Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa ni wakati wa kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi muhimu – ILO

Mhudumu wa afya safisha kituo cha nje cha kunawa mikono katika kituo cha matibabu ya dharura huko Kameza, Malawi.
© UNICEF/Thoko Chikondi
Mhudumu wa afya safisha kituo cha nje cha kunawa mikono katika kituo cha matibabu ya dharura huko Kameza, Malawi.

Sasa ni wakati wa kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi muhimu – ILO

Masuala ya UM

Baada ya janga la COVID-19 kufichua ni kwa kiasi gani jamii ilikuwa haipatii wafanyakazi muhimu thamani wanayotakiwa ikiwemo malipo ya kutosha na mazingira bora ya kazi, hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO limetoa ripoti inayosihi nchi zote duniani ziboreshe mazingira ya kazi ya watendaji hao.

Ripoti hiyo ikipatiwa jina  Mwelekeo wa Ajira Jamii mwaka 2023: Thamani ya kazi muhimu, inataja makundi manane ambamo kwayo wafanyakazi hao wanapatikana kuwa ni sekta ya afya, chakula, biashara ya rejareja, usafi na huduma za kujisafi, usafirishaji, kazi za mikono, ufundi na ukarani. 

Martha Maocha anaendesha kampuni ya kutengeneza sabuni lakini hivi karibuni ameanza kutengeneza sanitizer ambayo inasaidia kuzuia maambukizi dhidi ya COVID-19.
ILO/KB Mpofu
Martha Maocha anaendesha kampuni ya kutengeneza sabuni lakini hivi karibuni ameanza kutengeneza sanitizer ambayo inasaidia kuzuia maambukizi dhidi ya COVID-19.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watendaji katika sekta hizo walitegemewa kuliko ilivyotarajiwa wakati wa janga la coronavirus">COVID-19. 

Hata hivyo mazingira duni ya kazi na kutothaminiwa kwao kulisababisha wengi kuacha kazi na hivyo huduma za msingi kuvurugika. 

Ripoti inataka kuboreshwa kwa mazingira ya kazi na uwekezaji mkubwa kwenye sekta hizo kama njia mojawapo ya kujenga mnepo wa mtikisiko wowote. 

Mathalani katika nchi 90 ambako takwimu zimepatikana, asilimia 52 ya kazi hizo zinafanywa na wafanyakazi hao muhimu ingawa katika nchi za kipato cha juu kiwango ni asilimia 34 pekee. 

Kutokana na mazingira duni ya kazi wakati wa janga la COVID-19, wafanyakazi wengi muhimu walikufa kuliko wale wasio muhimu. 

Wanafanya kazi kwa muda mrefu huku ujira ukiwa ni chini ya theluthi mbili ya ujira wa wastani kwa saa. Na katika nchi za kipato cha juu, waajiriwa wengi kwenye sekta hii ni wahamiaji. 

Wafanyakazi katika Soko Kuu la Buenos Aires, Argentina, wakati wa janga la virusi vya corona.
UN Argentina
Wafanyakazi katika Soko Kuu la Buenos Aires, Argentina, wakati wa janga la virusi vya corona.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO Gilbert F. Houngbo anasema “watumishi wa sekta ya afya, makeshia wa maduka makubwa ya bidhaa, wasafishaji, mabaharia, wafanyakazi wa afya na wengine kwenye mnyororo wa usambazaji chakula waliendelea kufanya kazi usiku na mchana hata wakati janga lilipokuwa kiwango cha juu na wakati mwingine kwenye mazingira hatari. Kuthamini kazi yao ni kuhakikisha wanapata ujira sahihi na mazingira bora ya kazi. Kazi yenye utu ni lengo kwa wafanyakazi wote lakini ni muhimu zaidi kwa wafanyakazi hawa muhimu ambao wanatoa huduma muhimu nyakati za raha na shida.”