Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna tena visingizio, Guterres anatoa wito wa mapinduzi kuzisaidia nchi cha LCD

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa tano wa Umoja wa Mataifa wanchi zenye maendeleo duni duniani LDC5 mjini Doha Qatar
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa tano wa Umoja wa Mataifa wanchi zenye maendeleo duni duniani LDC5 mjini Doha Qatar

Hakuna tena visingizio, Guterres anatoa wito wa mapinduzi kuzisaidia nchi cha LCD

Ukuaji wa Kiuchumi

Viongozi wa dunia wamekusanyika mjini Doha, Qatar kwa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa unaotaka kuharakisha maendeleo endelevu ambapo usaidizi wa kimataifa unahitajika zaidi ili kufungua uwezo kamili wa nchi zenye maendeleo duni zilizo hatarini zaidi duniani na kuzisaidia kuziweka kwenye njia ya kuelekea ustawi.

Miaka mitatu baada ya ulimwengu kuanza mapambano makubwa dhidi ya janga la  coronavirus">COVID-19, nchi zenye maendeleo duni (LDCs) ambazo tayari zinakabiliwa na vikwazo vikubwa vya kimuundo kwa maendeleo endelevu na hatari ya mshtuko wa kiuchumi na kimazingira zimejikuta zikikwama, huku kukiwa na wimbi la mzozo, kutokuwa na uhakika wa chakula, janga la mabadiliko ya tabianchi na ukosefu mkubwa wa haki duniani.

"Mifumo imelemewa au haipo kuanzia kwenye suala la afya na elimu hadi ulinzi wa kijamii, miundombinu, na kuunda fursa za ajira. Na hali inazidi kuwa mbaya zaidi,” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameuambia mkutano wa tano wa Umoja wa Mataifa kuhusu nchi zenye maendeleo duni unaojulikana kama LDC5, ambao unaofanyika katika mji mkuu wa Qatar, Doha kuanzia leo tarehe 5 hadi tarehe 9 Machi.

Bwana Guterres amesisitiza kuwa mfumo wa fedha wa kimataifa, ulioundwa na nchi tajiri ili kuhudumia maslahi yao binafsi, hauna haki kabisa kwa nchi za LDCs, ambazo zinapaswa kulipa viwango vya riba ambavyo vinaweza kuwa mara 8 zaidi ya vile vya nchi zilizoendelea.

"Leo hii mataifa 25 yanayoendelea yanatumia zaidi ya asilimia 20 ya mapato ya serikali katika kulipa madeni," mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema.

Kama matokeo, amesisitiza kuwa nchi za LDCs "zinahitaji mapinduzi ya kuungwa mkono katika maeneo matatu muhimu.”

Msaada wa haraka unahitajika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa viongozi wa nchi zenye kipato duni zaidi, LDCs mjini Doha, Qatar tarehe 4 Machi 2023
UN /Evan Schneider

Mosi, amesema nchi zilizo hatarini zaidi duniani zinahitaji msaada wa haraka ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Hii ni pamoja na kutoa angalau dola bilioni 500 kwa mwaka kwa nchi zinazoendelea, pamoja na asilimia 0.15 hadi 0.20 ya GNI kwa ajili ya msaada rasmi wa maendeleo (ODA) kutoka nchi zilizoendelea.

Kwa kuongezea, amesema juhudi za kimataifa zinapaswa kufanywa kuzuia ukwepaji wa ushuru na mtiririko haramu wa kifedha.

"Hakuna visingizio tena," Katibu Mkuu amesisitiza. "Ninatoa wito kwa washirika wa maendeleo kuunga mkono utekelezaji wa haya yanayofikiwa na mafanikio ya shabaha za DPoA," amesema, akimaanisha mpango wa utekelezaji wa kihistoria wa Doha, ambao ni mwongozo wa dhamira mpya na ushirikiano kati ya LDCs na washirika wao wa maendeleo ikiwa ni pamoja na sekta binafsi, mashirika ya kiraia, na serikali katika ngazi zote.

Zama mpya za Bretton Woods

Pili, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema, itakuwa muhimu kurekebisha mfumo wa fedha duniani kupitia zama mpya za Bretton Woods.

"Hii ni pamoja na kupanua wigo wa ufadhili wa dharura na kuunganisha vifungu vya maafa na majanga katika mkakati wa madeni.Benki za maendeleo ya Kimataifa zinapaswa kubadilisha mtindo wao wa biashara ili kuvutia mtiririko mkubwa wa fedha za binafsi katika mataifa ya LDCs."

Ameongeza kuwa "Lazima tutafute njia mpya za akili za kawaida za kupima uchumi wa nchi kama vile vigezo vya kukopesha ambavyo vinapita zaidi ya Pato la Taifa."

Mapinduzi katika msaada wa tabianchi

Nchi za LDCs ziko hatarini zaidi kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi licha ya kuchangia kiasi kidogo tu cha gesi chafuzi.

Ili kutoa msaada unaohitajika, Bwana. Guterres amezitaka nchi zilizoendelea kutimiza ahadi yao ya dola bilioni 100 kwa nchi zinazoendelea, kurahisisha upatikanaji wa fedha za hali ya hewa, kuendesha mfuko wa hasara na uharibifu, ufadhili wa kukabiliana na hali maradufu, kutunisha mfuko wa mabadiliko ya tabianchi unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na kutoa mapema mifumo ya tahadhari kwa kila mtu duniani katikia kipindi cha ndani ya miaka mitano.

