Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres aiambia Afrika: Malizeni mkwamo wa kisiasa Libya

Taswira ya  Tripoli, mji mkuu wa Libya.
UNSMIL/Abel Kavanagh
Taswira ya Tripoli, mji mkuu wa Libya.

Guterres aiambia Afrika: Malizeni mkwamo wa kisiasa Libya

Amani na Usalama

Kumaliza mkwamo wa sasa wa kisiasa nchini Libya, kutatoa fursa ya kuchanua kwa maendeleo na kuondokana na mlolongo wa majanga yanayokabili taifa hilo, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo katika mkutano wa ngazi ya juu ya viongozi wa Muungano wa Afrika, AU huko Addis Ababa, Ethiopia.

Kile kinachohitajika haraka ni utashi wa kisiasa wa kuvunja mkwamo wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu na kufanikisha maendeleo katika Nyanja mbalimbali,” amesema Katibu Mkuu Guterres katika mkutano wa Kamati ya Ngazi ya Juu kuhusu Libya unaofanyika Addis Ababa.

Amesema maendeleo thabiti yanatakiwa ili hatimaye kufanyika kwa uchaguzi na kusongesha usalama, maridhiano ya kitaifa na haki za binadamu, akiongeza kuwa Umoja wa Mataifa umejizatiti kufanikisha majawabu yanayoongozwa na walibya wenyewe.

Maeneo ya kupatiwa kipaumbele

Akitambua kuwa Umoja wa Mataifa umeazimia kabisa kukabili ukosefu wa maelewano wa siku za nyuma, Katibu Mkuu ametaja maeneo ya kupatiwa vipaumbele.

“Hatuja ajenda wala lengo isipokuwa: kurejesha haki ya wananchi wa Libya ya kuishi kwa amani, kupiga kura kwenye uchaguzi huru na haki na kunufaika na ustawi wa nchi yao,” amesema Katibu Mkuu.

Changamoto ni nyingi. Jopo la Umoja wa Mataifa la kuchunguza haki za binadamu mwishoni mwa mwezi uliopita wa Januari lilipata shuhuda za mauaji ya kiholela, kuswekwa korokoroni kinyume cha sheria, usafirishaji haramu wa binadamu, utoweshwaji wa binadamu, ukimbizi wa ndani na uwepo wa makaburi walimozikwa watu wengi kwa pamoja.

Tangu mwaka 2011 alipopinduliwa Rais wa Libya, Muammar Gaddafi aliyeongoza nchi hiyo tangu mwaka 1969, taifa hilo lenye utajiri wa mafuta limegubikwa na majanga lukuki na kuweko kwa mamlaka zinazokinzana– serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, ina makao yake makuu kwenye mji mkuu Tripoli, ilhali kile kiitwacho jeshi la kitaifa la Libya, lina makao yake makuu mashariki mwa nchi hiyo.

‘Hakuna mbadala wa uchaguzi’

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia Kamati ya Ngazi ya Juu ya Muungano wa Afrika kuhusu Libya huko Addis Ababa, Ethiopia
© UNECA/Daniel Getachew
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia Kamati ya Ngazi ya Juu ya Muungano wa Afrika kuhusu Libya huko Addis Ababa, Ethiopia

Mwezi Disemba mwaka 2021, migogoro ya kisheria na changamoto nyingine zilishinikiza kufutwa kwa chaguzi za Rais na wabunge. Kushughulikia tatizo hilo kuu, Katibu Mkuu amesema Mwakilishi wake maalum anashirikisha pande kinzani nchini Libya na wadau wa kimataifa kukubaliana msingi wa kikatiba wa uchaguzi ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Februari.

“Natambua mkanganyiko na changamoto wanazozipata wananchi wa Libya,” amesema Katibu Mkuu. “Kutofanyika kwa chaguzi, kunazidi kuzorotesha ukosefu wa usalama wa kiuchumi, unaongeza ukosefu wa utulivu wa kisiasa, hatari ya kuibuka tena kwa mzozo, na unaongeza  hatari ya mgawanyiko.”

Lakini, bila mkataba, Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana kwa karibu na wadau wa karibu wa Libya, Muungano wa Afrika, wadau wa kimataifa lazima wapendekeze na wasake mifumo mbadala kuelekea kusaka suluhu. “Hakuna mbadala wa uchaguzi,” amesema Katibu Mkuu. “Chaguzi zinasalia kuwa njia halali na ya kisheria ya uongozi wa umoja.”

‘Chombo cha matumaini’

Wakati huo huo, makubaliano ya mwaka 2020 ya sitisho la mapigano bado yanaendelea kuzingatiwa, amesema Katibu Mkuu huku akipongeza hatua za kukabiliana na changamoto za usalama. Amesema jitihada hizo ni pamoja na kazi inayofanywa na kundi liitwalo “5+5’ Kamisheni ya pamoja ya kijeshi iliyoitishwa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini humo,”  akisema ni chombo kinachowakilisha matumaini ya walibya wote, bila kusahau ushiriki na msaada kutoka Muungano wa Afrika.

Kuondoka kwa wapiganaji mamluki

“Kipaumbele kifuatacho cha Kamisheni hiyo ya pamoja ya kijeshi lazima iwe kuondoka kabisa nchini Libya kwa wapiganaji wa kigeni au mamluki,” amesema Katibu Mkuu akirejelea kwamba wapiganaji hao wamechochea zaidi Libya kutumbukia kwenye mzozo.

Akikaribisha mkutano wa hivi karibuni wa huko Cairo, Misri kati ya kamisheni ya kijeshi na wawakilishi kutoka Libya, Sudan na Niger, Katibu Mkuu amesema uamuzi wa kuanzisha kamati ya uratibu na kubadilishana taarifa, ni hatua muhiu ya kuweka utulivu zaidi na amani nchini Libya na ukanda mzima.

Maendeleo kuelekea maridhiano ya kitaifa ni muhimu pia, akitaja juhudi zinazoendelea za Muungano wa Afrika za kusaidia mchakato jumuishi.

Hali tete ya haki za binadamu

Akitaja hofu kubwa kuhusu haki za binadamu, Katibu Mkuu amesema wahamiaji, wakimbizi na wasaka hifadhi wanaendelea kukumbwa na ukatili na manyanyaso huku wanaowatendea vitendo hivyo wakikwepa mkono wa sheria.

Maelfu wanaoamua kuvuka bahari ya Mediteranea wanarejeshwa Libya na kuswekwa rumande kwenye mazingira yasiyo na utu huku ikiwa ni vigumu kufikishiwa misaada ya kibinadamu.

Amesisitiza wito wake kwa nchi zote zinazohusika na suala hilo kuheshimu sheria ya kimataifa ya wakimbizi, na kwa mamlaka za Libya kusaka mbinu mbadala ya rumande, mbinu ambayo inazingatia haki za binadamu.

“Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika pamoja na watendaji na mashirika ya kikanda lazima kushirikiana kusaidia wananchi wa Libya kufikia matamanio yao ya kihalali ya kuwa na mustakabali bora wenye amani na ustawi,” amesema Katibu Mkuu.