Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kundi la wakimbizi kutoka Somalia waingia Ethiopia kusaka hifadhi

Wakimbizi kutoka Somalia wakiwasili katika kambi ya wakimbizi ya Burumino nchini Ethiopia. Kutokana na mvua duni, na kuendelea kwa ukosefu wa usalama nchini Somalia, idadi ya wakimbizi katika kambi hiyo iliongezeka. (Maktaba)
UNICEF/Jiro Ose
Wakimbizi kutoka Somalia wakiwasili katika kambi ya wakimbizi ya Burumino nchini Ethiopia. Kutokana na mvua duni, na kuendelea kwa ukosefu wa usalama nchini Somalia, idadi ya wakimbizi katika kambi hiyo iliongezeka. (Maktaba)

Kundi la wakimbizi kutoka Somalia waingia Ethiopia kusaka hifadhi

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya wasomali 600,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wamekimbilia kusaka hifadhi nchini Ethiopia katika mkoa wa Somali katika wiki za hivi karibuni.

Wananchi hao wamekimbia machafuko na ukosefu wa usalama katika mji wa Laascaanood mkoani Sool nchini Somalia.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini Geneva Uswisi Olga Sarrado Mur ambaye ni msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalo shughulika na wakimbizi UNHCR amesema zaidi ya nusu ya wakimbizi hao wamewasiki mapema wiki hii.

“Watu hawa wamefika wakiwa wamechoka na wakiwa na kiwewe, wamefika wakiwa na vitu vichache sana walivyoweza kubeba wakati wakikimbia kusaka usalama. Wanawake waliwaambia wafanyakazi wa UNHCR kuwa walilazimika kuuza mali zao ili kulipia usafiri ili waweze kufika maeneo yenye usalama. Wengi wao wamepoteza wapendwa wao katika mapigano hayo au wametenganishwa wakati wa kukimbia.” Amesema Sarrado.

Familia nyingi zimewekwa kwenye makazi ya muda maeneo 13 katika miji ya Bookh, Galhamur na Danot Woredasiin katika ukanda wa Doolo mkoa wa Somali nchini Ethiopia.

Shukran kwa jamii za wenyeji Ethiopia

“Katika maeneo ya pembezoni huko mbali sana ambapo kuna uwepo mdogo wa shughuli za misaada ya kibinadamu, jumuiya za wenyeji huko Doolo zimewakaribisha wakimbizi kwa ukarimu, wakigawana rasilimali walizonazo. Lakini hali hii imepungua kwa haraka kwani wastani wa watu 1,000 wanaendelea kuvuka kuingia Ethiopia kila siku.” Ameongeza msemaji huyo wa UNHCR.

Wakimbizi hawa wanapatiwa hifadhi katika baadhi ya maeneo yenye hali mbaya kutokana na ukame wa muda mrefu kutokana na kukosekana kwa mvua kwa misimu mitano mfululizo ambapo rasilimali ni chache sana.

Kukiwa na rasilimali chache familia nyingi za wakimbizi zinazowasili wamewekwa katika makazi ya muda kwenye shule na maeneo ya umma na waliokosa wamekuwa hawana namna isipokuwa kulala nje.

Watu wengi wanauhitaji wa haraka wa chakula, lishe, maji na huduma za kujisafi pamoja na huduma nyingine kutoka kwa wataalamu.

Juhudi zinazofanywa na UNHCR

Katika kuhakikisha wanashughulikia wimbi hili la wakimbizi wengi wanaoingia Ethiopia, UNHCR kwa kushirikiana na mamlaka ya kikanda ya Ethiopia ya kusaidia wakimbizi wanaorejea na wakimbizi RSS pamoja na wadau wengine wasio wa kiserikali wanashirikiana kuanzisha vituo vya mapokezi vya muda na kutoa msaada wa haraka wa kuokoa maisha.

“Misaada mingine kama Vifaa vya msaada, ikiwa ni pamoja na blanketi, ndoo, seti za kupikia jikoni, maturubai na vyandarua, tayari vimegawiwa kwa zaidi ya familia 1,000 zilizo katika mazingira magumu na UNHCR inalenga kufikia familia nyingine 9,000 katika siku zijazo.” Amesema Mur.

Uandikishwaji wa wakimbizi

Pia wakimbizi hawa mara wanapowasili wanapatiwa uangalizi wa kitabibu na kuandikishwa ili wawepo kwenye rekodi za UNHCR kabla ya Kwenda katika maeneo mbalimbali ambayo yametengwa kwa wanaowasili. Hata hivyo uandishwaji rasmi utakamilishwa hapo baadae katika maeneo mengine makubwa, uandikishwaji ambao utatoa taarifa kamili za takwimu za idadi ya watu hao.

Ndani ya Somalia, kuna zaidi ya watu 185,000 ambao wamefurushwa kutoka mji wa Laascaanood na maeneo yanayozunguka eneo hilo tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Februari, 2022.

Kulingana na mamlaka za mitaa, familia zilizohamishwa zimekaa katika maeneo 66 ndani ya Somaliland wakati wengine wamevuka hadi katika eneo la Puntland kaskazini mwa Somalia na vijiji vingine vinavyopakana na Ethiopia.

Wakimbizi wa ndani walioko Somalia

Kama njia ya awali ya kuwasaidia wakimbizi wa ndani UNHCR, kupitia washirika wake, itasambaza vitu vya msaada kwa familia 3,000 katika maeneo yaliyolengwa, na kwa sasa kunafanyika mchakato wa kutoa msaada wa fedha taslimu ili kufikia watu 42,000 kwa ajili ya kutumika kwa miezi mitatu mara tu hali ya usalama itakaporuhusu ufikiaji wa eneo hilo.

UNHCR imetoa wito kwa pande zote kuheshimu usalama wa raia na pia kutoa ombi la msaada wa ziada wa fedha ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi hawa wapya waliokimbia makazi yao.