima ziwe sehemu ya ushirikiano na ufumbuzi ulio jumuishi zaidi.

Amehitimisha tarifa yake akisema "Leo, tunashikilia vipande vya dunia isiyo na maji na amani mikononi mwetu, Kwa pamoja, tunaweza kuzindua mageuzi kwa ulimwengu usio na maji, na wanamabadiliko wanaweza kutupeleka huko."

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi akizungumza wakati wa mkutano wa maji wa UN 2023
UN Photo/Rick Bajornas
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi akizungumza wakati wa mkutano wa maji wa UN 2023

Ajenda ya Hatua ya Maji ni mwanzo tu

Wakitoa mitazamo na utaalamu mbalimbali ili kukabiliana na changamoto zilizo mbele yao, zaidi ya wawakilishi 2,000 wa serikali, wanasayansi, wasomi, mashirika ya kiraia, watu wa jamii za asili, wanachama wa sekta binafsi, na wajumbe wa vijana wamehudhuria mkutano huo, uliofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kuanzia tarehe 22 hadi 24 Machi.

Li Junhua, msaidizi wa Katibu Mkuu wa masuala ya uchumi na kijamii, amesema ahadi za ajenda za utekelezaji wa maji zinajumuisha hatua mbalimbali, kuanzia kujenga uwezo hadi mifumo ya takwimu na ufuatiliaji, hadi kuboresha mnepo wa miundombinu.

Amesema "Huu ni mwanzo tu. Jukwaa la mtandaoni linaloandaa Agenda ya Hatua ya Maji litaendelea kuwa wazi kwa mawasilisho na linapatikana kwa wote kwa kutazamwa kupitia tovuti ya Mkutano huu."

Matokeo mengine muhimu ya mkutano huo yatakuwa muhtasari wa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, akinasa mawazo mengi, mapendekezo, na ufumbuzi wa kulinda na kuunga mkono "damu yetu ya dunia" ambayo iliibuka wakati wa midahalo mitano ya maingiliano, matukio manne maalum na mamia ya matukio ya kandoni mwa mkutano.

Amemalizia kwa kusema "Katika Mkutano wa maji wa Umoja wa Mataifa wa 2023, jumuiya ya kimataifa iliyodhamiria imekusanyika kuleta mabadiliko sio tu kwa mustakabali wa maji bali kwa mustakabali wa dunia.”