Skip to main content

Ushirikiano ndio chachu ya ushindi kwa wote kuhusu mgogoro wa maji:UN Ripoti

Maji safi, vyoo safi na usafi wa mazingira ni muhimu kwa afya ya watoto nchini Afghanistan
© UNICEF/Omid Fazel
Maji safi, vyoo safi na usafi wa mazingira ni muhimu kwa afya ya watoto nchini Afghanistan

Ushirikiano ndio chachu ya ushindi kwa wote kuhusu mgogoro wa maji:UN Ripoti

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Maji huzusha vita, huzima moto, na ni muhimu kwa maisha ya binadamu, lakini ili kuhakikisha upatikanaji wa maji ni muhimu kuboresha ushirikiano, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumanne.

Ripoti hiyo iliyozunduliwa kuelekea mkutano wa Umoja wa Mataifa wa maji wa 2023 ulioanza leo inaangazia mada pacha za ubia na ushirikiano na imetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO).

Mambo ya muhimu inayoangazia ripoti ni njia shirikishi ambazo wahusika wanaweza kuzifanyia kazi pamoja ili kushinda changamoto zinazofanana kuhusu suala la maji.

Mkurugenzi mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay alisema."Kuna haja ya dharura ya kuanzisha mifumo madhubuti ya kimataifa ili kuzuia mzozo wa maji duniani kutoka nje ya udhibiti. Maji ni mustakabali wetu wa pamoja, na ni muhimu kuchukua hatua pamoja ili kuishiriki kwa usawa na kuisimamia kwa uendelevu."

Ulimwenguni nkote watu bilioni mbili hawana maji salama ya kunywa na bilioni 3.6 wanakosa huduma za usafi zinazosimamiwa kwa usalama,imebaini ripoti hiyo.

Idadi ya watu mijini duniani kote wanaokabiliwa na uhaba wa maji inakadiriwa kuwa na uwezekano wa kuongezeka mara mbili kutoka watu milioni 930 mwaka 2016 hadi kati ya watu bilioni 1.7 na 2.4, mwaka 2050.

Kwa mujibu wa ripoti kuongezeka kwa matukio ya ukame uliokithiri na wa muda mrefu pia kunasshinikiza mfumo wa ikolojia, na kuleta matokeo mabaya kwa aina zote za mimea na wanyama.”

Ripoti ya Maendeleo ya Maji duniani 2023
UN News
Ripoti ya Maendeleo ya Maji duniani 2023

Mgogoro wa kimataifa unakaribia

Richard Connor, mhariri mkuu wa ripoti hiyo, amewaambia waandishi wa habari katika mkutano na waandishi wa habari kwenye makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kabla ya uzinduzi huo kwamba "Hali ya kutokuwa na uhakika inaongezeka. Tusipoishughulikia, bila shaka kutakuwa na mzozo wa kimataifa,"

Amesema hayo akiashiria kuongezeka kwa uhaba ambao unaonyesha kupungua kwa upatikanaji na ongezeko la mahitaji, kutoka ukuaji wa miji na viwanda hadi kilimo, ambacho pekee kinatumia asilimia 70 ya usambazaji wa maji duniani.

Kujenga mshikamano na ushirikiano ni muhimu katika kutambua haki za binadamu za maji na kuondokana na changamoto zilizopo, amesema.

Akielezea mazingira ya uhaba huo, amesema uhaba wa maji kiuchumi ni tatizo kubwa, ambapo serikali zinashindwa kutoa huduma salama, mfano katikati ya Afrika, ambako maji yanapita.

Wakati huo huo, uhaba wa kutokuwepo kabisa kwa maji ni mbaya zaidi katika maeneo ya jangwa, ikiwa ni pamoja na kaskazini mwa India na kupitia Mashariki ya Kati.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu uwezekano wa "vita vya maji" katika uwanja wa mgogoro wa kimataifa, Bwana Connor amesema maji ambayo ni maliasili muhimu "huwa inasababisha kuwepo kwa amani na ushirikiano badala ya migogoro".

Amesisitiza kuwa “Kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ni nyenzo kuu ya kuepuka migogoro na kuongezeka kwa mivutano. Nchi 153 zinashiriki karibu mito 900, maziwa na mifumo ya chemichemi, na zaidi ya nusu wametia saini mikataba yam aji.”

