Teknolojia ya nyuklia yainua mapato ya wakulima Zimbabwe

2 Novemba 2018

Nchini Zimbabwe teknolojia ya nyuklia katika umwagiliaji na utambuzi wa kiwango cha mbolea imesaidia wakazi wa maeneo kame zaidi nchini humo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Sauti hii ya Emmanuel Chikwari, afisa kutoka taasisi ya utafiti wa kemia na udongo nchini Zimbabwe akieleza kuwa iwapo kuna ukame, kuna chakula kidogo sana cha kulisha familia na wazazi wanahaha kusaka chakula, wakiacha watoto wao bila huduma muhimu kama vile elimu.

Katika video hii iliyoandaliwa na shirika la nishati ya atomiki la Umoja wa Mataifa IAEA,  inaelezwa kuwa ukame uliokithiri unamaanisha kuwa familia katika eneo la Domboshava nchini humo hazina mazao ya ziada ya kuuza ili kujipatia kipato, na hivyo wazazi wengi hawawezi kulipa karo ya shule.

Hata hivyo IAEA ilianzisha mradi wa kutumia teknolojia ya nyuklia kutambua kiwango cha maji kutoka ardhini kinachohitajika kwa ajili ya umwagiliaji sambamba na mbolea,  ikimaanisha hakuna tena kutembea muda mrefu kusaka maji kwa ajili ya mazao.

Mfumo huu hutumia nusu ya maji ya kiwango cha maji ambacho awali wakazi wa eneo hili laDomboshava walitumia. Dadurai Nduna ni shuhuda..

 “Kabla ya kuanza kilimo cha kunyunyuzia matone ya maji , tulikuwa tunavuna  tani sita za nyanya kwa kila  nusu hekta, lakini sasa tunavuna tani 18 za nyanya kwa kila nusu hekta.”

Kutokana na mavuno mazuri, sasa familia zinaweza hata kuanza kuuza tena mazao na vilevile kulipa karo za watoto wao shuleni.

“ Mwaka jana shuleni  tulikuwa na wanafunzi 895, lakini mwaka huu tuna 960. Hii ni kutokna na kuanzishwa kwa kilimo cha kunyunyuzia maji ya matone. Kwa kweli hii ilikuwa baraka kwa shule hii.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud