Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukwepaji sheria waaminisha watuhumiwa wa uhalifu kuwa hawawezi kufanywa chochote- ICC

Ni nyakati za asubuhi katika kituo cha Qanfoodah wanakoshikiliwa wahamiaji na  wanaume hawa waafrika wanasubiri kuitwa majina yao ili kuthibitisha uwepo wao.
OCHA/Giles Clarke
Ni nyakati za asubuhi katika kituo cha Qanfoodah wanakoshikiliwa wahamiaji na wanaume hawa waafrika wanasubiri kuitwa majina yao ili kuthibitisha uwepo wao.

Ukwepaji sheria waaminisha watuhumiwa wa uhalifu kuwa hawawezi kufanywa chochote- ICC

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limejulishwa kuwa Mahakama ya kimataifa ya jinai, watekelezaji wa uhalifu mbaya zaidi duniani wanahamasika zaidi pale wanapoamini kuwa katu hawawezi kukumbwa na mkono wa sheria.

Kauli hiyo ya mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC, Fatou Bensouda ameitoa leo wakati akihutubia wajumbe wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Libya kwa kuzingatia azimio namba 1970 lililopitishwa na Baraza hilo mwaka 2011, likiridhia kwa kauli moja kuwasilishwa kwa suala la Libya ICC.

 Ametolea mfano wa Libya ambako amesema watuhumiwa watatu wa  uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu Saif Al-Islamu Gaddafi, Al-Tuhamy Mohamed Khaled na Mahmoud Mustafa Busayf Al-Werfalli bado  hawajafikishwa mbele ya ICC lakini mahakama hiyo ina taarifa za  uhakika za mahali waliko hivi sasa.

Mathalani Gaddafi yaaminika yuko Zintan nchini Libya ilhali Al-Tuhamy yaaminika yuko Cairo nchini Misri.

Hati za kukamatwa kwa watu hao na kufikishwa ICC zilitolewa mwaka 2011 ambapo Bi. Bensouda amesema kutotekelezwa kwa amri hiyo ya mahakama kunasababisha waathirika wa vitendo vya uhalifu kushindwa kupata haki yao kisheria.

Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Libya. (06 Novemba 2019)
UN /Manuel Elias
Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Libya. (06 Novemba 2019)

“Ingawa serikali ya Libya kwa zaidi ya mara mbili imepinga kesi hiyo kusikilizwa ICC, kitengo cha rufaa cha ICC kiisisitiza uwezo wa ICC kusikiliza kesi hiyo kwa maelezo kuwa serikali ya Libya haitazingatia haki na sheria katika kuendesha kesi dhidi ya Saif,” amesema Bi. Bensouda na kufahamisha Baraza juu ya nuru inayoonekana ya kuweza kesi hiyo kuanza kusikilizwa ICC.

Amesema kuwa kufuatia rufaa ya hivi karibuni ya Saif dhidi ya kesi yake kusikilizwa ICC, “kitengo cha rufaa ICC hivi karibuni kiliagiza kuanza kusikilizwa kwa rufaa hiyo kuanzia tarehe 11 hadi 12 mwezi huu wa novemba. Kitengo hicho kimekaribisha serikali ya Libya kuwasilisha mawazo yake kuhusu rufani hiyo kesho tarehe 7 Novemba 2019. Halikadhalika kilikaribisha Baraza hili liwe limewasilisah maoni yake kabla ya tarehe 24 ya mwezi uliopita.”

Hata hivyo amesema Baraza la Usalama liliamua kutofanya hivyo lakini serikali ya Libya na Baraza la Usalama wamekaribishwa kwenye usikiliza wa rufani hiyo wiki ijayo huko The Hague, Uholanzi, makao makuu ya ICC.

Mwendesha mashtaka huyo mkuu wa ICC amekumbusha kuwa, ‘hebu na nisisitize kuwa bila kujali hoja ya kesi kuendeshwa ICC au la, Libya inasalia na wajibu wa kumkamata na kumsalimisha Gaddafi kwenye mahakama ya ICC.”

Hii ilikuwa ni hotuba ya 8 ya mwendesha mashtaka huyo mkuu wa ICC tangu Baraza la Usalama lipitishe mwaka 2011 azimio namba 1970 ambalo liliridhia kuwasilishwa kwenye mahakama hiyo suala la Libya.

Uharibifu Tripoli, Libya.
OCHA/Giles Clarke
Uharibifu Tripoli, Libya.

Ukwepaji wa sheria washamirisha ghasia Libya

Bi. Bensouda amesema ukwepaji wa sheria ukizidi Libya, ghasia nazo zimeendelea kushika kasi nchini Libya na kwamba kumekuwepo na ongezeko la idadi ya vifo, maelfu ya watu wamekimbia makazi yao na kuna ongezeko pia la matukio ya watu kutekwa, kutoweka na kukamatwa kiholela na hivyo, “ni vyema Baraza hili na jamii ya kimataifa wakaunga mkono juhudi za kumaliza mzozo wa Libya  uliodumu kwa muda mrefu sasa.”

Pamoja na kusisitiza kuwa lazima mamlaka za Libya zichagize kumalizika kwa mzozo huo, Bi. Bensoud amesema ukwepaji sheria ambao ni kikwazo na tishio la utulivu Libya, ni lazima upatiwe suluhu.

“Ofisi yangu inaendelea kuhaha kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha haki inapatikana kwa manusura na waathirika wa vitendo vya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu nchini Libya.

Kwa upande wake Mwakilishi wa kudumu wa Libya kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Elmahdi S. Elmajerbi amesema kuwa, “serikali  yake inatambua msisitizo wa Bi. Bensouda juu ya kasi ndogo ya mahakama Libya kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya watuhumi. Hii ni kutokana na hali ya usalama Libya isababishwayo na mashambulizi ya kijeshi ambayo yalitulia lakini yameibuka tena na pia kutokana na mashambulizi dhidi ya mji wa Tripoli yanayofanywa na vikosi vya Haftar.”

Ameongeza kuwa miongoni mwa wanaosakwa na mahakama ya Libya na ICC ni watu ambao hivi sasa hawaishi nchini Libya.