Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yajengea uwezo jamii Zimbabwe kushiriki katika uhifadhi endelevu wa wanyamapori

Mtazamo wa karibu wa jaguar akipumzika ardhini.
Public domain
Mtazamo wa karibu wa jaguar akipumzika ardhini.

FAO yajengea uwezo jamii Zimbabwe kushiriki katika uhifadhi endelevu wa wanyamapori

Tabianchi na mazingira

Kesho tarehe 3 mwezi Machi ni siku ya wanyamapori duniani, siku ambayo ni fursa ya kuhamasisha uelewa kuhusu kutoweka kwa wanyamapori na kusaka majawabu. Maudhui ya mwaka huu ni Ubia katika Uhifadhi wa wanyamapori

Nchini Zimbabwe shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO, kwa kutambua kuwa idadi ya wanyamapori inaendelea kupungua kila uchao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo migongano kati ya wanyamapori na binadamu, halikadhalika ukame, linatekeleza mradi wa Usimamizi Endelevu wa Wanyamapori, SWM, kwa ushirikiano na wadau kama vile taasisi ya Ufaransa ya utafiti wa kilimo na maendeleo duniani, CIRAD, taasisi ya kimataifa ya utafiti wa misitu, CIFOR na Chama cha uhifadhi wa wanyamapori, WSC. 

Mradi ni wazo la shirika la nchi za Afrika, Karibea na PAsifiki na unafadhiliwa na Muungano wa Ulaya, kwa fedha kutoka Ufaransa.  

Mradi unatekelezwa katika eneo la Mucheni, wilaya ya Binga katika jimbo la Matebeleland Kaskazini nchin Zimbabwe na mbuga husika ni Rosslyn. 

Soundcloud

Kupitia Video ya FAO, anaonenaka Chipo Munsaka, mwenye umri wa miaka 22 ambaye ni miongoni mwa wanufaika 18 wa mafunzo kupitia mradi wa Usimamizi Endelevu wa rasilimali za Wanyamapori, SWM unaondeshwa na FAO. 

Chipo anasema, “nataka kuhifadhi maliasili zetu ili zisitumike kiholela. Vile vile nataka kupunguza mvutano kati ya binadamu na wanyama wa porini. Je ni kwa vipi? Kwa kuelimisha jamii, jinsi ya kuishi na wanyama wao na vile vile kuishi na miti yao.” 

FAO ilianzisha mradi huu baada ya kuona kuwa nchini Zimbabwe, idadi ya wanyamapori imekuwa ikipungua katika kipindi cha miaka 30 iliyopita kutokana na ukame, kutoweka kwa maeneo ya makazi ya wanyama na uuzaji wa mazao ya wanyamapori. 

Halikadhalika kitendo cha wanyamapori kuvamia mashamba na kula mazao kumeleta mvutano baina yao na jamii  bila kusahau mifugo kuliwa na wanyama pori, vyote hivyo vimesababisha changamoto kwa jamii za vijijini. 

Ushiriki sawa wa wanawake na wanaume kwenye uhifadhi wa wanyamapori 

Mradi unahamasisha ushiriki sawa wa wanawake na wanaume kwenye upitishaji wa uamuzi na usimamizi wa mipango ya kijamii ya uhifadhi wa wanyamapori. Mchango wa wanawake na wasichana kwenye usimamizi wa wanyamapori na uhakika wa upatikanaji wa chakula mara nyingi hupuuzwa ingawa wana nafasi muhimu na kubwa katika kufanikisha miradi hiyo.  

Chipo anafafanua kuwa “kazi hii zamani ilionekana kama vile ni kazi ya wanaume pekee. Lakini mimi msichana niliamua kushiriki vema katika kazi hii kwa sababu katika zama za sasa wasichana lazima washiriki katika miradi ya uhifadhi wa wanyamapori.” 

Harakati za uhifadhi wa wanyamapori katika jamii ya Mucheni hapa nchini Zimbabwe inahusisha wanawake na wanaume na mradi huu wa SWM unalenga kuwajengea uwezo wanajamii ili waweze kusimamia uhifadhi kwa uendelevu na pia wanufaike na uwepo wa wanyamapori kwenye eneo lao, badala ya wanyamapori kuwa chanzo cha matatizo.  

Chipo kupitia jukumu lake la usimamizi endelevu anasaidia kurejesha idadi ya wanyamapori na vile vile kupunguza vitisho vya kutoka kwa wanyamapori na ujangili na hivyo anasema lengo lake, “hakuna ujangili, hakuna shughuli haramu na hebu twende pamoja, hakuna wa kuachwa nyuma kwenye uhifadhi wa wanyamapori wetu na hii ni kwa maslahi yetu.” 

Hubert Boulet Mratibu wa Mradi wa SWM akiwa Roma, Italia ambako ni makao makuu ya FAO anazungumzia mradi huo na anasema, ”kwa ushirikiano na wadau, pamoja na jamii na serikali tunaandaa majawabu bunifu na yanayotekelezeka katika nchi 15. Lengo ni kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori na uhakika wa upatikanaji wa chakula.” 

FAO  inasema idadi kubwa ya wanyamapori iko nje ya maeneo ya hifadhi na hivyo kuendelea kukutana na jamii za vijijini, jambo ambalo linaweza kuleta mzozano kati ya binadamu na wanyamapori. Ili kuhamasisha pande mbili hizo kuishi pamoja ,ni muhimu kuwa na mipango ili jamii zinufaike na maliasili. 

“FAO inafanya kazi kupitia mradi wa usimamizi endelevu wa wanyamapori, ikivutia wanajamii kupunguza migongano na wanyamapori. Hatua moja ni kupitia shughuli za uhifadhi zinazofanywa na jamii, shughuli ambazo zinapatia jamii umiliki na kifuta jasho au motisha wa kuhifadhi wanyamapori.” 

Mathalani kwa pamoja wanapitisha kanuni za uwindaji wanyamapori, kuongeza upatikanaji wa bidhaa za nyama zitokanazo na ufugaji endelevu, halikadhalika ufugaji wa samaki, na kupunguza ulaji wa nyamapori kwenye miji na majiji. 

Na sasa FAO inasisitiza kuwa kujengea uwezo wanawake kutoka jamii za watu wa asili na jamii za vijijini ni muhimu zaidi katika kuhifadhi wanyamapori na kuweka hakikisho la kupata chakula kwa sababu..  “duniani kote, wanawake na wasichana ni kitovu cha jamii za vijijini. Na kwa njia nyingi wanachangia katika usimamizi endelevu wa maliasili na uhakika wa kupata chakula duniani kote. Ni kwamba wanawake wana nafasi muhimu katika uhifadhi wa wanyamapori. Wanaweza kuwa na ushawishi ni kwa vipi jamii zao zivue samaki, zilinde maeneo na zizingatie sheria za uhifadhi.” 

Na ni kwa kutambua hilo sasa ndoto ya Chipo ni kujiongeza zaidi kimasomo kwa kujiunga na Taasisi ya Uhifadhi wa wanyamapori nchini Zimbabwe ili aweze kupata diploma ya uhifadhi wa wanyamapori.