Akiwa na malengo haya na mengine muhimu akilini, Katibu Mkuu amewaambia wajumbe kwamba ataandaa mkutano wa Kilele wa matarajio ya mabadiliko ya tabianchi katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mwezi Septemba ili kuondokana na maneno na kuingia kwenye vitendo na "kutoa haki ya mabadiliko ya tabianchi kwa wale walio mstari wa mbele wa janga hilo".

Csaba Kőrösi,Rais wa Baraza Kuu kikao cha 77 akihutubia kwenye mkutano wa LDC5 Doha Qarat
UN Photo/Evan Schneider
Csaba Kőrösi,Rais wa Baraza Kuu kikao cha 77 akihutubia kwenye mkutano wa LDC5 Doha Qarat

 

Timizeni ahadi zenu

"Enzi ya kuvunjika kwa ahadi lazima ikome sasa," amesisitiza mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akiendelea kwamba "Hebu tuweke mahitaji ya nchi zenye maendeleo duni mahali zinapostahili. Kwanza katika mipango yetu, katika vipaumbele vyetu na katika uwekezaji wetu.”

Tangu kuanza kwa janga la COVID-19, nchi 46 za LDCs zimekumbwa na uhaba wa rasilimali za kupambana na janga hili na kuongezeka kwa madeni ambayo yamerudisha nyuma maendeleo yao.

Pamoja na jitihada kubwa za kukabiliana na hali hizi, mtu mmoja kati ya watatu katika nchi za LDCs anaishi katika umaskini uliokithiri.

"Nina imani kwamba sote tunataka kutimiza ahadi yetu ya kufikia ajenda ya 2030 na kubadilisha uchumi wa nchi za LDCs," amesema Csaba Kőrösi, Rais wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika hotuba yake kwa viongozi wa dunia.

Ameongeza kuwa "Ili hilo lifanyike, ni muhimu kwamba nchi kuhisi umiliki halisi wa DPoA. Washirika wa maendeleo wanapaswa kuhakikisha kwamba ahadi za kusaidia LDCs kuondokana na hatari zinazowakabili zinatimizwa.”

Ushirikiano wa kweli

Bwana Kőrösi. Ameendelea kusema kwamba "Ikiwa tutaimarisha ushirikiano wa kweli, na kutumia teknolojia, na uvumbuzi, malengo yetu bado yanaweza kufikiwa ifikapo 2030, ambayo yatahitaji maamuzi yenye athari kubwa na hatua za kuleta mabadiliko.”

Hii itajumuisha kuzingatia kile ambacho taasisi za fedha za kimataifa zinapaswa kuzingatia, kupima utajiri na maendeleo endelevu, kutegemea sayansi katika kufanya maamuzi, kuhamasisha mshikamano, kuboresha viwango vya utawala, na kuelewa malengo ya pamoja ya kimataifa.

"Maendeleo haya hayatakuwa rahisi, lakini sioni chaguo lingine lililo bora zaidi kwa wanadamu," amesema Kőrösi.

Ahadi ya nchi mwenyeji wa mkutano

Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani mtawala wa Qatar akitoa hotuba yake kwenye mkutano wa LDC5 mjini Doha
UN Photo/Evan Schneider
Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani mtawala wa Qatar akitoa hotuba yake kwenye mkutano wa LDC5 mjini Doha

Mkutano wa ufunguzi wa LDC5 uliongozwa na Sheikh Tamim ibn Hamad Al Thani, mtawala wa Qatar ambaye alitangaza mchango wa kifedha wa dola milioni 60 kwa DPoA wakati wa hotuba yake kuu.

Kiongozi huyo wa taifa la Ghuba amesisitiza hitaji la mshikamano wa kimataifa katika kupambana na migogoro duniani kote.

"Kuna wajibu wa kimaadili kwa nchi tajiri na zilizoendelea kuchangia zaidi kusaidia nchi zenye maendeleo duni kukabiliana na changamoto za kimataifa tunazokabiliana nazo sasa,"

Huku changamoto ya madeni ikiwa suala muhimu kwa viongozi wa LDC5, ametoa wito wa kuzingatiwa kwa athari zake kwa nchi zenye maendeleo duni.

"Ninawaomba washirika wa maendeleo kuiga mfano wa Qatar na kuchukua hatua ya kuunga mkono utekelezaji wa mpango wa utendaji wa Doha kama sehemu ya wajibu wetu wa kibinadamu na maendeleo kwa watu wa nchi zenye maendeleo duni," amesema.

Rais wa Uturuki nchi mwenyeji wa mkutano uliopita wa Umoja wa Mataifa mwaka 2011, na waziri mkuu wa Bangladesh pia wamehutubia katika kikao cha ufunguzi.

Katika siku chache zijazo, zaidi ya viongozi wa dunia 130 na wakuu wa wajumbe watajitokeza kwenye mjadala mkuu watabadilishana mawazo kuhusu jinsi ya kushughulikia kwa pamoja changamoto za pamoja na kutafuta suluhisho la maana kwa nchi za LDCs.