Mvulana akikusanya maji kutoka kwenye bonde la ukamataji lililokarabatiwa katika jimbo la kusini mwa Sudan la White Nile.
UNEP/Lisa Murray
Mvulana akikusanya maji kutoka kwenye bonde la ukamataji lililokarabatiwa katika jimbo la kusini mwa Sudan la White Nile.

Vuta nikuvute kuhusu maji

Ikielezea kwa kina uzoefu mzuri na mbaya wa juhudi za wadau kushirikiana, ripoti inasema jinsi gani kuharakisha maendeleo katika kufikia malengo yanayohusiana na maji ya Ajenda ya 2030 kunategemea kuimarisha ushirikiano chanya, wa maana kati ya maji, usafi wa mazingira, na jumuiya za kimataifa za maendeleo.

Ubunifu wakati wa mwanzo wa janga la COVID 19 uliona ushirikiano kati ya mamlaka za afya na maji machafu, ambao ulikuwa pamoja na kuweza kufuatilia ugonjwa huo na kutoa takwimu muhimu na za wakati halisi.

“Kuanzia kwa wakazi wa mijini hadi wakulima wadogo wadogo, ushirikiano umetoa matokeo yenye manufaa kwa pande zote. Kwa kuwekeza katika jumuiya za kilimo sehemu, wakulima wanaweza kufaidika kwa njia zinazosaidia miji wanayoilisha iliyo chini ya mito.”

Maji kukauka

Mataifa na wadau wanaweza kushirikiana katika maeneo kama vile udhibiti wa mafuriko na uchafuzi wa mazingira, kushirikiana takwimu na ufadhili wa pamoja. Kuanzia mifumo ya kutibu maji machafu hadi kulinda ardhi oevu, juhudi zinazochangia kupunguza utoaji wa gesi chafuzi zinapaswa "kufungua mlango wa ushirikiano zaidi na kuongeza upatikanaji wa fedha za maji", amesema.

"Hata hivyo, jumuiya zenye maji hazitumii rasilimali hizo," amesema, akionyesha matumaini kwamba ripoti na mkutano huo unaweza kuanzisha mijadala yenye tija na matokeo ya msingi.

Johannes Cullmann, mshauri maalum wa kisayansi wa rais wa shirika la uatabiri wa hali ya hewa duniani (WMO), amesema "ni suala la kuwekeza kwa busara".

Wakati rasilimali za maji na jinsi zinavyosimamiwa zinaathiri karibu nyanja zote za maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na malengo 17 SDGs, amesema uwekezaji wa sasa lazima uongezwe mara nne ili kufikia makadirio ya kila mwaka ya dola bilioni 600 hadi trilioni moja zinazohitajika kufikia lengo la SDG 6, linalohusu maji na usafi wa mazingira.

Ameongeza kuwa "Ushirikiano ni moyo wa maendeleo endelevu, na maji ni kiunganishi chenye nguvu kubwa. Hatupaswi kujadiliana kuhusu maji, tunapaswa kujadiliana juu ya maji. Maji, baada ya yote, ni haki ya binadamu.”

Msichana mdogo huko Ninh Thuan, Viet Nam, alinawa mikono yake katika maji safi na salama.
© UNICEF/Truong Viet Hung
Msichana mdogo huko Ninh Thuan, Viet Nam, alinawa mikono yake katika maji safi na salama.

Ni muhimu kwa wote na sio bidhaa

Kwa hakika, maji yanapaswa "kusimamiwa kama manufaa ya wote, sio bidhaa", kundi la wataalam 18 wa Umoja wa Mataifa na wawakilishi maalum walisema katika taarifa ya pamoja iliyotolewa jana Jumanne.

"Kuchukulia maji kama bidhaa au fursa ya biashara kutawaacha nyuma wale ambao hawawezi kupata au kumudu bei za soko," wamesema wawakilishi hao, na kuongeza kuwa maendeleo katika lengo la SDG 6 yanaweza kutokea kwa ufanisi ikiwa jamii na haki zao za binadamu ziko katikati ya majadiliano hayo.

"Ni wakati wa kuacha mbinu ya kiteknolojia ya maji na kuzingatia mawazo, ujuzi na ufumbuzi wa watu wa asili na jumuiya za wenyeji ambao wanaelewa mifumo ya ikolojia ya ndani ya maji ili kuhakikisha uendelevu wa ajenda ya maji,"

Wataalam hao wameendelea kusema kwamba Kuuzwa kwa maji kutakatisha mafanikio ya SDGs na kutatiza juhudi za kutatua shida za maji duniani",

Wataalam hao maalum huteuliwa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, ni wataalam huru na sio wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa