Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

LDC5 inaangazia michango ya wanawake na wasichana katika teknolojia, licha ya vikwazo vinavyoendelea 

Timu ya wasichana watengeneza roboti kutoka Afghanistan wakihudhuria mkutano wa LDC5 Doha
UN News/Anold Kayanda
Timu ya wasichana watengeneza roboti kutoka Afghanistan wakihudhuria mkutano wa LDC5 Doha

LDC5 inaangazia michango ya wanawake na wasichana katika teknolojia, licha ya vikwazo vinavyoendelea 

Ukuaji wa Kiuchumi

Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Nchi zenye maendeleo duni (LDC5) umeungana na ulimwengu kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake, kuadhimisha mafanikio ya wanawake na wasichana kila mahali. Wito mkali wa uwezeshaji umesikika katika Kituo kikuu cha mikutano, huku wanawake vijana wanasayansi na wavumbuzi, kama Timu ya Roboti ya Wasichana wa Afghanistan, wakihimiza: "Usikate tamaa!" 

Saa sita mchana Jumatano, LDC5 imefanya maadhimisho karibu na Maman, sanamu ya shaba na chuma cha pua ya msanii Louise Bourgeois ambayo inaonekana mara tu unapoingia katika ukumbi mkuu katika Kituo cha Mikutano cha Kitaifa cha Qatar, ambapo Mkutano umekuwa ukiendelea tangu Jumapili iliyopita.  

"Leo inapaswa kuwa siku ya kutafakari na kudhamiria kufanya vizuri zaidi, lakini pia iwe sherehe, kusherehekea mchango wa kimsingi unaotolewa na wanawake na wasichana, mara nyingi dhidi ya vikwazo, kwa mafanikio ya ulimwengu bora, "amesema Rabab Fatima, Katibu Mkuu wa Mkutano huu wa LDC5.   

Hata hivyo, amewakumbusha washiriki kwamba mabadiliko ya jamii zetu kwa ajili ya dunia bora, yenye ustawi na amani "hayawezi kutokea bila kwanza kuwawezesha wanawake na wasichana". 

Washiriki wa mkutano wa LDC5 wakiwa wamekutana mjini Doha Qatar kwenye ukumbi wa mikutano
UN News/Pengfei Mi
Washiriki wa mkutano wa LDC5 wakiwa wamekutana mjini Doha Qatar kwenye ukumbi wa mikutano

Mpango wa Utekelezaji wa Doha (DPoA) - ambao unalenga kuondoa vikwazo vya kimuundo katika ukuaji wa kina na maendeleo endelevu - "unaweza kuongeza kasi ya upatikanaji na kufungua milango ya madarasa, vyumba vya kulala na vyumba vya wafanyakazi kwa wanawake na wasichana katika LDCs zote," amesema. Bi. Fatima, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Mkutano wa LDC5. 

"Wacha tuendelee kufanya kazi kuelekea ulimwengu ambapo wanawake na wasichana wote wana ufikiaji sawa wa kila fursa." Amesema.  

Sherehe hiyo pia imeshirikisha ngoma ya kitamaduni ya Kiafrika iliyofanywa na Muda Africa, kundi la wasanii kutoka Tanzania, washindi wa Ufadhili wa Kimataifa wa UNESCO kwa ajili ya tofauti za Utamaduni, ambao huwasaidia wabunifu kuchangamkia fursa zinazotolewa na mazingira ya kidijitali.